033-Asbaabun-Nuzuwl: Al-Ahzaab Aayah 53: يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَدْخُلُوا بُيُوتَ النَّبِيِّ إِلَّا أَن يُؤْذَنَ لَكُمْ
أسْبابُ النُّزُول
Asbaabun-Nuzuwl
(Sababu Za Kuteremshwa Suwrah Na Aayaat Za Qur-aan)
Imekusanywa na: Alhidaaya.com
033-Asbaabun-Nuzuwl Al-Ahzaab Aayah 53
Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى):
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَدْخُلُوا بُيُوتَ النَّبِيِّ إِلَّا أَن يُؤْذَنَ لَكُمْ إِلَىٰ طَعَامٍ غَيْرَ نَاظِرِينَ إِنَاهُ وَلَـٰكِنْ إِذَا دُعِيتُمْ فَادْخُلُوا فَإِذَا طَعِمْتُمْ فَانتَشِرُوا وَلَا مُسْتَأْنِسِينَ لِحَدِيثٍ ۚ إِنَّ ذَٰلِكُمْ كَانَ يُؤْذِي النَّبِيَّ فَيَسْتَحْيِي مِنكُمْ ۖ وَاللَّـهُ لَا يَسْتَحْيِي مِنَ الْحَقِّ ۚ وَإِذَا سَأَلْتُمُوهُنَّ مَتَاعًا فَاسْأَلُوهُنَّ مِن وَرَاءِ حِجَابٍ ۚ ذَٰلِكُمْ أَطْهَرُ لِقُلُوبِكُمْ وَقُلُوبِهِنَّ ۚ وَمَا كَانَ لَكُمْ أَن تُؤْذُوا رَسُولَ اللَّـهِ وَلَا أَن تَنكِحُوا أَزْوَاجَهُ مِن بَعْدِهِ أَبَدًا ۚ إِنَّ ذَٰلِكُمْ كَانَ عِندَ اللَّـهِ عَظِيمًا ﴿٥٣﴾
Enyi walioamini! Msiingie nyumba za Nabiy isipokuwa mkipewa idhini ya kwenda kula si kungojea kiive. Lakini mtakapoitwa, basi ingieni, na mkimaliza kula, tawanyikeni, na wala msikae kujiliwaza kwa mazungumzo. Hakika hiyo ilikuwa inamuudhi Nabiy, naye anakustahini, lakini Allaah Hasitahi (kubainisha) haki. Na mnapowauliza wake zake haja, waulizeni nyuma ya pazia. Hivyo ni utwaharifu zaidi kwa nyoyo zenu na nyoyo zao. Na haipasi kwenu kumuudhi Rasuli wa Allaah. Na wala kuwaoa wake zake baada yake abadani. Hakika jambo hilo mbele ya Allaah ni kubwa mno. [Al-Ahzaab (33:53)]
Sababun-Nuzuwl:
حَدَّثَنَا إِسْحَاقُ بْنُ مَنْصُورٍ، أَخْبَرَنَا عَبْدُ اللَّهِ بْنُ بَكْرٍ السَّهْمِيُّ، حَدَّثَنَا حُمَيْدٌ، عَنْ أَنَسٍ رضى الله عنه قَالَ أَوْلَمَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم حِينَ بَنَى بِزَيْنَبَ ابْنَةِ جَحْشٍ فَأَشْبَعَ النَّاسَ خُبْزًا وَلَحْمًا ثُمَّ خَرَجَ إِلَى حُجَرِ أُمَّهَاتِ الْمُؤْمِنِينَ كَمَا كَانَ يَصْنَعُ صَبِيحَةَ بِنَائِهِ فَيُسَلِّمُ عَلَيْهِنَّ وَيَدْعُو لَهُنَّ وَيُسَلِّمْنَ عَلَيْهِ وَيَدْعُونَ لَهُ فَلَمَّا رَجَعَ إِلَى بَيْتِهِ رَأَى رَجُلَيْنِ جَرَى بِهِمَا الْحَدِيثُ، فَلَمَّا رَآهُمَا رَجَعَ عَنْ بَيْتِهِ، فَلَمَّا رَأَى الرَّجُلاَنِ نَبِيَّ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم رَجَعَ عَنْ بَيْتِهِ وَثَبَا مُسْرِعَيْنِ، فَمَا أَدْرِي أَنَا أَخْبَرْتُهُ بِخُرُوجِهِمَا أَمْ أُخْبِرَ فَرَجَعَ حَتَّى دَخَلَ الْبَيْتَ، وَأَرْخَى السِّتْرَ بَيْنِي وَبَيْنَهُ وَأُنْزِلَتْ آيَةُ الْحِجَابِ
