014-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji: Al-Jallaalah: (الْجَلَّالَةُ)

 

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا

 

 Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi

 

Alhidaaya.com

 

Vyakula Vilivyoharamishwa Na Hadiyth Za Rasuli

 

 

014-Al-Jallaalah: (الْجَلَّالَةُ)

 

 

 

4-  Al-Jallaalah: (الْجَلَّالَةُ)

 

Hawa ni wanyama wanaokula najisi – au sehemu kubwa ya majani wanayokula au malisho au chakula ni najisi – ni sawa wakiwa ni ngamia, ng’ombe, mbuzi, kondoo, kuku na kadhalika.  Wanyama hawa si halali nyama zao wala maziwa yao.

 

Hii ni kauli ya Ahmad – katika moja ya riwaayah mbili – kutokana na Hadiyth ya Ibn ‘Umar:

 

"نَهَى رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ عَنْ أَكْلِ الْجَلَّالَةِ وَأَلْبَانِهَا"

 

“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza kula mnyama mwenye kula najisi pamoja na maziwa yake”.  [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh.  Imekharijiwa na Abu Daawuwd (3767), At-Tirmidhiy (1883) na Ibn Maajah (3189)].

 

Lakini Ash-Shaafi’iy amekamata mwelekeo wa kusema kwamba ni makruhu na wala si haramu kula (nyama ya mnyama huyu au kunywa maziwa yake).  Na hii ni riwaayah nyingine toka kwa Ahmad.

 

·        Ni Wakati Gani Inakuwa Halali Kumla Mnyama Anayekula Najisi?

 

Mnyama huyu kama atafungiwa siku tatu (ili asije kula vyakula najisi) na akalishwa malisho twahara safi, basi itahalalika kumchinja, kula nyama yake na kunywa maziwa yake.

 

Imeripotiwa kuhusiana na Ibn ‘Umar kwamba:

 

"كَانَ يَحْبِسُ الدًجَاجَةَ الْجَلاًلَةَ ثَلَاثًا"

 

“Alikuwa anamfungia kuku mla najisi siku tatu”.  [Isnaad yake ni Swahiyh.  Imekharijiwa na Ibn Abiy Shaybah (4660 – 8847).  Angalia Al-Irwaa (2504)].

 

Imenukuliwa pia toka kwa Imaam Ahmad (Rahimahul Laah) akisema kwamba atafungiwa siku tatu, ni sawa akiwa ndege au mnyama.  Na pia katika riwaayah aliyonukuliwa amesema:  “Kuku atafungiwa siku tatu, na ngamia, ng’ombe na mfano wao, watazuiliwa siku 40”.

 

Alaa kulli haal, tunasema kuwa “Al Jallaalah” anahalalika kwa kumfungia na kumlisha chakula safi twahara kwa makubaliano ya ‘Ulamaa wote, lakini wamekhitalifiana muda wa kumfungia.

 

 

 

Share