26-Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu Na Sharh Yake: Kuepushwa Na Adhabu Ya Jahannam

Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu

 

Na Sharh Yake

 

Alhidaaya.com

 

 

26-Kuepushwa Na Adhabu Ya Jahannam

 

 

 

 

"رَبَّنَا اصْرِفْ عَنَّا عَذَابَ جَهَنَّمَ إِنَّ عَذَابَهَا كَانَ غَرَامًا*إِنَّهَا سَاءَتْ مُسْتَقَرًّا وَمُقَامًا"

 

“Rabb wetu! Tuepushe adhabu ya Jahannam.  Hakika adhabu yake ni yenye kugandamana daima; isiyomwacha mtu  •  Hakika hiyo (Jahannam) ni mahali paovu mno pa kustakiri na mahali pa kuishi”.  [Al-Furqaan: (65-66)]

 

Hii ni du’aa ya Waja wema wa Allaah.  Amewasifu kwa sifa njema kabisa zilizotukuka, na Akawategemezea Kwake mtegemezo wa tashrifa na taadhima kwa ajili ya kunyanyua hadhi yao Akisema:

 

"وَعِبَادُ الرَّحْمَـٰنِ الَّذِينَ يَمْشُونَ عَلَى الْأَرْضِ هَوْنًا وَإِذَا خَاطَبَهُمُ الْجَاهِلُونَ قَالُوا سَلَامًا"

 

Na Waja wa Ar-Rahmaan ni wale wanaotembea katika ardhi kwa unyenyekevu na upole, na majahili wanapowasemesha, wao husema:  Salaam! [Al-Furqaan: (63)].

 

Waja hawa wema katika du’aa yao hii wamemwomba Awaepushe na adhabu ya Jahannamu pamoja na sababu zake za kuweza kufanikisha mwepusho huo hapa duniani kwa kuwepesishiwa utendaji wa ‘amali njema na kuepushiwa machafu yenye kupelekea huko.

 

Waja hawa pamoja na kuwajibika kwao vyema katika makalifisho yote na pupa yao kubwa ya kumcha Allaah, lakini hata hivyo, bado wanaiogopa adhabu ya Allaah ya Jahannamu na wanaendelea kumlilia Allaah Awaepushe nayo bila kujinata kwa ‘amali zao hizo wala kujiona bora kuliko wengineo.  Na hii ni katika uzuri wa ‘ibaadah na ukamilifu wake.  Muislamu hatakiwi kabisa kujiona kwa matendo yake mema vyovyote yawavyo.  Hapa waja hawa wanamwomba Allaah kana kwamba wao wamezamia kwenye maasia na madhambi.  Hofu imewatamalaki. Ni kama Allaah Alivyosema kuhusiana na Waumini:

 

"وَالَّذِينَ يُؤْتُونَ مَا آتَوْا وَقُلُوبُهُمْ وَجِلَةٌ أَنَّهُمْ إِلَى رَبِّهِمْ رَاجِعُونَ"

 

Na ambao wanatoa vile wavitoavyo na huku nyoyo zao zinakhofu kwamba hakika watarejea kwa Rabb wao”.  [Al-Muuminuwna: (60)].

 

Kisha wakaeleza sababu ya ombi lao hilo, nayo ni kuwa adhabu hiyo ni shari ya kudumu milele, na ni maangamivu yasiyomwacha atakayeingia ndani ya Jahannam.  Hakuna mapumziko wala kutoka isipokuwa kwa Waumini walioingia humo kwa muda, na wale watakaotolewa humo kwa shifaa ya Rasuli na baadhi ya Waumini wema.  Isitoshe, Jahannam hiyo ni mashukio yenye mwonekano mbaya kabisa wa kutisha na kuchefua.

 

Bila shaka haifichikani kwetu umuhimu wa kujilinda na moto kwa kuwa ndio shari mbaya zaidi Aliyowahadharisha watu nayo Allaah.  Na hapa tunajulishwa kuwa ni vizuri kwa mwombaji aelezee sababu ya akiombacho kama walivyoeleza Waja hawa wema.

 

 

Tunapata faida zifuatazo kutokana na du’aa hii:

 

 

 

1-  Umuhimu wa du’aa hii kwa vile:

 

 

(a) Allaah Ta’aalaa Ameitaja kwa watu ambao Yeye Mwenyewe Amewasifu na Kuwategemezea kwa Nafsi Yake kwenye Qur-aan ambayo itasomwa mpaka Siku ya Qiyaamah.

 

(b) Imekuja kwa muundo wa kitenzi cha wakati uliopo katika Neno Lake: "وَالَّذِينَ يَقُولُون kinachoonyesha kukithirisha kwao na kudumu kwao kuomba hilo.

 

 

2-  Inapendeza zaidi kwa mwombaji kueleza sababu ya ombi lake.  Hii pia ni katika kuitanua du’aa, na Allaah Analipenda hili.

 

 

3-  Kutawassal kwa Jina la Rabbu ni katika tawassulaati bora zaidi kuliko zote.

 

 

 

Share