Ametuhadithia Is-haaq bin Mansuwr, ametueleza ‘Abdullaah bin Bakr As-Sahmiy, ametuhadithia Humayd toka kwa Anas (رضي الله عنه) ambaye amesema: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alifanya walima ya mikate na nyama, watu wakala wakashiba hadi kusaza wakati alipomwoa Zaynab bint Jahsh. Kisha akatoka kwenda kwenye nyumba za (Wakeze) Mama wa Waumini kama ilivyokuwa ada yake asubuhi ya kila baada ya sherehe ya harusi yake, akawasalimia na kuwaombea, na wao wakamsalimia na kumwombea. Aliporudi nyumbani kwake, aliwakuta watu wawili wamezama kwenye maongezi. Alipowaona, alirudi na hakuingia nyumbani. Watu wale wawili walipomwona Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amerudi na hakuingia nyumbani kwake, walinyanyuka haraka na kuondoka. Nami (Anas) sikumbuki kama ni mimi niliyemweleza kuwa washaondoka au alielezwa na mtu mwingine. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akarejea akaingia nyumbani na akateremsha pazia kati yangu na yeye, na Aayah ya hijaab ikateremshwa.”
[Al-Bukhaariy Mujallad 10 ukurasa wa 149]
Na Ibnu Abiy Marmaa amesema: “Ametueleza Yahyaa, amenihadithia Humayd ambaye amemsikia Anas toka kwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم).
[Al-Bukhaariy ameikhariji Hadiyth hii mwahala kadhaa katika Swahiyh yake ukiwemo ukurasa wa 147 wa kifungu hichi ambapo ameeleza akisema: Na hapo Allaah Akateremsha:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَدْخُلُوا بُيُوتَ النَّبِيِّ
Enyi walioamini! Msiingie nyumba za Nabiy.
Pia katika ukurasa wa 148, Mujallad wa 11 kurasa za 134 na 139, ukurasa wa 519, na Mujallad wa 13 ukurasa wa 259 na ukurasa wa 305]
[Kadhalika, imekharijiwa na Muslim katika Mujallad wa 9 kurasa za 229, 230, 232 na 233 kwa matamshi na Isnaad tofauti toka kwa Anas. Vile vile At-Tirmidhiy katika Mujallad wa 8 kurasa za 168 na 169. Riwaayah ya kwanza amesema ni Hasan, na ya pili ni Hasan Swahiyh].
[Aidha, Ahmad ameikhariji katika Mujallad wa 3 kurasa za 105, 168, 169, 242, na 246. Pia Al-Bukhaariy katika Al-Adab Al-Mufrad katika ukurasa wa 632. Vile vile Ibn Sa‘ad katika At-Twabaqaat Mujallad wa 1 ukurasa wa 75, Ibn Jariyr katika Mujallad wa 22 kurasa za 37 na 38, na Al-Haakim katika Mujallad wa 2 ukurasa wa 418 ambapo amesema Isnaad yake ni Swahiyh. Adh-Dhahabiy ameikubali.
