01-Sifa Na Akhlaaq Za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Huruma Na Upole Wake: Hakumtaka Jibriyl Awaangamize Makafiri Waliomfukuza Na Kumtesa
Sifa Na Akhlaaq Za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Huruma Na Upole Wake:
01-Hakumtaka Jibriyl Awaangamize Makafiri Waliomfukuza Na Kumtesa
Pindi Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alporudi kutoka Twaaif ambako wakaazi wake hawakumpokea kwa wema bali walimfukuza na kumtesa; waliwatuma watoto wadogo na wendawazimu na watumwa wao wamfukuze. Wakawa wanamuandama huku wakimtukana na kumpiga mawe mpaka damu ikaanza kumtoka Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na viatu vyake vikarowa damu. Alipokuwa anarudi kuelekea Makkah katika eneo la Qarn Al-Manaazil, Jibriyl pamoja na Malaika wa majabali wakamuuliza iwapo anataka yaangushwe majabali mawili na kuwaangamiza watu wa Makkah, lakini Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikataa kutokana na huruma zake. Maelezo kama ilivyothibiti katika Hadiyth ifuatayo:
عن عَائِشَةَ ـ رضى الله عنها ـ زَوْجَ النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم حَدَّثَتْهُ أَنَّهَا قَالَتْ لِلنَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم هَلْ أَتَى عَلَيْكَ يَوْمٌ كَانَ أَشَدَّ مِنْ يَوْمِ أُحُدٍ قَالَ " لَقَدْ لَقِيتُ مِنْ قَوْمِكِ مَا لَقِيتُ، وَكَانَ أَشَدُّ مَا لَقِيتُ مِنْهُمْ يَوْمَ الْعَقَبَةِ، إِذْ عَرَضْتُ نَفْسِي عَلَى ابْنِ عَبْدِ يَالِيلَ بْنِ عَبْدِ كُلاَلٍ، فَلَمْ يُجِبْنِي إِلَى مَا أَرَدْتُ، فَانْطَلَقْتُ وَأَنَا مَهْمُومٌ عَلَى وَجْهِي، فَلَمْ أَسْتَفِقْ إِلاَّ وَأَنَا بِقَرْنِ الثَّعَالِبِ، فَرَفَعْتُ رَأْسِي، فَإِذَا أَنَا بِسَحَابَةٍ قَدْ أَظَلَّتْنِي، فَنَظَرْتُ فَإِذَا فِيهَا جِبْرِيلُ فَنَادَانِي فَقَالَ إِنَّ اللَّهَ قَدْ سَمِعَ قَوْلَ قَوْمِكَ لَكَ وَمَا رَدُّوا عَلَيْكَ، وَقَدْ بَعَثَ إِلَيْكَ مَلَكَ الْجِبَالِ لِتَأْمُرَهُ بِمَا شِئْتَ فِيهِمْ، فَنَادَانِي مَلَكُ الْجِبَالِ، فَسَلَّمَ عَلَىَّ ثُمَّ قَالَ يَا مُحَمَّدُ، فَقَالَ ذَلِكَ فِيمَا شِئْتَ، إِنْ شِئْتَ أَنْ أُطْبِقَ عَلَيْهِمِ الأَخْشَبَيْنِ، فَقَالَ النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم بَلْ أَرْجُو أَنْ يُخْرِجَ اللَّهُ مِنْ أَصْلاَبِهِمْ مَنْ يَعْبُدُ اللَّهَ وَحْدَهُ لاَ يُشْرِكُ بِهِ شَيْئًا ".
Amesimulia ‘Aaishah Mke wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa alimuuliza Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): Hivi imekupitia siku iliyo ngumu zaidi ya siku ya Uhud? Akasema: “Nimepata mateso niliyo yapata kutoka kwa jamaa zako, na mateso zaidi niliyoyapata kwao ni siku ya ‘Aqabah, pale nilipojipeleka mwenyewe kwa Ibn ‘Abd Yaaliyl ibn ‘Abd Kulaal. Hakunikubalia nilicho kitaka. Nikaondoka sielewi niendako, sikuzinduka isipokuwa nilipokaribia Qarn Ath-Tha‘alib, nikainua kichwa change nikaliona wingu limenifunika, nikaangalia nikamkuta humo Jibriyl, akaniita akasema: ‘Hakika Allaah Ameisikia kauli ya watu wako kwako na jibu walilokupa, na Amekuletea Malaika wa milima ili umuamuru unachotaka katika adhabu kuwafikia jamaa zako’. Akaniita Malaika wa milima, akanisalimia, kisha akasema: ‘Ee Muhammad!’ Akasema: ‘Ikiwa ni katika unachokitaka niwafunike kwa milima miwili’. Akasema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): “Bali nataraji Allaah atawatoa migongoni mwao watakao mwabudu Allaah Peke Yake, hawamshirikishi na chochote.” [Al-Bukhaariy, Muslim]