015-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri: Masuala Mawili Tata Na Majibu Yake

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الأَيْمَانِ وَالنُّذُوْرِ

 

Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri

 

015- Masuala Mawili Tata Na Majibu Yake

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Suala La Kwanza:  Ni Hadiyth:

 

" أَفْلَحَ وَأَبِيهِ إِنْ صَدَقَ"

 

“Atafaulu, naapa kwa baba yake, kama atasema kweli”… na mfano wa Hadiyth hii ya kuapa kwa baba au mama.

 

Imeelezwa katika baadhi ya Sanad za Hadiyth ya Twalha bin ‘Ubaydul Laah (Radhwiya Allaah ‘anhu) kuhusiana na kisa cha mtu ambaye alimuuliza Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu  Uislamu, Rasuli akamweleza yale aliyofaradhiwa.  Sehemu ya kisa inasema:

 

"فقالَ: هلْ عَلَيَّ غَيْرُهَا؟ قالَ: لا، إلَّا أنْ تَطَّوَّعَ، قَالَ: فأدْبَرَ الرَّجُلُ، وَهُوَ يَقُوْلُ: وَاللَّهِ لاَ أَزِيْدُ عَلَى هذَا، وَلَا أنْقُصُ مِنْهُ، فَقَالَ رَسُوْلُ اللهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: أفْلَحَ [وَأَبِيهِ] إنْ صَدَقَ، أَوْ: دَخَلَ الجنَّةَ [وَأَبِيهِ] إنْ صَدَقَ "

 

“Akauliza tena:  Je, kuna jingine zaidi ya hilo nililofaradhishiwa?  Akamwambia: Hapana, isipokuwa ukijitolea la ziada mwenyewe.  Akasema:  Mtu yule akageuka akiondoka na kusema:  Wa Allaah, sizidishi zaidi ya haya wala sipunguzi chochote.  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:  “Atafaulu, [naapa kwa baba yake], kama atasema kweli, au: Ataingia Peponi [naapa kwa baba yake] kama atasema kweli”.  [Ameikhariji kwa nyongeza hii Muslim (11) na Abu Daawuwd (392).  Al-Bukhaariy hakuikhariji (46)].

 

Kuna Hadiyth nyingine kama hii.  Ni ya Abu Hurayrah aliyesema:

 

"جَاءَ رَجُلٌ إلى النّبِيِّ صلّى الله عَلَيْهِ وَسَلّمَ، فَقَالَ: يا رَسُوْلَ اللهِ، أَيُّ الصَّدَقَةِ أَعْظَمُ أَجْرًا ؟ فَقَالَ: أَمَا وَأَبِيكَ لَتُنَبَّأَنَّهُ"

 

“Mtu mmoja alikuja kwa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumwambia:  Ee Rasuli wa Allah!  Ni Swadaqah ipi yenye malipo makubwa zaidi?  Akasema:  “Angalia, naapa kwa baba yako, hakika hilo utaelezwa…..”. [Muslim ameikhariji ikiwa na nyongeza hii (1032).  Walioikhariji bila nyongeza hii ni Al-Bukhaariy (1419), Abu Daawuwd (2865) na An-Nasaaiy (3611)].

 

Pia Hadiyth nyingine ya Abu Hurayrah:

 

"جَاءَ رَجُلٌ إِلَى النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ، فَقَالَ: مَنْ أَحَقُّ النَّاسِ بحُسْنِ صَحَابَتِي؟ فَقَالَ: نَعَمْ [وَأَبِيكَ] لَتُنَبَّأَنَّ، أُمُّكَ... "

 

“Mtu mmoja alikuja kwa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumuuliza:  Ni mtu yupi mwenye haki zaidi ya mimi kutangamana naye vizuri? Akamwambia:  “Na’am, [naapa kwa baba yako] hakika utaelezwa.  Ni mama yako……”.  [Imekharijiwa na Muslim (2548), Ibn Maajah (2706), na Ahmad (2/327).  Katika Sanad yake yupo Shurayk bin ‘Abdallah Al-Qaadhwiy].

 

Baadhi ya ‘Ulamaa –akiwemo Maalik na Ash-Shaafi’iy- wametolea dalili kwa kutumia riwaayaat hizi  kuwa ni makruhu na si haramu kuapa kwa asiye Allaah!!

 

‘Ulamaa wameliraddi hilo kwa majibu kadhaa.  Kati ya majibu hayo ni:

[Fat-hul Baariy (11/534) na Twarhut Tathriyb (7/145].

 

1-  Kutothibiti nyongeza ya  "وَأَبِيْهِ"Ibn ‘Abdul Barri ameashiria kuwa nyongeza hii haikuhifadhiwa.  Kadhalika, baadhi ya ‘Ulamaa wamezungumzia shaka yao kuhusu kuthibiti neno lake Rasuli "وَأَبِيكَ لَتُنَبَّأَنَّ" .  

