005-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji: Sababu Ya Kuharamishwa Baadhi Ya Vyakula Na Vinywaji
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا
Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi
005- Sababu Ya Kuharamishwa Baadhi Ya Vyakula Na Vinywaji
· Sababu Ya Kuharamishwa Baadhi Ya Vyakula Na Vinywaji
[Al-Mughniy (8/585), Ibn ‘Aabidiyna (5/194) na Matwaalibu Ulin Nuhaa (6/311)].
Kwa upembuzi na ufuatiliaji wa karibu wa sababu zilizotolewa na Fuqahaa katika vile walivyovihukumu kuwa ni haramu kuliwa, tunakuta kwamba ni haramu kula chochote, vyovyote iwavyo aina yake, kwa moja ya sababu hizi tano zifuatazo:
1- Kiwe kinasababisha madhara kwa mwili au akili. Allaah Amesema:
"وَلَا تَقْتُلُوا أَنفُسَكُمْ ۚ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ بِكُمْ رَحِيمًا"
“Wala msijiue. Hakika Allaah Ni Mwenye Kuwarehemuni”. [An-Nisaa: 29].
2- Kiwe kinalewesha, au kinaondosha hisia au kinalaza. Ni haramu kutumia vilevi vyenye kuondosha akili kama pombe na tembo, au mada zote zenye kuondosha hisia na kujitambua kama hashishi, afyuni na mfano wake.
3- Kiwe najisi. Ni haramu kila kilicho najisi au kilichonajisika kwa najisi isiyosameheka.
4- Chenye kuonekana kinyaa na kuhisika kichafu kwa watu wenye maumbile yaliyo salama. Ni kama kinyesi, mkojo, chawa na kiroboto.
5- Kutopata ruksa ya kisharia kama ni mali ya mtu mwingine. Ni haramu mtu kula chakula kisicho chake bila idhini ya mwenyewe au Idhini ya Allaah. Ni kama chakula cha kupora na kuiba, au kilichopatikana kwa njia ya kamari, ukahaba na mfano wa hayo.