024-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri: Kusema “In Shaa Allaah” Katika Yamini

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

 

كِتَابُ الأَيْمَانِ وَالنُّذُوْرِ

 

Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri

 

024- Kusema “In Shaa Allaah” Katika Yamini

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Muradi wa neno hili “In Shaa Allaah” ni kutegemeza Matashi ya Allaah au mfano wake kwa kila tamshi ambalo haidhaniki mtu kuvunja kiapo kwalo.  Ni kama kusema mwapaji baada ya kiapo chake: "إِلَّا أَنْ يَشَاءَ اللَّـهُ" ila Atakapotaka Allaah, au: "إنْ أعَانَنِي الله"  kama Allaah Atanisaidia, au "إنْ يسَّرَ اللَّهُ" Allaah Akifanya wepesi, na mfano wa hivyo.  [At-Tamhiyd (14/372), Al-Mughniy (11/226) na Fat-hul Baariy (11/602)].

 

 

Toka kwa Abu Hurayrah kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:

 

"‏ مَنْ حَلَفَ عَلَى يَمِينٍ فَقَالَ إِنْ شَاءَ اللَّهُ، لَمْ يَحْنَثْ".

 

“Mwenye kuapa yamini na akasema In Shaa Allaah, basi hakuvunja kiapo (asipotekeleza)”.  [Isnaad yake ni Swahiyh, lakini Al-Bukhaariy ameitia dosari.  Imekharijiwa na At-Tirmidhiy (1532), An Nasaaiy (7/30) na Ibn Maajah (2104).  Al-Bukhaariy ameikosoa akisema kuwa ‘Abdul Razzaaq ameifupisha toka kwa Hadiyth ya Ma’amar kuhusu kisa cha Nabiy Sulaymaan kinachofuatia baada yake.  Nami nasema:  “Inawezekana zikawa ni Hadiyth mbili tofauti. Angalia Al-Irwaa (8/197)”].

 

Lakini Hadiyth hii inatiliwa nguvu na Hadiyth ya Abu Hurayrah toka kwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) kuhusiana na kisa cha Nabiy Sulaymaan (‘Alayhis Salaam) aliposema:

 

"‏ لأَطُوفَنَّ اللَّيْلَةَ عَلَى تِسْعِينَ امْرَأَةً تَلِدُ كُلُّ امْرَأَةٍ مِنْهُنَّ غُلاَمًا يُقَاتِلُ فِي سَبِيلِ اللَّهِ فَقَالَ لَهُ صَاحِبُهُ : قُلْ إِنْ شَاءَ اللَّهُ ، فَلَمْ يَقُلْ ، فَطَافَ بِهِنَّ فَلَمْ تَلِدْ مِنْهُنَّ إِلاَّ امْرَأَةٌ وَاحِدَةٌ نِصْفَ إِنْسَانٍ ‏"‏ ‏.‏ فَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ‏"‏ لَوْ قَالَ إِنْ شَاءَ اللَّهُ لَمْ يَحْنَثْ وَكَانَ دَرَكًا لِحَاجَتِهِ ‏"

 

“Wa Allaah, nitawazungukia (kuwajimai) wanawake 90 leo usiku, kila mwanamke kati yao atazaa kijana atakayepigana Jihaad katika Njia ya Allaah. Sahibu yake akamwambia: Sema In Shaa Allaah, naye hakusema. Akawazungukia, na hakuzaa yeyote kati yao isipokuwa mwanamke mmoja tu aliyezaa mtu nusu (mtoto ambaye hakukamilika).  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah “alayhi wa aalihii wa sallam) akasema: Lau kama angelisema In Shaa Allaah, basi asingelivunja kiapo chake, na ingekuwa sababu ya kupata lengo lake”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al Bukhaariy (6720) na Muslim (1654)].

 

·      Faida:

 

[Al Fat-h (11/605) na Subulus Salaam (4)]

 

Baadhi ya ‘Ulamaa wamejuzisha kusema In Shaa Allaah baada ya kumalizika kiapo kwa kitambo kidogo kutokana na Hadiyth hii.  Hili limejibiwa kwa kuambiwa kuwa maneno ya yamini ya Sulaymaan yamekuwa ni marefu, hivyo inajuzu kuwa sahibu yake kumwambia sema In Shaa Allaah kulifanyika wakati huo huo.  Hivyo hakuna hoja inayobakia.

 

La sahihi ni lile walilosema Jumhuwr ya kuwa neno In Shaa Allaah linazuia kufungika yamini kwa sharti ya yamini kuunganika moja kwa moja nalo bila kuwepo mtengano.  Na lau ingejuzu kutenganika (kuwepo mnyamao) –kama walivyosema baadhi ya Salaf- basi asingeliwajibishwa yeyote kwa kuvunja kiapo na wala asingelihitajia kutoa kafara.

 

Na wamekhitalifiana kuhusu kitambo cha muunganiko.  Jumhuwr wamesema: Ni kusema In Shaa Allaah na kuunganisha na kiapo moja kwa moja bila ya kunyamaza kati yake, na kupumua hakuharibu jambo.  Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

 

Kwa muhtasari kuhusu hili, ni kuwa mwenye kusema In Shaa Allaah katika yamini yake, basi hawajibishwi kafara asipotekeleza.  Lakini pamoja na hivyo, kuna masharti katika hili:

 

1-  Neno liungane na yamini.  Lisitenganishwe na mnyamao ambao kati yake panaweza kuingia maneno mengine, na wala lisitenganishwe na maneno mengine ya kando yasiyohusika.

 

2-  Aliseme mtu kwa ulimi wake.  Haifai kulisemea moyoni.

 

3-  Alikusudie kikweli.  Si sharti alikusudie toka anapoanza kuzungumza.

 

4-  Hakuna tofauti kati ya kulitanguliza kabla ya yamini au kulileta mwisho.

 

[Fiqhul Aymaan cha ‘Iswaam Jaad (uk 188-189) kwa mabadilisho madogo].

 

 

 

 

Share