025-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri:Je, Yamini Ni Kwa Mujibu Wa Mwapaji Au Mwenye Kuapisha?
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الأَيْمَانِ وَالنُّذُوْرِ
Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri
025- Je, Yamini Ni Kwa Mujibu Wa Mwapaji Au Mwenye Kuapisha?
[Al-Mughniy (11/242, 284), Al-Badaai’u (3/99), Ad-Dusuwqiy (2/138) na Sharhu Muslim cha An-Nawawiy].
Mchujo tunaoupata kutokana na maneno ya Wanachuoni kuhusiana na suala hili ni kuwa mwenye kuapa ana hali mbili:
Ya Kwanza:
Asiwepo kiasili mwenye kumwapisha bali aape yeye mwenyewe kwa khiyari yake mwenyewe. Marejeo ni kwa niyyah yake, kutokana na ujumuishi wa kauli yake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam):
"إنَّما الأعمالُ بالنِّيَّاتِ"
“Hakika si vinginevyo, matendo yote yanategemea niyyah”. Hivyo basi, kama atanuwia kwa yamini yake lile ambalo yeye analikusudia, basi yamini yake itaelekea huko huko, ni sawa likiwa alilolinuwia linaafikiana na mwonekano wa maneno yake au linatofautiana.
Ya Pili:
Awe ameapishwa na hakimu au mtu mwingine kwa jambo la haki. Hapa yamini inafungika kwa mujibu wa alilolinuwia mwapishaji, na si mwapaji. Na “tawriyah” (neno lenye kubeba maana mbili; ya juu dhahiri na ya ndani fiche) haitomfaa mwapaji katika hali hii kutokana na Hadiyth ya Abu Hurayrah aliyesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:
"يَمِينُكَ عَلَى مَا يُصَدِّقُكَ عَلَيْهِ صَاحِبُكَ"
“Yamini yako ni kwa mujibu wa ambalo sahibu yako atakuamini”.
Na katika riwaayah:
"الْيَمِينُ عَلَى نِيَّةِ الْمُسْتَحْلِفِ"
“Yamini inachukulika kwa mujibu wa niyyah ya mwapishaji”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1653), Abu Daawuwd (3255), At-Tirmidhiy (1354), Ibn Maajah (2120-2121) na wengineo].
Na kama si hivyo, basi yamini mbele ya hakimu isingelikuwa na maana yoyote, na haki za watu zingepotea.
Inavuliwa kutokana na hili kama mwapishaji atakuwa amemdhulumu mwapaji au mtu mwingine. Hapo itajuzu kwa mwapaji kutumia “tawriyah” (neno lenye kubeba maana mbili; ya juu dhahiri na ya ndani fiche) ili kulinda haki au kumnusuru mdhulumiwa. Ni kama katika Hadiyth ya Suwayd bin Handhwalah aliyesema:
"خَرَجْنَا نُرِيدُ رَسُولَ اللَّهِ وَمَعَنَا وَائِلُ بْنُ حُجْرٍ فَأَخَذَهُ عَدُوٌّ لَهُ فَتَحَرَّجَ الْقَوْمُ أَنْ يَحْلِفُوا وَحَلَفْتُ أَنَّهُ أَخِي فَخَلَّى سَبِيلَهُ فَأَتَيْنَا رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَأَخْبَرْتُهُ أَنَّ الْقَوْمَ تَحَرَّجُوا أَنْ يَحْلِفُوا وَحَلَفْتُ أَنَّهُ أَخِي قَالَ: "صَدَقْتَ الْمُسْلِمُ أَخُو الْمُسْلِمِ ".
“Tulitoka kwa niyah ya kwenda kwa Rasuli wa Allaah tukiwa pamoja na Waail bin Hujr. Adui yake akamkamata, na watu wakahisi dhiki na kuona hilo ni dhambi wakakataa kuapa. Mimi nikaapa kwamba yeye ni ndugu yangu, na adui akamwachilia. Tukafika kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) nami nikamweleza kwamba wenzangu walihisi ni kosa kuapa nami nikaapa kuwa ni ndugu yangu. Akasema: “Umesema kweli. Muislamu ni ndugu ya Muislamu”. [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh].
Na kwa sababu pia dhalimu hana haki ya kuapisha, hivyo imejuzu “tawriyah” (kuwa huyo ni ndugu yake katika Uislamu na iymaan lakini si nduguye wa damu).