04-Vipi Uweze Kuhifadhi Qur-aan? (كَيْفَ تَحْفَظُ الْقُرآن): Nasaha Za Kuhifadhi Qur-aan
Vipi Uweze Kuhifadhi Qur-aan?
كَيْفَ تَحْفَظُ الْقُرآن؟
04-Nasaha Za Kuhifadhi Qur-aan
04-Nasaha Za Kuhifadhi Qur-aan
Kabla ya kuanza kuhifadhi Qur-aan jitayarishe kutekeleza nasaha zifautazo:
i-Kutia Niya Safi (Ikhlaasw)
Anza na kutia niya ya dhati kwamba unakusudia kuhifadhi Qur-aan kwa ajili ya kupata Radhi za Allaah (سبحانه وتعالى) na kutegemea fadhila na malipo yake, na hivi ndivyo inavyopasa katika ‘ibaada na amali zote.
ii-Weka Azimio La Nguvu Bila Ya Kukata Tamaa.
Weka azimio la nguvu, usichoke, usikate tamaa wala usivunjike moyo hasa pale utakapoona kwamba unazorota katika baadhi ya Aayah au Suwrah utakazoziona ngumu. Chukua mfano wa anayetaka kupanda mlima, akaupanda polepole hadi kufikia kileleni. Hivyo basi japokuwa utakuwa unahifadhi kidogo kidogo, endelea usiache na kumbuka kauli ya Nabiy ﷺ:
((... لاَ يَمَلُّ اللَّهُ حَتَّى تَمَلُّوا وَكَانَ أَحَبَّ الدِّينِ إِلَيْهِ مَادَامَ عَلَيْهِ صَاحِبُهُ)) متفق عليه
(…Allaah Hachoki [kulipa thawabu] mpaka mchoke wenyewe. Na ‘Ibaadah Aipendayo zaidi ni ile inayodumishwa na mtendaji)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
iii-Kuomba Du'aa
Muombe Allaah (سبحانه وتعالى) Akupe tawfiyq ya kuhifadhi maneno Yake. Usiache kuomba kila mara. Tumia Wasiylah[1] na nyakati za kukubaliwa du'aa.
iv-Tambua Fadhila Za Kusoma Na Kuhifadhi Qur-aan:
Soma fadhila hizo upate hima ya kuzichuma na ikupe azimio la nguvu.
v-Kubakia Katika Taqwa:
Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۖ وَيُعَلِّمُكُمُ اللَّـهُ ۗ
Na mcheni Allaah, na Allaah Anakufunzeni. [Al-Baqarah (2: 282)]
Kwa hiyo jisafishe kwanza na madhambi kwa kuomba maghfirah na kutubia kwa Allaah (سبحانه وتعالى), kisha jiepushe na maasi yote kwani maasi yanamzuia mja kushika maneno ya Allaah (سبحانه وتعالى). Ibn Mas‘uwd (رضي الله عنه) amesema:
إِن َّالرَّجُلَ لَيُحْرَمَ العِلْمَ بِذَنْبٍ يُصِيبُه
"Hakika mtu hunyimwa elimu kwa dhambi anazozitenda"
Imaam Ash-Shaafi'iy (رحمه الله)alikuwa mwepesi wa kuhifadhi Qur-aan lakini Qur-aan ilipokuwa nzito kuihifadhi alisema:
شَكَوْتُ إلَى وَكِيعٍ سُوءَ حِفْظِي، فَأرْشَدَنِي إلَى تَرْكِ المعَاصِي . وَأخْبَرَنِي بأَنَّ العِلْمَ نُورٌ،
ونورُ اللهِ لاَ يُهْدَى لِعَاصِي
"Nililalamika kwa Wakiy’i kuhusu kushindwa kuhifadhi Qur-aan akaninasihi kuacha maasi na akanijulisha kuwa nuru ya elimu na nuru ya Allaah haimfikii mwenye kuasi"
vi-Kutoshughulika Na Anasa Za Dunia
Inampasa mwenye kutaka kuhifadhi Qur-aan atumie muda wake wote kwa ajili ya kuhifahdi Qur-aan. Ajitenge na anasa za dunia asizichanganye na kazi hii, ili akili na moyo wake upate utulivu kwa ajili ya hifdhwul-Qur-aan. Watu hupoteza wakati wao mwingi kushughulika na mambo ya upuuzi yasiyomzidishia Iymaan wala kumfaa Aakhirah yake. Fitnah zimekuwa nyingi na nyenzo zake zimekithiri; mitandao, televisheni, simu za mkono na huduma zake n.k. Wengineo hukaa mabarazani kwa maongezi au michezo ya karata n.k. Anayechanganya anasa, upuuzi n.k. na huku akitaka kuhifadhi Qur-aan hatoweza kabisa kwani Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
مَّا جَعَلَ اللَّـهُ لِرَجُلٍ مِّن قَلْبَيْنِ فِي جَوْفِهِ ۚ
Allaah Hakufanya mtu yeyote kuwa na nyoyo mbili kifuani mwake. [Al-Ahzaab: (33: 4)]
vii-Kuipa Hifdhwul-Qur-aan Kiupambele.
