19-Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu Na Sharh Yake: 19-Kukunjuliwa Kifua Na Kuwepesishiwa Jambo

 

Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu

 

Na Sharh Yake

 

Alhidaaya.com

 

19-Kukunjuliwa Kifua Na Kuwepesishiwa Jambo

 

 

 "رَبِّ اشْرَحْ لِي صَدْرِي* وَيَسِّرْ لِي أَمْرِي* وَا حْلُلْ عُقْدَةً مِّن لِّسَانِي * يَفْقَهُوا قَوْلِي"

 

Rabb wangu!  Nikunjulie kifua changu  •  Na  Niwepesishie shughuli yangu •  Na Fungua fundo (la kigugumizi) katika ulimi wangu  •  Ili wafahamu kauli yangu”.  [Twaahaa : (25-28)]

 

 

Hii ni du’aa ya Nabiy Muwsaa (‘Alayhis Salaam).  Alimwomba Allaah kutokana na jambo kubwa wakati Allaah Alipomwamuru aende kumlingania kafiri mkubwa zaidi duniani, aliyechupa mipaka na mwenye nguvu kubwa za jeshi na zana.  Naye ni Fir-‘awn aliyedai uungu kwa uongo na uzushi.

 

Na kutokana na umuhimu mkubwa wa jukumu lenyewe na hatari yake, alimwomba Allaah Amsaidie na Amwepesishie.  Kwani du’aa ni silaha ya Muumini ambayo anaombea kwayo msaada huku akiegemeza dhana njema kwa Allaah Ta’aalaa.

 

Akamwomba Amkunjulie kifua chake kwa nuru, iymaan na hekima ili aweze kubeba adha zote za maneno na vitendo toka kwa Fir-‘awn.  Kifua kinapokunjuka, hugeuza mazito ya jukumu kuwa pumziko na wepesi.

 

Akamwomba Amsahilishie kila jambo analolipitia, kila njia anayoikusudia kufikia kwa Allaah, na mazito yote yaliyo mbele yake.

 

Na kwa vile ufasaha wa ulimi ni nyenzo kubwa ya kufikisha ujumbe, Nabiy Muwsaa (‘Alayhis Salaam) alimwomba Allaah Amwezeshe kuzungumza maneno bayana na ya hikmah yatakayoziathiri akili na hisia za Fir-‘awn na watu wake.  Mlinganiaji akiwa fasaha wa ulimi, ameiva kielimu, mkali wa hoja na msomaji mzuri wa wakati na mazingira, basi bila shaka kazi yake itafanikiwa.

 

Walinganiaji wa dini, watoaji mihadhara na hotuba elimishi, ni vizuri sana kwao kusoma du’aa hii ili Allaah Awawezeshe na Awasaidie katika kufikisha ujumbe wao kwa walengwa.

 

 

Tunapata  faida zifuatazo kutokana na du’aa hii:

 

 

1-  Du’aa ni ‘ibaadah ambayo viumbe wameumbwa kwa ajili yake.

 

2-  Du’aa ni silaha ya Muislamu wakati anapoelekea kutekeleza jukumu lolote lile zito au jepesi.

 

3-  Du’aa hii inawafaa walinganiaji, watoa hotuba, wahadhiri, waalimu na kila mwenye kuhitajia jambo la kheri lenye uzito ndanimwe.

 

 

 

Share