24-Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu Na Sharh Yake: Iymaan, Maghfirah Na Rahmah

Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu

 

Na Sharh Yake

 

Alhidaaya.com

 

 

24-Iymaan,  Maghfirah Na Rahmah

 

 

 

 

"رَبَّنَا آمَنَّا فَاغْفِرْ لَنَا وَارْحَمْنَا وَأَنتَ خَيْرُ الرَّاحِمِينَ"

 

“Rabb wetu!  Tumeamini, basi Tughufurie na Uturehemu, Nawe  Ndiye Mbora wa wenye kurehemu”.  [Al-Muuminuuna: (109)]

 

 

Hii ni du’aa ya Waumini wenye iymaan ya kweli.  Imekusanya ndani yake kumwomba Allaah kwa Jina Lake Tukufu la Rabbi pamoja na kujieleza waombaji kuwa wao wamemwamini Yeye na yote waliyokuja nayo Mitume Wake.  Hii kama tulivyoashiria nyuma ni wasiylah ya kupelekea kujibiwa du’aa.

 

Sababu ya kuja du’aa hii njema ni kwamba makafiri motoni wataomba watolewe humo ili warejeshwe duniani.  Na Allaah Atawaambia:

 

" اخْسَئُوا فِيهَا وَلَا تُكَلِّمُونِ"

“Hizikeni humo! Na wala msinisemeshe!”

 

Halafu Allaah Akabainisha sababu ya kuadhibiwa kwao Akisema:

 

"إِنَّهُ كَانَ فَرِيقٌ مِّنْ عِبَادِي يَقُولُونَ رَبَّنَا آمَنَّا فَاغْفِرْ لَنَا وَارْحَمْنَا وَأَنتَ خَيْرُ الرَّاحِمِينَ"

 

Hakika lilikuwa kundi miongoni mwa Waja Wangu, wakisema:  Rabb wetu! Tumeamini, basi Tughufurie na Uturehemu, Nawe Ndiye Mbora wa wenye kurehemu”.  [Al-Muuminuwna: (109)].

 

Na walipokuwa wakisema hivi na kushikamana na iymaan yao, makafiri hao walikuwa wanawacheza shere na kuwadharau.

 

 

"فَاتَّخَذْتُمُوهُمْ سِخْرِيًّا حَتَّىٰ أَنسَوْكُمْ ذِكْرِي وَكُنتُم مِّنْهُمْ تَضْحَكُونَ  • إِنِّي جَزَيْتُهُمُ الْيَوْمَ بِمَا صَبَرُوا أَنَّهُمْ هُمُ الْفَائِزُونَ"

 

“Mkawafanyia dhihaka, hadi wakakusahaulisheni kunidhukuru, na mlikuwa ni wenye kuwacheka  •  Hakika Mimi Nimewalipa leo (Jannah) kwa vile walivyosubiri, hakika wao ndio wenye kufuzu”.  [Al-Muuminuuna: (110-111)]. 

 

Waombaji katika du’aa hii wamejumuisha iymaan, kuomba maghfirah na rahmah, kutawassal kwa Allaah kwa Jina Lake Tukufu la Rabb na kumsifu kwa Rahmah pana zisizo na mipaka.

 

Tunapata faida zifuatazo kutokana na du’aa hii:

 

 

1-  Kutawassal kwa Allaah kwa ‘amali njema ni katika tawasulati zenye kuvuta matarajio makubwa zaidi ya kujibiwa du’aa.  Na kutawassal Muislamu kwa iymaan yake ni katika tawasulati bora zaidi.

 

 

2-  Kuomba maghfirah ni katika maombi muhimu ambayo Muislamu anatakiwa awe na pupa nayo. Ukipata maghfirah, utasalimika na adhabu na yote ya kuchukiza.

 

 

3-  Maghfirah huombwa kwanza kabla ya rahmah.  Bila maghfirah, hakuna rahmah. Maghfirah kwanza, halafu rahmah.

 

 

4-  Hatari ya kuwacheza shere Waumini.  Hatima ya hili ni motoni.  Mbaya zaidi ni Muislamu kumcheza shere nduguye Muislamu.

 

 

 

Share