58-Fadhila Za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Masiyh Dajjaal Haingii Katika Mji Wake Madiynah
Fadhila Za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)
58-Masiyh Dajjaal Haingii Katika Mji Wake Madiynah
Pindi atakapotokeza Masiyh Dajjaal kama ni alama mojawapo kubwa za Qiyaamah, ataenea ulimwengu mzima isipokuwa mji wa Madiynah kutokana na utukufu wa mji huu na utukufu wake Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم). Hadiyth kadhaa zimetaja kuhusu Masiyh Dajjaal na fitnah zake miongoni mwazo ni hizi zinazotaja kutokuweza kuingia Madiynah:
عن أَنَس بْن مَالِكٍ رضى الله عنه عَنِ النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم قَالَ " لَيْسَ مِنْ بَلَدٍ إِلاَّ سَيَطَؤُهُ الدَّجَّالُ، إِلاَّ مَكَّةَ وَالْمَدِينَةَ، لَيْسَ لَهُ مِنْ نِقَابِهَا نَقْبٌ إِلاَّ عَلَيْهِ الْمَلاَئِكَةُ صَافِّينَ، يَحْرُسُونَهَا، ثُمَّ تَرْجُفُ الْمَدِينَةُ بِأَهْلِهَا ثَلاَثَ رَجَفَاتٍ، فَيُخْرِجُ اللَّهُ كُلَّ كَافِرٍ وَمُنَافِقٍ ".
Amesimulia Anas bin Maalik (رضي الله عنه) kuwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakuna mji hata mmoja ambao Dajjaal hatoingia isipokuwa Makkah na Madiynah, na hakutakuwa na njia (za Makkah na Madiynah) ila watasimama kwa safu Malaika wakiilinda dhidi yake. Kisha Madiynah itatetemeka mitetemeko mitatu pamoja na watu wake, hapo Allaah Atawatoa makafiri na wanafiki wote kwayo.”
Pia,
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رضى الله عنه قَالَ قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم. " عَلَى أَنْقَابِ الْمَدِينَةِ مَلاَئِكَةٌ، لاَ يَدْخُلُهَا الطَّاعُونُ وَلاَ الدَّجَّالُ ".
Amesimulia Abu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Katika milango inayoingia Madiynah kuna Malaika wenye kulinda njia zake. Madiynah haingiwi na tauni wala Dajjaal.” [Al-Bukhaariy, Muslim]
Pia,
عَنْ أَبِي بَكْرَةَ رضى الله عنه عَنِ النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم قَالَ " لاَ يَدْخُلُ الْمَدِينَةَ رُعْبُ الْمَسِيحِ الدَّجَّالِ، لَهَا يَوْمَئِذٍ سَبْعَةُ أَبْوَابٍ، عَلَى كُلِّ باب مَلَكَانِ ".
Amesimulia Abu Bakrah (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Madiynah haitafikiwa na khofu itakayoletwa na Al-Masiyh Dajjaal. Na wakati huo Madiynah itakuwa na milango saba, kila mlango utakuwa na Malaika wawili, wanaolinda.”
Maelezo mafupi kuhusu Masiyh Dajjaal:
Masiyh Ad-Dajjaal ni mtu miongoni mwa wana wa Aadam. Atadhihiri duniani akiwa ni alama kubwa mojawapo za Qiyaamah. Sifa zake kadhaa zimetajwa miongoni mwazo ni kwamba atakuwa ni mtu mwenye jicho moja na baina ya macho yake kuna herufi zisizoungana za ك ف ر (ka fa ra) au كافر (kaafir) kwa herufi za kuungana. Kila Muislamu anayejua kusoma au asiyejua kusoma ataweza kusoma neno hilo.
Atakuja kuwafitinisha watu na fitnah yake itakuwa ni fitnah kubwa kabisa haijapata kutokea tangu Allaah (‘Azza wa Jalla) kumuumba Aadam kwa sababu Allaah Atamjaalia uwezo wa kufanya miujiza mikubwa ambayo itawashangaza na kuwachanganya watu wasio na iymaan. Ama Waumini hawatapotoshwa na Masiyd Dajjaal. Na ndio maana Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akaifanya du’aa ya kujikinga na fitnah za Masiyh Dajjaal katika Swalaah kuwa ni jambo la muhimu mno.