009-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji:Kilichotajiwa Asiyekuwa Allaah Wakati Wa Kuchinjwa

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا

 

 Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi

 

Alhidaaya.com

 

009-Vyakula Vilivyoharamishwa Na Kitabu Cha Allaah:

 

Kilichotajiwa Asiyekuwa Allaah Wakati Wa Kuchinjwa

 

 

 

4-  Kilichotajiwa Asiyekuwa Allaah Wakati Wa Kuchinjwa

 

Ni kwa Neno Lake Ta’aalaa:

 

"حُرِّمَتْ عَلَيْكُمُ الْمَيْتَةُ وَالدَّمُ وَلَحْمُ الْخِنزِيْرِ وَمَا أُهِلَّ لِغَيْرِ اللَّـهِ بِهِ"

 

“Mmeharamishiwa nyamafu, na damu, na nyama ya nguruwe, na kilichotajiwa asiyekuwa Allaah katika kuchinjwa kwake”.  [Al-Maaidah: 03].

 

Na Neno Lake ‘Azza wa Jalla:

 

"وَلَا تَأْكُلُوا مِمَّا لَمْ يُذْكَرِ اسْمُ اللَّـهِ عَلَيْهِ وَإِنَّهُ لَفِسْقٌ"

 

“Na wala msile katika ambavyo halikutajwa Jina la Allaah (wakati wa kuchinjwa), kwani huo ni ukiukaji wa utiifu kwa Allaah”.  [Al-An’aam : 121].

 

Na kwa ajili hiyo, haifai kula mnyama aliyechinjwa na mshirikina, au mmajusi au aliyeritadi.  Ama mnyama aliyechinjwa na Mnaswara au Myahudi, huyo inajuzu kumla madhali haikujulikana kwamba amechinjwa kwa kutajwa Jina lisilo la Allaah.  Na hii ni kwa Neno Lake Ta’aalaa:

 

"وَطَعَامُ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ حِلٌّ لَّكُمْ"

 

“Na nyama iliyochinjwa na waliopewa Kitabu ni halali kwenu”.  [Al-Maaidah: 05].

 

Faida Mbili:

 

Ya Kwanza:  Nyama Zinazoagizwa Toka Nchi Zisizo Za Kiislam

 

Ikiwa zinazoagizwa toka nchi zisizo za Kiislamu ni nyama za wanyama wa bahari kama samaki na nyangumi, basi hizo ni halali kula, kwa kuwa hata bila kuchinjwa (chinjo la kisharia) ni halali, ni sawa akiwa aliyewavua ni Muislamu au asiye Muislamu.

 

Ama zikiwa ni za wanyama wa nchi kavu ambao ni halali kuliwa kama ngamia, ng’ombe, mbuzi, kondoo na ndege, na zikawa zimeagizwa toka nchi ambazo wakazi wake ni wamajusi, au mapagani, au wenye kukanusha kuwepo kwa Allaah kama Wakomunisti, basi nyama hizi hazifai kuliwa.

 

Na ama zikiagizwa toka nchi ambazo wakazi wake ni Manaswara au Mayahudi (Watu wa Kitabu), basi zinafaa kuliwa lakini kwa masharti mawili:

 

La kwanza:

 

Isijulikane kwamba wao walimelitaja jina la asiye Allaah wakati wa kuchinja kama msalaba au masihi na kadhalika.

 

La pili:

 

Mnyama achinjwe chinjo la kisharia kwa namna ambayo itakuja kubainishwa mbeleni.

 

“Katika miaka iliyopita, kwa hakika, ilikuwa tunatosheka kudai nchi hizi zinazosafirisha nyama kwetu kwamba zinachinja kwa mujibu wa sharia ya Kiislamu.  Lakini ikaja kugundulika kwa njia mbalimbali kwamba nchi hizi hazichinji chinjo la kisharia, na kwamba muhuri unaotiwa juu ya nyama hizi kuonyesha kwamba zimechinjwa kwa mujibu wa sharia ya Kiislamu, si lolote bali ni utapeli wa kula mali za Waislamu kwa njia haramu.  Shehena za kuku walioagizwa toka nje zishawahi kuwasili katika baadhi ya nchi za Kiarabu na kukutwa shingo ya kuku ikiwa nzima na kamili kabisa bila athari yoyote ya chinjo, pamoja na kuandikwa juu yake maneno ya kijadi ya kuwa “Zimechinjwa chinjo la Kiislamu!!  Bali hata wamefikia kuzichezea akili za Waislamu kwa kukutwa maboksi ya samaki walioagizwa toka nchi hizo yakiwa yameandikwa juu yake:  “Samaki hawa wamechinjwa kwa mujibu wa sharia ya Kiislamu!!”  [Al-Fiqhul Waadhwih cha Dk. Muhammad Bakr Ismaa’iyl (2/390 – 395)].

 

Ya Pili:  Jibini Zinazoagizwa Toka Nchi Zisizo Za Kiislamu

[Al-Mufas-swal cha ‘Abdul Kariym Zaydaan (3 / 54-55)]

 

Ikiwa jibini zinaagizwa toka nchi za Watu wa Kitabu na wao wanazitengeneza kutokana na “rennet” za wanyama ambao ni halali sisi kuwala, basi jibini hizi ni halali kwetu. 

 

Ama ikiwa zinaagizwa toka nchi za wamajusi au wasoshalisti au waabudu masanamu, na wao wanatengeneza jibini hizo kutokana na “rennet” za wanyama wao waliowachinja, basi wanyama hawa kwa upande wa Waislamu ni kama mzoga. 

 

Lakini je, ni halali kula jibini hizi zilizotengenezwa kutokana na “rennet” za mizoga hii?

 

Sheikh wa Uislamu (Allaah Amrehemu) amesema kuhusiana na jibini za wamajusi zilizotengenezwa kutokana na “rennet” za vichinjwa vyao kwamba kuna kauli mbili za ‘Ulamaa.  Kisha akasema: “Lenye kigezo cha nguvu zaidi ni kwamba jibini zao ni halali, na kwamba “rennet” za mfu na maziwa yake ni twahara, kwa vile Maswahaba walipoiteka Iraki walikula jibini za wamajusi, na hili lilikuwa liko wazi limeenea baina yao”.  [Majmuw’ul-Fataawaa (21/102 – 103)].

 

 

Share