022-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri: Kumwapia Kitendo Mtu Mwingine Na Hukmu Kwa Mwenye Kuapiwa
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الأَيْمَانِ وَالنُّذُوْرِ
Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri
022- Kumwapia Kitendo Mtu Mwingine
Na Hukmu Kwa Mwenye Kuapiwa
Mtu anaweza kuapa kufanyika au kuachwa jambo kwa kumnasibishia mtu mwingine. Anaweza kusema kwa mfano: “Wa Allaah, utafanya”, au “Wa Allaah, usifanye kadha”.
Kama amemwapia kufanya jambo la waajib au kuacha jambo la haraam, basi ni lazima kwa aliyeapiwa akitekeleze kiapo hicho. Na kama atamwapia kufanya jambo la haraam au kuacha la waajib, basi hapo haitojuzu kukitekeleza kiapo hicho. Na kama amemwapia jambo la makruhu, basi itakuwa ni makruhu kukitekeleza kiapo. Ama akimwapia kufanya jambo la Sunnah au la mubaah, au kuacha jambo la makruhu au la mubaah, basi hapo itapendeza kukitekeleza kiapo kutokana na Hadiyth ya Al-Barraa:
" أَمَرَنَا رَسولُ اللهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ بسَبْعٍ : أَمَرَنَا بعِيَادَةِ المَرِيضِ، وَاتِّبَاعِ الجَنَازَةِ، وَتَشْمِيتِ العَاطِسِ، وإبْرَارِ المُقْسِمِ، وَنَصْرِ المَظْلُومِ، وإجَابَةِ الدَّاعِي، وإفْشَاءِ السَّلَامِ"
“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) ametuamuru mambo saba: Ametuamuru kumzuru mgonjwa, kwenda kuzika, kumwombea Rahmah mpiga chafya, kutekeleza kiapo cha aliyekuapia, kumnusuru mwenye kudhulumiwa, kuitikia wito wa anayekuita na kueneza (maamkizi ya) salaam”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (6654) na Muslim (2066)].
Agizo la kutekeleza kiapo cha anayemwapia mtu atekeleze au aache jambo linaonekana kuwa ni la waajib. Lakini pamoja na hivyo, linageuzwa na kuwa mustahabbu kutokana na Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas kuhusiana na kisa cha Abu Bakr kuifasiri njozi aliyoiota mtu mmoja mbele ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) [akapatia baadhi na akakosea mengine]. Abu Bakr akasema:
"فَو اللَّهِ يَا رَسُولَ اللَّهِ لَتُحَدِّثَنِّي مَا الَّذِي أَخْطَأْتُ . فَقَالَ النَّبِيُّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: " لاَ تُقْسِمْ "
“Naapa kwa Allaah ee Rasuli wa Allaah. Utanieleza lile ambalo nimekosea. Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akamwambia: Usiape”. Yaani: “Usiape tena mara ya pili, kwani mimi sitokujibu”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na At-Tirmidhiy (2293), Abu Daawuwd (3268), na Ibn Maajah (3918)].
Na huenda jibisho hili la Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) lilikuwa kwa ajili ya kubainisha kujuzu (kutotekeleza uliloapiwa kulifanya), kwani Rasuli hafanyi kinyume na jambo linalopendeza kufanywa isipokuwa kwa lengo la kubainisha kujuzu hilo. Na kama si hivyo, basi Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa akitekeleza viapo walivyomwapia watu atekeleze jambo fulani au aache. Katika Hadiyth ya Al-Mughiyrah bin Shu-‘bah:
"...قلتُ: يا رَسُوْلَ اللَّهِ، أقسَمْتُ عَلَيْكَ إلَّا مَا أعْطَيْتَنِي ْيَدَكَ، فَنَاوَلَني يَدَهُ، فَأَدْخَلْتُهَا فِيْ كَمِّي حتَّى انتَهَيتُ بها إلى صَدرِيْ فَوَجدَهُ مَعْصُوْبًا، فَقَالَ : إنَّ لَكَ عُذرًا"
“…..nikasema: Ee Rasuli wa Allaah! Nimekuapia kuwa lazima utanipa mkono wako. Akanipa mkono wake, nikauingiza kwenye mpenyo wa nguo yangu nikaufikisha hadi kifuani kwangu, akakikuta kimefungwa kitambaa. Akasema: Hakika wewe una udhuru”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (3826), Ahmad (4/249) na Al-Bayhaqiy (3/77)].
· Ikiwa Mwapiwa Hakutekeleza Kiapo Cha Nduguye, Je Mwapaji Ni Lazima Atoe Kafara?
1- Akimwambia nduguye: “Bil Laah (kwa Jina la Allaah), fanya kadha”, au: “Bil Laah, nakuomba, utafanya”, basi hili linakuwa ni ombi tu na si kiapo, hivyo linakuwa halina kafara ndani yake.
Hadiyth ya Rasuli inasema:
"وَمَنْ سَأَلَكُمْ بِاَللَّهِ فَأَعْطُوْهُ"
“Na atakayewaombeni kwa Jina la Allaah, basi mpeni”. [Imekharijiwa na Al-Bayhaqiy].
Na hapa hakuna kafara kwa wenye kuombwa kama hawatompa kitu.
2- Akisema: “Wa Allaah, utafanya kadha” kisha mwapiwa asitekeleze, hapa kuna kauli mbili. Kuna inayosema kuwa ni lazima mwapaji atoe kafara. Kauli hii imenukuliwa toka kwa ‘Umar, watu wa Madiynah, ‘Atwaa, Qataadah, Al-Awzaa’iy na Ash-Shaafi’iy. [Al-Mughniy (11/247). Angalia pia Al-Muhallaa (8/35)].
Kauli ya pili ya Ibn Hazm inasema kuwa hana kafara kwa kuwa hakukusudia kuvunja kiapo. Kauli hii inatiliwa nguvu na Hadiyth iliyotangulia ya Abu Bakr. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.