028-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri:Mushkil Na Ufumbuzi Wake
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الأَيْمَانِ وَالنُّذُوْرِ
Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri
028- Mushkil Na Ufumbuzi Wake
[Tafsiyr At-Twabariy, Ihkaamul Ihkaam cha Ibn Daqiyq Al-‘Iyd (2/266), na Naylul Awtwaar (8/277)].
Kusema nadhiri ni jambo makruhu, na kusema nadhiri ni jambo mustahabu lipendezalo, misemo yote hii miwili ni mushkil kwa dalili za kila upande.
Jumhuwr wanaposema nadhiri ni makruhu, basi ndani ya msemo huu kuna mushkil kwa upande wa kanuni (principles). Kanuni inasema: “Njia ya twa’a ni twa’a, na njia ya ma’aswiyah ni ma’aswiyah”. Na kwa kuwa nadhiri ni njia ya kuwajibika kufanya jambo la kujikurubisha kwa Allaah, imekuwa lazima kwa hili iwe ni ukurubisho kwa Allaah. Lakini matini za mwanzo zinaonyesha kinyume chake. Basi vipi matini hizi zinakabiliwa kuweka mambo sawa?
Njia nzuri zaidi ya kuondosha mushkil huu ni kusemwa kwamba nadhiri ya kujikurubisha kwa Allaah iko aina mbili:
1- Nadhiri iliyofungamanishwa na upatikanaji wa manufaa. Ni kama mtu kusema: “Allaah Akimponya mgonjwa wangu, basi nimenadhiria kwa Allaah kufanya kadha” na mfano wa hili.
2- Nadhiri huria ambayo mweka nadhiri hakuifungamanisha na manufaa. Ni kama kujikurubisha mtu tu kwa Allaah kwa nadhiri akajisemea tu mwenyewe: “Ni juu yangu kwa Allaah kutoa swadaqah kitu kadhaa” na mfano wake.
Na itasemwa: Katazo katika Ahaadiyth linaelekea kwenye aina ya kwanza (iliyofungamanishiwa manufaa), kwa kuwa nadhiri yenyewe haikuwekwa hasa kwa ajili ya kujikurubisha kwa Allaah, bali imewekwa kwa sharti ya kupatikana manufaa kwa mweka nadhiri. Na manufaa hayo ambayo mweka nadhiri anajaribu kuyapata ndiyo hayo ambayo Ahaadiyth zimedulisha kwamba qadar humo iko juu ya nadhiri hiyo. Naye anaweka wazi kabisa kwamba kama mgonjwa wake hatopona, basi hatotoa swadaqah kwa kuwa amefungamanisha ponyo na swadaqah. Na hii ndiyo hali ya bakhili, hatoi chochote katika mali yake ila kwa mkabala wa maslaha ya haraka yanayozidi kile anachokitoa. Na maana hii ndiyo iliyoashiriwa kwenye neno lake Rasuli:
"وإنَّما يُسْتَخْرَجُ به مِنَ اَلْبَخِيلِ"
“bali kwa hakika hutolewa kwayo ('amali njema) toka kwa bakhili (wa kutenda mema”.
Na mtu asiye na ufahamu mzuri wa dini anaweza kuingizwa kwenye itikadi ya kudhani kwamba nadhiri yake ni lazima ifanikishe lengo lake, au kwamba Allaah Ta’aalaa Atafanikisha pamoja naye dhamira yake eti tu kwa sababu ya nadhiri hiyo. Hayo yote mawili yameashiriwa na Hadiyth ya Rasuli aliposema:
"إنَّهُ لا يَرُدُّ شَيْئًا".
“Hakika (nadhiri) hairudishi lolote (lililopangwa na Allaah)”.
Ninasema: “Ufafanuzi huu ni kuntu na imara kabisa. Nao umekusanya (nususi zote zinazoonekana kukinzana na kuzifanyia kazi), hivyo unatangulizwa juu ya “tarjiyh” (kuzipa nguvu baadhi ya nususi za kuziacha zingine)”.