حَدَّثَنَا إِسْحَاقُ، أَخْبَرَنَا يَعْقُوبُ، حَدَّثَنَا أَبِي، عَنْ صَالِحٍ، عَنِ ابْنِ شِهَابٍ، قَالَ أَخْبَرَنِي عُرْوَةُ بْنُ الزُّبَيْرِ، أَنَّ عَائِشَةَ رضى الله عنها زَوْجَ النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم قَالَتْ كَانَ عُمَرُ بْنُ الْخَطَّابِ يَقُولُ لِرَسُولِ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم احْجُبْ نِسَاءَكَ. قَالَتْ فَلَمْ يَفْعَلْ، وَكَانَ أَزْوَاجُ النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم يَخْرُجْنَ لَيْلاً إِلَى لَيْلٍ قِبَلَ الْمَنَاصِعِ، خَرَجَتْ سَوْدَةُ بِنْتُ زَمْعَةَ، وَكَانَتِ امْرَأَةً طَوِيلَةً فَرَآهَا عُمَرُ بْنُ الْخَطَّابِ وَهْوَ فِي الْمَجْلِسِ فَقَالَ عَرَفْتُكِ يَا سَوْدَةُ. حِرْصًا عَلَى أَنْ يُنْزَلَ الْحِجَابُ. قَالَتْ فَأَنْزَلَ اللَّهُ عَزَّ وَجَلَّ آيَةَ الْحِجَابِ.
Ametuhadithia Is-haaq, ametuhadithia Ya’quwb aemtuhadithia baba yangu, kutoka kwa Swaalih kutoka kwa Ibn Shihaab, amesema: amenijulisha ‘Urwah bin Zubayr kwamba ‘Aaishah (رضي الله عنها)mke wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ambaye amesema: ‘Umar bin Al-Khattwaab alikuwa akimwambia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم): Wavalishe Wakezo hijaab (au waamuru wasitoketoke). (‘Aaishah anaendelea kusema): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) hakufanya hilo, na Wake wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) walikuwa wanatoka usiku kwa usiku nje kidogo ya mji kwenda kujisaidia. Sawdah bint Zum ‘ah ambaye alikuwa mwanamke mrefu (wa kupambanuka) akatoka, na ‘Umar akamwona akiwa barazani. Akamwambia: “Tumekutambua ee Sawdah”, kuonyesha pupa na hamu ya kuteremshwa amri kwa wanawake kuvaa hijaab. Na Allaah (عز وجل) Akateremsha Aayah ya hijaab.
[Al-Bukhaariy, Muslim]
Na pia,
عَنْ عَائِشَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا قَالَتْ: كُنْتُ آكُلُ مع النَّبيِّ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم حَيْسًا في قَعْبٍ فمرَّ عُمَرُ فدعاه فأكَل فأصابَتْ إِصبَعَه إِصبَعي فقال حسن أوَّهْ أوَّهْ لو أُطاعُ فيكنَّ ما رأَتْكنَّ عَينٌ فنزَلَتْ آيةُ الحِجابِ
Toka kwa ‘‘Aaishah (رضي الله عنها) amesema: “Nilikuwa nakula pamoja na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) katika “qa‘ab” (sahani ya mbao au jiwe). ‘Umar akapita na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akamkaribisha chakula. Akakaa kula pamoja nasi, na kidole chake kikagusana na kidole changu (ndani ya sahani). Akasema: Aw! Aw! Ningelikuwa na amri na mamlaka juu yenu, basi jicho (la wanaume) lisingeliwaona. Na hapo ikateremka Aayah ya hijab.”
[Adab Al-Mufrad, At-Twabaraaniy ameikhariji katika As-Swaghiyr Mujallad wa 1 ukurasa wa 83, na Al-Haythamiy akainasibisha kwa Al-Awsatw katika Mujallad wa 7 ukurasa wa 93 na kusema wapokezi wake ni wapokezi wa As-Swahiyh isipokuwa Muwsaa bin Abiy Kathiyr, naye ni Thiqah (mwema mwadilifu na mdhibiti wa kifua na maandiko)].
