05-Vipi Uweze Kuhifadhi Qur-aan? (كَيْفَ تَحْفَظُ الْقُرآن): Utaratibu Wa Kuhifadhi Qur-aan
Vipi Uweze Kuhifadhi Qur-aan?
كَيْفَ تَحْفَظُ الْقُرآن؟
05-Utaratibu Wa Kuhifadhi Qur-aan
05-Utaratibu Wa Kuhifadhia Qur-aan
Kuhifadhi Qur-aan inategemea uwezo wa mtu; kuna wanaoweza kuhifadhi ukurasa mmoja kwa dakika chache tu. Wengineo huwachukua masaa. Kulingana na uwezo wako, fuatilia utataribu ufuatao unaotumika zaidi kwa kuwa umeonekana ni muwafaka na unaoleta najita nzuri.
i-Soma Aayah unazotaka kuhifadhi uhakikishe unazisoma sawa sawa bila ya makosa yoyote.
ii-Anza kuhifadhi Aayah moja, ikithibitika moyoni, isome mara kumi.
iii-Ongeza Aayah ya pili ikithibitika soma mara kumi, kisha rudia Aayah ya mwanzo na hii ya pili usome mara kumi zote mbili.
iv-Ongeza Aayah ya tatu uhifadhi, ikithibitika, isome mara kumi, kisha rudi kuanzia Aayah ya mwanzo, ya pili na hii ya tatu usome mara kumi zote. Endelea hivyo hivyo kwa kadiri ya uwezo wako wa kuhifadhi kwa siku kama ni Aayah tatu utakomea hapo, kama una uwezo wa kuhifadhi zaidi utaendelea kwa utaratibu huo huo.
v-Usiendelee mbele hadi uwe umezithibitisha Aayah ulizozihifadhi vizuri. Ukifanya kosa urudie kuihifadhi Aayah yenye kosa hadi kusikuweko na makosa kabisa. Hatimaye Utakapoweza kuhifadhi ukurasa mzima, usikilizwe na Mwalimu na pindi ukikosea makosa zaidi ya matatu basi urudie kuzihifadhi tena ukurasa huo mpaka uthibitike. Utaratibu huu wa kurudia tokea Aayah za mwanzo na kuzirudia kusoma mara kumi au zaidi husaidia kukumbuka mfuatano wa Aayah bila ya kuipita moja katikati.
vi-Ikiwa unajihifadhisha mwenyewe, ni muhimu upate mtu akusikilize kila unapothibitisha moyoni Aayah kadhaa. Akusikilize pia unapofanya marejeo ya hifdhw ya Suwrah ulizozihifadhi.
vii-Soma kwa sauti ya kusikilizika na sio kimya kimya. Ukiwa ni peke yako, jifungie chumbani uwe huru kuisoma kwa sauti ya juu.
viii-Siku ya pili, endelea kuchukua Aayah mpya kadiri uwezavyo. Zihifadhi kwa utaratibu huo huo.
ix-Utakapomaliza, fanya marejeo ya kuzisoma Aayah ulizohifadhi mwanzo yaani jana yake, kisha unganisha na hizi mpya hadi zote zithibitike moyoni.
x-Siku ya tatu endelea hivyo hivyo, kila unapozidi kuhifadhi ndipo unapozidi kupanua ubongo wako kuweza kuhazini Aayah nyingi akilini, lakini pia ndipo kila unapohitaji muda wa kurudia Aayah za mwanzo ulizozihifadhi.
x-Kuziandika Aayah katika kitabu au ubao ni njia mojawapo iliyojaribiwa na kuonenakana imeleta natija ya kusaidia hifdhw ya Qur-aan.