18-Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu Na Sharh Yake: Rahmah Na Kutengenekewa Mambo

Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu

 

Na Sharh Yake

 

Alhidaaya.com

 

18- Rahmah Na Kutengenekewa Mambo

 

 

"رَبَّنَا آتِنَا مِن لَّدُنكَ رَحْمَةً وَهَيِّئْ لَنَا مِنْ أَمْرِنَا رَشَدًا"

 

“Rabb wetu! Tupe kutoka Kwako rahmah, na Tutengenezee katika jambo letu mwongozo wa sawa.  [Al-Kahf: (18)]

 

Hii ni du’aa ya vijana waliokimbilia pangoni (Ahlul Kahf).  Walikimbilia huko kuokoa dini yao na iymaan yao kutokana na watu wao, ili wasije kuwakamata, wakawatesa na kuiingiza iymaan yao katika hatari.  Walipoingia ndani, walimwomba Allaah Ta’aalaa kwa unyenyekevu wa hali ya juu kabisa Awape rahmah maalum kutoka Kwake, kwa kuwa viumbe vyote viko ndani ya Rahmah ya Allaah.  Hivyo wakaomba rahma maalum kwa ajili yao kutokana na hali yao ngumu ya kuandamwa na makafiri.  Wakamwomba pia Awarahisishie jambo lao hilo la kufikia kwenye njia ya uongofu na ulingamanifu katika maneno na vitendo.

 

 

Tunapata faida zifuatazo kutokana na du’aa hii:

 

 

1-  Muislamu anatakiwa aondoke au akimbie toka sehemu ambayo hawezi kutekeleza maamrisho ya dini yake kwa mujibu wa hali.  Hilo ni katika nyajibu kubwa.

 

2-  Mwenye kuacha jambo kwa ajili ya Allaah, Allaah Humpa badali bora kuliko jambo aliloliacha.

 

3-  Mwenye kumcha Allaah, Allaah Humpa fumbuzi za matatizo yake, na Humruzuku kwa njia asiyoitarajia.

 

4-  Mja anatakiwa atumie nyenzo za kidunia na kisharia ili kufanikisha malengo yake.  Vijana hao badala ya kusubiri, walichakarika na kukimbia, kisha wakamwomba Allaah Awakunjulie Rahmah Zake maalum kwao.

 

5-  Rahmah za Allaah ziko aina mbili:  Rahmah jumuishi kwa viumbe wote; Waumini na makafiri, na Rahmah maalum kwa Waja Wake wema.  Muislamu anatakiwa amwombe Allaah daima Rahmah hii maalum itokayo kwenye Hazina Zake.

 

6-  Du’aa inatakiwa iende sambamba na mchakariko.  Walikimbilia pangoni kujificha, kisha wakaelekea kwa Allaah kumwomba.

 

7-  Malipo ni kwa mujibu wa kitendo.  Wao walilinda iymaan yao, na Allaah Akawalindia iymaan yao na miili yao isiharibike ndani ya pango.

 

8-  Du’aa iwe ndiyo kazi ya muumini katika majukumu yake yote katika maisha yake.

 

9-  Du’aa za kisharia zinakusanya kila analolitamani mja katika dini yake na dunia yake.  Hivyo basi Muislamu anatakiwa azitumie na ashikamane nazo kuliko du’aa za kutungwa

 

 

Share