016-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri: Mwenye Kuapa Kwa Asiye Allaah, Nini Afanye?
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الأَيْمَانِ وَالنُّذُوْرِ
Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri
016- Mwenye Kuapa Kwa Asiye Allaah, Nini Afanye?
Toka kwa Abu Hurayrah, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
" مَنْ حَلَفَ فَقَالَ فِي حَلِفِهِ: بِاللَّاتِ وَالْعُزَّى فَلْيَقُلْ: لَا إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ. وَمَنْ قَالَ لِصَاحِبِهِ: تَعَالَ أُقَامِرُكَ فَلْيَتَصَدَّقْ "
“Mwenye kuapa akasema katika kiapo chake: Naapa kwa Al-Laata na Al-‘Uzza, basi aseme: Laa ilaaha illa Allaah. Na mwenye kumwambia mwenzake: Njoo tucheze kamari, basi atoe Swadaqah”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (6650) na Muslim (1647)].
Na Sa’ad bin Abiy Waqqaasw amesema:
"حَلَفْتُ بِاللاَّتِ وَالْعُزَّى، فَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ : " قُلْ لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ وَحْدَهُ لاَ شَرِيْكَ لَهُ ثُمَّ انْفُثْ عَنْ يَسَارِكَ ثَلاَثًا وَتَعَوَّذْ وَلاَ تَعُدْ " .
“Niliapa kwa Allaata na Al-‘Uzza. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaniambia: Sema: Laa ilaaha illa Allaah wahdahu laa shariyka lahu. Kisha pulizia pulizia mate upande wako wa kushoto mara tatu, na jilinde kwa Allaah, na usirudie tena”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Ibn Maajah (2097), Ahmad (1/183) na wengineo. Ama kwa An-Nasaaiy (7/7), kuna nyongeza ya: “Laa ilaaha illa Allaahu wahdahu laa shariyka Lahu, mara tatu”. Nayo ni Dhwa’iyf kama ilivyotajwa katika Al-Irwaa (8/192)].
Na je hili ni kwa aliyeapa kwa Al-Laata na Al-‘Uzza tu, au linamhusu kila aliyeapa kwa kinginecho badala ya Allaah? Inavyoonekana ni kwa kila aliyeapa kwa kinginecho badala ya Allaah. Na kwa ajili hiyo, Sheikh wa Uislamu amesema: [Majmuw’u Al-Fataawaa (33/122)].
“…Kuapa kwa viumbe kama kuapa kwa Al-Ka’abah, wafalme, mababu, upanga na kadhalika, viapo hivi havina dhima ndanimwe, bali pia havifungiki na wala hana kafara atakayevivunja kwa makubaliano ya Waislamu wote. Bali atakayeapa kwa vitu hivyo, anatakiwa tu aseme “Laa ilaaha illa Allaah wahdahu laa shariyka lahu” kama alivyosema Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa sallam)…”. Kisha akataja Hadiyth ya Abu Hurayrah iliyotangulia.
……………………….