02-Sifa Na Akhlaaq Za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Huruma Na Upole Wake: Mwenye Moyo Laini Si Mkali Wala Si Mjeuri
Sifa Na Akhlaaq Za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Huruma Na Upole Wake:
02-Mwenye Moyo Laini Si Mkali Wala Si Mjeuri
Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa mpole, mwenye moyo laini wa huruma na hakuwa mkali wala mjeuri kwa Swahaba zake. Amejaaliwa kuwa hivyo kutokana na Rahmah ya Allaah (سبحانه وتعالى) kama Anavyosema:
فَبِمَا رَحْمَةٍ مِّنَ اللَّـهِ لِنتَ لَهُمْ ۖ وَلَوْ كُنتَ فَظًّا غَلِيظَ الْقَلْبِ لَانفَضُّوا مِنْ حَوْلِكَ ۖ فَاعْفُ عَنْهُمْ وَاسْتَغْفِرْ لَهُمْ وَشَاوِرْهُمْ فِي الْأَمْرِ ۖ فَإِذَا عَزَمْتَ فَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ ۚإِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الْمُتَوكِّلِينَ ﴿١٥٩﴾
Basi ni kwa rahmah kutoka kwa Allaah umekuwa mpole kwao (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم). Na lau ungelikuwa mjeuri mwenye moyo mgumu wangelitawanyika mbali nawe. Basi wasamehe na waombee maghfirah na washauri katika mambo. Na unapoazimia basi tawakali kwa Allaah. Hakika Allaah Anapenda wanaotawakali. [Aal-‘Imraan: 159]
Imaam Ibn Kathiyr amesema kuhusu kauli hiyo: “Yaani ungelikuwa na maneno maovu ya ujeuri, na moyo mgumu kwao basi wangelikutenga na kukukimbia, lakini Allaah (سبحانه وتعالى) Amewaunganisha kwako na kukufanya uwe mwema na laini kwao ili mioyo yao iunganike nawe.” Na ‘Abdullaah bin ‘Amr amesema kuwa alisoma sifa za Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) katika Vitabu (Vya Mbinguni) vilivyotangulia kwamba: "Yeye si mjeuri, si mwenye moyo mgumu, si mfidhuli sokoni na halipizi maovu kwa maovu bali anasamehe na kupuuza.”
Na ndio maana alikuwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) anawafanyia Swahaba zake wepesi katika mambo yao ya Dini kama ilivyothibiti katika Hadiyth ifuatayo:
عَنْ عَائِشَةَ، قَالَتْ مَا خُيِّرَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم بَيْنَ أَمْرَيْنِ أَحَدُهُمَا أَيْسَرُ مِنَ الآخَرِ إِلاَّ اخْتَارَ أَيْسَرَهُمَا مَا لَمْ يَكُنْ إِثْمًا فَإِنْ كَانَ إِثْمًا كَانَ أَبْعَدَ النَّاسِ مِنْهُ .
‘Aaishah (رضي الله عنها) amesema: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) hakupewa khiyari ya mambo mawili ila alichagua lilokuwa wepesi kati ya hayo mawili madamu si dhambi. Na kama (hilo la wepesi lilikuwa) ni dhambi, basi alikuwa mbali mno na jambo hilo kuliko watu watu. [Muslim]
Na sifa zake na huruma zake kwa Swahaba Anazitaja Allaah (سبحانه وتعالى) katika kauli Yake:
لَقَدْ جَاءَكُمْ رَسُولٌ مِّنْ أَنفُسِكُمْ عَزِيزٌ عَلَيْهِ مَا عَنِتُّمْ حَرِيصٌ عَلَيْكُم بِالْمُؤْمِنِينَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ﴿١٢٨﴾
Kwa yakini amekujieni Rasuli anayetokana na nyinyi wenyewe, yanamtia mashaka (na huzuni) yanayokutaabisheni, anakujalini, mwenye huruma kwa Waumini ni mwenye huruma mno, mwenye rahmah. [At-Tawbah: 128]