01-Vipi Uweze Kuhifadhi Qur-aan? (كَيْفَ تَحْفَظُ الْقُرآن): Utangulizi

Vipi Uweze Kuhifadhi Qur-aan?

 

كَيْفَ تَحْفَظُ الْقُرآن؟

 

Alhidaaya.com

 

 

01-Utangulizi

 

 

01-Utangulizi:

 

Qur-aan ni maneno ya Allaah (سبحانه وتعالى), Aliyopelekewa Wahyi Nabiy Muhammad kupitia Jibriyl ‘alayhis-salaam, akawasomea Swahaba, nao wakawasomea waliofuatia, ikaendelea kusomwa na kufundishwa hadi kutufikia sisi.  Qur-aan ni Mwongozo wetu na Nuru inayonawirisha nyoyo zetu. Qur-aan ni kamba nene inayounganisha Waislamu, ni miyzani ya uadilifu, ni shifaa ya moyo ya kila aina ya maradhi; maradhi ya kufru, shirki, unafiki, uhasidi, uchoyo na ni kinga ya kila aina ya maasi na maovu. Imejaa hikma katika Aayah zake na Shariy’ah zake ambazo zinamfaa bin-Aadam wakati wowote, zama zote, na popote alipo. Amri na makatazo Yake Allaah (سبحانه وتعالى) humo pamoja na kumtii Rasuli Wake ni sababu ya furaha na kufaulu kwa bin Aadam katika dunia yake na Aakhirah yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

يَا أَيُّهَا النَّاسُ قَدْ جَاءَتْكُم مَّوْعِظَةٌ مِّن رَّبِّكُمْ وَشِفَاءٌ لِّمَا فِي الصُّدُورِ وَهُدًى وَرَحْمَةٌ لِّلْمُؤْمِنِينَ﴿٥٧﴾ قُلْ بِفَضْلِ اللَّـهِ وَبِرَحْمَتِهِ فَبِذَٰلِكَ فَلْيَفْرَحُوا هُوَ خَيْرٌ مِّمَّا يَجْمَعُونَ﴿٥٨﴾

Enyi watu! Kwa yakini yamekujieni mawaidha kutoka kwa Rabb wenu, na shifaa ya yale yaliyomo vifuani, na mwongozo na rahmah kwa Waumini. Sema: Kwa fadhila za Allaah na kwa rahmah Yake basi kwa hayo wafurahi. Hayo ni khayr kuliko wanayoyakusanya. [Yuwnus (10: 57-58)]

 

 

Lakini manufaa na fadhila hizo haziwezi kumfikia mtu isipokuwa kwa atakayeisoma Qur-aan kwa njia itakayomridhisha Allaah (سبحانه وتعالى) kama Anavyosema: 

 

الَّذِينَ آتَيْنَاهُمُ الْكِتَابَ يَتْلُونَهُ حَقَّ تِلَاوَتِهِ أُولَـٰئِكَ يُؤْمِنُونَ بِهِ ۗ

Wale Tuliowapa Kitabu wanakisoma kwa haki ipasavyo ya kusomwa kwake; hao ndio wanaokiamini. [Al-Baqarah (2: 121)]

 

Kitabu hiki In Shaa Allaah, kitaweza kumsaidia anayetaka kuhifadhi Qur-aan pindi mtu atakapoweka azimio la nguvu na kuanza kwanza Niya safi moyoni mwake na kuomba du’aa, pia kufanya juhudi kubwa ya kuendelea nayo Hifdhi yake bila ya kukata tamaa na kuithibitisha Qur-aan baada ya kuihifadhi. Hapo ndipo itakapomthibitikia kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى) iliyokariri mara nne katika Suwratul-Qamar:

 

وَلَقَدْ يَسَّرْنَا الْقُرْآنَ لِلذِّكْرِ فَهَلْ مِن مُّدَّكِرٍ ﴿١٧﴾

Na kwa yakini Tumeiwepesisha Qur-aan kwa kuikumbuka, basi je, yuko yeyote mwenye kuwaidhika? [Al-Qamar: (54: 17, 22, 32, 40)]

 

 

Namuomba Allaah (سبحانه وتعالى) Ajaalie kazi hii iwe kwa ajili ya kupata Radhi Zake Pekee na Ajaalie iwe yenye manufaa kwa ndugu zetu wa Kiislamu na namuomba Atughufurie na Atusamehe kwa makosa yoyote yatakayokuwemo. 

 

وَصَلَّ اللَّهُ عَلَى نَبِيِّنا مُحَمَّدٍ وَعَلى آلِهِ وَاَصْحَابِهِ وَسَلَّمَ تَسْلِيماً  كَثِيراً

 

 

Ummu Iyyaad

 

20 Rabiy’ul-Awwal 1434 (2 Februari 2003)

Kimehaririwa 18 Swafar 1442H (5 Oktoba 2020)

 

 

 

 

Share