Maana Ya Taqwa
Maana Ya Taqwa
Taqwa ni mojawapo ya maneno ya kipekee katika lugha ya Kiarabu ambayo hayawezi kutafsiriwa kwa neno moja au mawili. Kwa hiyo maana zake kilugha ni kinga, kujilinda, himaya, hifadhi, kutahadhari, kukhofu.
Na katika istilahi, Salaf wametaja mengi kuhusu taqwa, miongoni mwayo ni kumwabudu Allaah ipasavyo, kutekeleza yaliyoamrishwa na Allaah (سبحانه وتعالى) na Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم), kujiepusha makatazo Yao na kubakia katika mipaka ya Shariy’ah ya Dini, kumkhofu Allaah na kukhofu Adhabu na Ghadhabu Zake, kuwa na raghba (utashi) na kutaraji thawabu Zake, kumuadhimisha Allaah (سبحانه وتعالى) na kumpenda mapenzi ya kikweli pamoja na Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم).
Na taqwa haihitajii kuhakikishwa mtu kuwa mahali fulani au wakati fulani, bali taqwa ya hakika ni pale mtu anapokua yuko peke yake, akajiepusha na yaliyo haraam japokuwa hakuna mtu anayemuona. Na ndipo aliposema Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kuwa “Taqwa ipo hapa!” Akiashiria kwenye kifua chake palipo na moyo na kusema mara tatu.
Umar (رضي الله عنه) alimuuliza ‘Ubayy bin Ka’b (رضي الله عنه): “Taqwa ni nini?” Akajibu: “Ee Amirul-Muuminyn! Je, hukuwahi kupita njia yenye miiba?” Akasema: “Naam!” Akasema: “Ulifanya nini?” Akasema: “Niliinua miguu yangu huku nikiitazama na kuinua mguu mmoja na mwingine, nikikhofia mwiba usije kunichoma.” ‘Ubay akamwambia: “Hiyo ndiyo taqwa!”
‘Aliy bin Abi Twaalib (رضي الله عنه) amesema: “Taqwa ni kumkhofu Al-Jaliyl (Allaah) na kufanyia kazi Tanziyl (Qur-aan) na kuridhika na kidogo, na kujiandaa Siku ya Rahiyl (kuondoka duniani, kufariki).”