023-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri: Matokeo Ya Kukitekeleza Kiapo Au Kukivunja
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الأَيْمَانِ وَالنُّذُوْرِ
Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri
023- Matokeo Ya Kukitekeleza Kiapo Au Kukivunja
Ikiwa mwapaji atatekeleza jambo aliloliapia katika yamini ya kufungika, basi hana kitu juu yake na wala halazimiwi kafara. Lakini kama atakivunja kiapo chake kwa kutotekeleza jambo aliloliapia kwa kuthibiti aliloliapia kuwa halipo, au kutokuwepo lile aliloliapia kuwa lipo, basi ni lazima atoe kafara.
· Je, Kusahau, Kukosea Na Kulazimishwa Kunazuia Adhabu Ya Kuvunja Kiapo?
Mwenye kuapa kwamba hatofanya jambo fulani kisha akalifanya kwa kusahau, au kwa kukosea, au kwa kulazimishwa, basi huyo anazingatiwa kuwa hakuvunja kiapo chake kutokana na Hadiyth:
"إنَّ اللَّهَ تَجَاوَزَ لِي عَنْ أُمَّتِي الْخَطَأَ وَالنِّسْيَانَ وَمَا اسْتُكْرِهُوا عَلَيْهِ" .
“Hakika Allaah Ameusamehe Umati wangu kwa ajili yangu wakikosea, wakisahau, na kwa yale waliyolazimishwa”. [Hadiyth Hasan].
Na kwa Kauli Yake Ta’aalaa:
"رَبَّنَا لَا تُؤَاخِذْنَا إِن نَّسِينَا أَوْ أَخْطَأْنَا"
“Rabb wetu! Usituchukulie tukisahau au tukikosea”. [Al-Baqarah: 286].
Katika Hadiyth, Allaah Ta’aalaa Amesema (kuandamizia Aayah hii): “Hakika Nimefanya”. Na katika riwaayah: “Na’am”. [Hadiyth Swahiyh].
Na kwa Neno Lake Ta’aalaa:
"وَلَـٰكِن يُؤَاخِذُكُم بِمَا كَسَبَتْ قُلُوبُكُمْ"
“lakini Atakuchukulieni kwa yaliyochuma nyoyo zenu.” [Al-Baqarah: 252].
Haya ni madhehebu ya Ash-Shaafi’iy na Hanbali. Ni kauli pia ya Ibn Hazm. [Al Wajiyz cha Al-Ghazaaliy (2/229), Matwaalibu Ulin Nuhaa (6/369) na Al-Muhallaa (8/35)].