Njia Ya Kuoanisha Kati Ya Riwaayah Hizi
Al-Haafidh katika Al Fat-h Mujallad wa 1 ukurasa wa 260 amesema: “Njia ya kuoanisha kati ya Riwaayah mbili ni kwa kusema kuwa sababu ya kuteremka (amri ya) hijaab si moja bali ni sababu kadhaa, na kisa cha Zaynab kilikuwa ndicho cha mwisho. Au kusema kuwa muradi wa Aayah ya hijaab katika baadhi ya Riwaayah ni Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى):
يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِن جَلَابِيبِهِنَّ
wajiteremshie jilbaab zao. [Al-Ahzaab (33:59)]
Nami (Muqbil Al-Waadi’iyy) nasema, kunahitajika utafiti zaidi katika kusema kuwa muradi wa Aayah ya hijaab ni Kauli Yake Ta’aalaa:
يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِن جَلَابِيبِهِنَّ
…kwani Riwaayah zinazozungumzia kisa cha Zaynab zimeeleza kuwa Aayah iliyoshuka kuamuru hijaab ni Kauli Yake Ta’aalaa:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَدْخُلُوا بُيُوتَ النَّبِيِّ
Enyi walioamini! Msiingie nyumba za Nabiy. [Al-Ahzaab (33:53)]
Na kuhusiana na kauli ya ‘Umar, maelezo zaidi yako katika Mujallad wa Kumi na Mbili wa Tafsiyr ya At-Twabariy.
Al-Haafidh katika Al Fat-h Mujallad wa Kwanza ukurasa wa 260 amesema kuwa Abu ‘Awwaanah ameongeza katika Swahiyh yake kwa Isnaad ya Az-Zubaydiy toka kwa Ibn Shihaab akisema: ”Allaah Akateremsha Aayah ya hijaab:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَدْخُلُوا بُيُوتَ النَّبِيِّ
Enyi walioamini! Msiingie nyumba za Nabiy. “ [Al-Ahzaab (33:53)]
Hivyo basi, kusema kuwa sababu ni tofauti tofauti za kuteremka Aayah ya hijaab ni bora zaidi.
Angalizo Muhimu
Tunafahamu kutokana na Hadiyth hii kuwa ‘Umar kumwambia Sawdah: “Tumekutambua ee Sawdah”, kulikuwa ni kabla ya hijaab, na katika baadhi ya Riwaayah nyingine inaelezwa kuwa ilikuwa ni baada ya hijab. Kutokana na mielekeo hii miwili ya kabla na baada, vipi tunaweza kuioanisha? Al-Haafidhw katika Al Fat-h Mujallad wa 10 ukurasa wa 150 amesema: “Al-Karmaaniy amesema: Ikiwa utasema kuwa uhalisia hapa unaonyesha kuwa ilikuwa baada ya kufaradhishwa hijaab wakati huko nyuma katika mlango wa wudhuu ilielezwa kuwa ilikuwa kabla ya hijaab, basi jibu ni kwamba huenda tukio lilitokea mara mbili (kabla na baada)”.
Ameongeza kusema: “Bali muradi wa hijaab ya kwanza si wa hijaab ya pili. Na tunaloambulia ni kuwa ‘Umar (Radhwiya Allaah ‘anhu) alipatwa na uchungu moyoni mwake kutokana na ajaanib kuwaona na kuwaangalia Wake wa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) (bila hijab) mpaka akathubutu kumwambia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم): Waamuru Wakezo wavae hijaab. Na akalisisitizia hilo mpaka ikateremka Aayah ya hijaab. Kisha akapania zaidi kwa hilo kuwa wasidhihirishe mikatiko ya miili yao kabisa hata kama wamejisitiri. Hapo akachupa mipaka, na akazuiwa. Wanawake wakaruhusiwa watoke kwa ajili ya haja zao ili kuwaondoshea uzito na tabu.”