 

Ninasema (Abu Maalik):  “Tukijaalia kwamba ziada zote hizi zipo, basi tutakuta ‘Ulamaa wana maelekezo kwa Hadiyth hizi –pamoja na unadra wake- ambayo inabidi tukomee kwenye baadhi yake kutokana na kukhalifiana kwake na Hadiyth mashuhuri zilizo wazi ambazo tumezitaja nyuma zikikataza hilo (la kuapa kwa asiye Allaah).  Kati ya maelekezo hayo ni:

 

2-  Kwamba tamko hili (la naapa kwa baba yake n.k) lilikuwa limezoeleka ulimini mwao bila kukusudia kiapo halisi.  Al-Bayhaqiy ameelemea kwenye mwono huu.  An-Nawawiy kasema:  “Ni jibu ridhishi”.

 

3-  Kwamba tamko lilikuwa linatokea katika maneno yao kwa picha mbili. Kwanza kwa ajili ya utukuzisho, na pili kwa ajili ya usisitizo wa neno, na katazo linahusu picha ya kwanza ya utukuzisho.

 

4-  Kwamba hili lilikuwa linajuzu hapo nyuma kisha likafutwa.  Hili linaradiwa kwa kusemwa kuwa haiwezekani kwa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa alikuwa anaapa kwa asiye Allaah kama ambavyo hawezi pia kuapa kwa mtu kafiri.  Halafu madai ya kuwa hilo lilifutwa ni dhaifu, kwa kuwa upo uwezekano wa kukusanya nususi zote, kuzioanisha na kuzifanyia kazi.

 

5-  Kwamba katika jawabu kuna neno limeondoshwa ambalo ni  ,"رَبِّ"na taqdiyr yake ni: 

 " أَفْلَحَ وَرَبِّ أَبِيهِ" (Amefaulu naapa kwa Mola wa baba yake).

 

6-  Ni kwa ajili ya mshangao.  Linalodulisha hilo ni kutotumiwa neno: أَبِي" (Naapa kwa baba yangu), bali limetumika neno la "وَأَبِيهِ" (Naapa kwa baba yake), au "وَأَبِيك" (Naapa kwa baba yako) kwa kuegemezwa kiwakilishi cha msemeshwa aliyepo (yako) au asiyepo (yake).

 

7-  Kwamba hilo linamhusu Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) peke yake, halimhusu mwingine yeyote katika Ummah wake.

 

Hili linaradiwa kwa kusema:  Mambo maalumu yanayomhusu Rasuli hayathibiti kwa makisio, bali kwa dalili thabiti.

 

Ninasema:  “Linaloonekana lenye nguvu zaidi ni kuwa kuapa kwa asiye Allaah ni haramu kutokana na dalili bayana kuhusiana na hilo.  Ni kama neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

"مَنْ حَلَفَ بِغَيْرِ اللَّهِ فَقَدْ أَشْرَكَ"

 

“Mwenye kuapa kwa asiye Allaah, basi hakika amefanya shirki”.

 

Haiwezekani kwa tamshi hili bayana la shirki kupindishwa na kupelekwa kwenye ukaraha.  Na hili ni katika vinavyowekwa nje ya qaaidah (kanuni) isemayo:   الْجَمْعُ أَوْلَى مِنْ التَّرْجِيْحِ “Kukusanya (nususi na kuzifanyia kazi zote) ni bora kuliko kuteua baadhi (kwa kuzipa nguvu) na kuacha nyingine”.  

 

Suala La Pili:  Allaah Ta’aalaa Kuapa Kwa Viumbe Vyake

 

Kati ya mambo ambayo wanayatolea dalili wenye kusema kuwa ni karaha kuapa kwa asiye Allaah na si haramu, ni kwamba Allaah Mtukufu Ameapa kwa Viumbe Vyake Mwenyewe kwenye Kitabu Chake.  Amesema:

 

وَالسَّمَاءِ وَالطَّارِقِ 

 

1.  Naapa kwa mbingu na kinachokuja usiku.

 

Na:

 

وَالشَّمْسِ وَضُحَاهَا 

 

1.  Naapa kwa jua na mwangaza wake.

 

Na:

 

وَالْفَجْرِ 

 

1.  Naapa kwa Alfajiri.

 

وَلَيَالٍ عَشْرٍ 

 

2.  Na Naapa kwa masiku kumi.

 

Hili linajibiwa kwa majibu mawili:

 

Jibu La Kwanza:  Ndani ya viapo hivi kumefichwa kiapo kwa Rabbi wa Viumbe hivi.  Ni kama Amesema:

 

"وَرَبِّ السَّمَاءِ"

 

“Naapa kwa Rabbi wa mbingu”.  Na:

 

"وَرَبِّ الشَّمْسِ"

 

“Naapa kwa Rabbi wa jua” na kama hivi.

 

Pili:  Kuapa Allaah kwa Viumbe Vyake ni dalili juu ya Uwezo Wake na Uadhwama Wake.  Anaapa kwa Kiumbe Chake chochote Akitakacho, na hakuna njia ya ulinganishi juu ya Viapo Vyake.

 

Ninasema:  “Imejulikana kwamba wenye kusema kwamba si haramu kuapa kwa asiye Allaah, hawana chochote tena cha kukitegemea katika yote waliyoyatolea dalili”.

                                               

 

Share