20-Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu Na Sharh Yake: Kuzidishiwa ‘Ilmu

Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu

 

Na Sharh Yake

 

Alhidaaya.com

 

 

20-Kuzidishiwa ‘Ilmu

 

 

 

 

رَّبِّ زِدْنِي عِلْمًا"

 

“Rabbi wangu!  Nizidishie ‘ilmu”.  [Twaahaa: (114)]

 

Allaah ‘Azza wa Jalla Amemwamuru Nabiy Wake Muhammad (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amwombe Amzidishie elimu.  Amri hii inayoelekezwa kwa Nabiy wetu, inaelekezwa pia vile vile kwetu, isipokuwa amri maalum yenye vielelezo vya kumhusisha yeye tu pasina sisi.

 

Elimu muhimu zaidi hapa ya kuombwa ni elimu ya Kitabu Chake Kitukufu Qur-aan.  Elimu hii humpandisha mtu kufikia kuyajua mambo ya kumnufaisha hapa duniani na kesho aakhirah.  Allaah Hakumwamuru amwombe ziada katika jambo jingine lolote isipokuwa kwenye elimu.  Na hii inaonyesha fadhila ya elimu, na kwamba elimu ni katika amali bora kabisa.

 

Kuna Hadiyth nyingi zinazohimizia jambo hili tukufu.  Na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ilikuwa katika du’aa zake:

 

"اللَّهُمَّ انْفَعَني بِمَا عَلَّمْتنِي، وَعَلِّمْنِي مَا يَنْفَعُني، وَزِدْنِي عِلْمًا"

 

“Ee Allaah! Ninufaishe kwa yale Uliyonifundisha, na Unifundishe ya kuninufaisha, na Nizidishie elimu”.  [Sunan At-Tirmidhiy.  Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh]

 

Tunapata faida zifuatazo kutokana na du’aa hii:

 

1-  Muislamu anatakiwa asichoke kutafuta elimu, bali aendelee kusoma umri wake wote na hususan elimu ya dini.  Rasuli pamoja na elimu pana aliyopewa, lakini hata hivyo Allaah Amemwamuru amwombe Amzidishie elimu.

 

2-  Elimu bora ya kupewa kipaumbele ni elimu ya dini.  Elimu hii itamfanya Muislamu kumwabudu Mola wake kama inavyotakikana na kufuzu kesho aakhirah.

 

3-  Taaluma nyingine pia ni muhimu sana kwa maisha yetu kama uhandisi, udaktari, udereva, urubani na kadhalika.  Hizi pia Muislamu anatakiwa amwombe Allaah Amzidishie ili aifanye kazi kwa ufanisi zaidi.  Kazi ni ‘ibaadah muhimu kwa Muislamu, na kila anavyoifanya kwa ufanisi, Allaah Humpenda zaidi na kumlipa thawabu zaidi.  Lakini elimu ya dini asiisahau kabisa, bali aipe kipaumbele.

 

4-  Kwa sasa hakuna udhuru tena kwa Muislamu wa kutafuta au kusoma elimu yake ya dini kutokana na teknolojia wezeshi tuliyonayo.  Tovuti za kidini na mitandao ya kijamii imesheheni taaluma zote za dini.  Ni yeye tu kuamua.

 

 

Share