03-Vipi Uweze Kuhifadhi Qur-aan? (كَيْفَ تَحْفَظُ الْقُرآن): Umri Muwafaka Wa Kuhifadhi Qur-aan

Vipi Uweze Kuhifadhi Qur-aan?

 

كَيْفَ تَحْفَظُ الْقُرآن؟

 

Alhidaaya.com

 

 

03-Umri Muwafaka Wa Kuhifadhi Qur-aan

 

 

 

03-Umri Muwafaka Wa Kuhifadhi Qur-aan

 

 

Umri muwafaka na bora zaidi utakaofanya sahali kuihifadhi Qur-aan ni kuanzia  utotoni kabla ya kufikia umri wa kubaleghe, kwani wakati huo vijana hushughulishwa na dunia, hasa zama hizi zilizojaa fitnah huwa si wepesi kuepukana nazo ila tu kwa Rahma ya Allaah (سبحانه وتعالى). Lakini mtoto anapokuwa angali katika umri mdogo, basi kuhifadhi kwake chochote kichwani huwa ni sahali kwa sababu bongo huwa na kumbukumbu nzuri bado na si wepesi kusahau anachokihifadhi. Imesemekana kwamba: 

 

 

"الْحِفْظُ فِي الصِّغَرِ كالنَّقْشِ عَلى الْحَجَرِ، والْحِفْظُ فِي الْكِبَرِ كالنَّقْشِ علَى الْمَاءِ"

"Kuhifadhi udogoni ni kama nakshi katika jiwe, na kuhifadhi ukubwani ni kama nakshi katika maji

 

 

(Kauli nyingine imetaja ‘Elimu udogoni ….)

 

Ina maana: Kuchonga au kuchora nakshi katika udongo uliomaji, mchoro huo hubakia milele kuwa ni alama katika jiwe litakapokauka. Ama mwenye kuchora katika maji, mchoro huo hutoweka.

 

 

Hata hivyo, haimaanishi kwamba aliyefikia umri mkubwa haitowezekana kwake kuihifadhi Qur-aan, bali mtu anapopendelea kutekeleza ‘amali hii tukufu, ajitahidi na Allaah (سبحانه وتعالى) Atamfanyia sahali kwa sababu ahadi ya Allaah (سبحانه وتعالى) katika Suwratul-Qamar haikutofautisha kati ya mtoto au mtu mzima. Wako walioihifadhi Qur-aan wakiwa na umri zaidi ya miaka arubaini. Bali imesemekana kwamba mtu aliyefikia miaka zaidi ya sabiini aliweza kuihifadhi Qur-aan. Muislamu anapaswa awe na iymaan na yakini kuhusu maneno ya Allaah (سبحانه وتعالى) na awe na dhana njema na matumaini na matarajio mazuri daima. Kufanya hivyo, itampa nguvu na azimio la kuihifadhi Qur-aan.

 

 

Hivyo ni fursa tukufu kwa Muislamu kuhifadhi Qur-aan. Lakini ikiwa fursa hii imekupita na sasa inaelekea kwamba huna uwezo wa kuhifadhi Qur-aan, basi fanya hima na juhudi kuwahifadhisha watoto wako wakiume na wakike.  Usiache fursa hii ikawapita wao pia kwani furaha yao ya kuhifadhi Qur-aan itakuwa ni furaha na fakhari kwako na kupata Radhi za Allaah (سبحانه وتعالى) na utakuwa umeshajitangulizia akiba huko Aakhera.

  

 

 

Share