Katika ratiba za siku maishani mwako, lazima uipe hifdhwul-Qur-aan (kuhifadhi Qur-aan) kiupambele. Jiwekee wakati maalumu kila siku uwe kwa ajili ya kuhifadhi Qur-aan tu. Wakati bora kabisa uliotambulika kuwa ni muwafaka kuihifadhi Qur-aan ni nyakati za usiku ambako kuna ukimya na utulivu. Bali wakati mzuri kabisa ni kabla ya Alfajiri au baada ya kuswali tu Alfajiri kwa sababu hapo bongo bado liko tupu na safi na liko tayari kupokea na kuhifadhi kinachosomwa. Hilo limetambulikana kutokana na uzeofu wa waliohifadhi Qur-aan na jambo hilo halina shaka kwani kulingana na mchana, ni tofauti kabisa kwa sababu mchana kuna harakati nyingi ambazo zinaweza kukukatiza hifdhw yako; mfano watu ingia toka, simu n.k.
viii-Jifunze Kwanza Kuisoma Qur-aan Bila Ya Makosa
Inapasa mwenye kutaka kuhifadhi Qur-aan kwanza ajifunze kuisoma Qur-aan sawasawa bila ya makosa kwani unapohifadhi kosa huwa vigumu baadaye kulirekebisha. Juu ya hivyo kuisoma Qur-aan kimakosa hubadilisha na kupotosha kauli za Allaah (سبحانه وتعالى).[2]
ix-Jifunze Kuisoma Qur-aan Kwa Hukmu Za Tajwiyd
Kusoma kwa kufuata hukmu za Tajwiyd husaidia kutambua maneno yanayofuatia, mfano baada ya maddum-munfaswil (madd ya kuachana) utajua tu kwamba neno la pili litakuwa linaanzia na herufi ya hamza. Vile vile unapojifunza Tajwiyd ndipo utakapoweza kuisoma Qur-aan kwa kuitamka vizuri ipasavyo na kuvuta panapotakiwa na kufanya ghunnah[3] panapotakiwa n.k na ndipo qiraa-a cha mtu kinapokuwa kizuri.
x-Jifunze Lugha Ya Kiarabu
Muislamu anapaswa kujifunza lugha ya Kiarabu aweze kufahamu maneno ya Rabb wake. Lugha ya Kiarabu itamsadia pia mwenye kuhifadhi Qur-aan kutambua vipi kutamka neno linaloanzia au linalofuatia kwa vile maneno hubadilika kutokana na hukmu za serufi ya lugha ya Kiarabu.[4] Waislamu wengi hawatilii hima kujifunza lugha hii tukufu. Baadhi ya watu wako tayari kulipia gharama kubwa ya kujifunza lugha nyinginezo na hali lugha ya Kiarabu ndio iliyowajibika kwanza ili kuweza kufahamu maneno ya Allaah (سبحانه وتعالى) na ya Rasuli Wake ﷺ.
xi-Tumia Aina Moja Ya Mswahafu
Tumia Mswahafu wa aina moja, usichanganye Miswahafu katika kuhifadh kwa sababu mpangilio wa Suwrah zinavyoanza na kumalizikia zinatofautiana katika baadhi ya miswahafu, na hivyo hata Ayaah huwa zimetofautiana katika kupangika kwake kwenye ukurasa. Utakuta katika aina ya Mswahafu mmoja Aayah fulani imeanzia juu ya ukurasa, lakini Aayah hiyo hiyo katika aina nyingine ya Mswahafu imepangika katikati au chini ya ukurasa. Kutumia aina mbili za mswahafu kutambabaisha mwenye kuhifadhi kwa sababu mtu anapohifadhi Aayah huwa ni kama taswira (picha) iliyotua akilini na kubakia katika kumbukumbu. Ndio maana utamuona aliyehifadhi Qur-aan huwa ni sahali kwake kutambua Aayah iko sehemu gani ya ukurasa.
xii-Sikiliza Ulichohifadhi Kila Mara
Mchague Qaariu (msomaji) unayependa kumsikiza urudie kuzisikiliza Aayah ulokwishazihifadhi hadi zithibitike moyoni. Ni neema za Allaah (سبحانه وتعالى) kwamba imekuwa sahali mno zama hizi za maendeleo ya teknologia, kupata visaidizi mbali mbali vya kumsaidia mwanafuzi katika mafunzo ya Dini yake tena bila ya gharama kubwa.
xiii-Vyakula Na Miti Shamba Ya Kusaidia Kumbukumbu
Imetambulikana kuwa baadhi ya vyakula au miti shamba husaidia ubongo kuamsha kumbukumbu na kutibu usahaulifu. Tumia vyakula na miti shamba ifuatayo ambayo imethibiti katika Qur-aan na Tiba Ya Nabiy ﷺ upate natija nzuri In Shaa Allaah:
Asali, habbat-sawdaa (haba soda), lozi, tende, majani ya jarjiyr, zabibu, mafuta ya zaytuni au zaytuni zenyewe, tiyn, lubaan-adhikr (ubani wa kumbukumbu au ubani wa maji), nanaa (weka katika chai ukipenda), zaatari, tangawizi, 'arqisus (vijiti fulani vya mitishamba vinaponyesha kifua pia). Michanganyiko ifuatayo Imetambulikana kuleta manufaa:
- Saga njugu za pistachio, zabibu nyeusi, lozi, lubaan-adhikr kisha tia katika asali kiasi cha kuchanganyika vitu vyote hivyo vizuri na kula asubuhi na jioni kijiko kimoja cha chai.
- Loanisha nyuzi chache za zaafarani katika maziwa ya dafudafu, subiri ilowanike kisha kunywa.
[1] Kujikurubisha kwa Allaah (سبحانه وتعالى) kwa ‘ibaadah
[2] Rejea kitabu cha: Alhidaayah Katika Ahkaam Za Tajwiyd- Mlango wa ‘Makosa Ya Dhahiri Na Yaliyofichika’
[3] Sauti inayaotokea puani