029-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri: Vigawanyo Vya Nadhiri Na Ahkaam Zake: Cha Kwanza
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الأَيْمَانِ وَالنُّذُوْرِ
Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri
029-Vigawanyo Vya Nadhiri Na Ahkaam Zake: Cha Kwanza
Nadhiri ambazo Waislamu wanajiwekea zina vigawanyo viwili:
Kigawanyo Cha Kwanza
Nadhiri ya kufanya jambo jema kwa ajili ya Allaah.
Hii ni “Nadhiri ya Twa’aa”. Katika nadhiri hii, mtu hujilazimishia mwenyewe ima kufanya jambo ambalo Shariy’ah imelisunisha kufanywa kama Swalaah (za Sunnah), Swawm, Hajji (ya pili), kutoa swadaqah, kukaa ‘itikafu na mambo mengine mema yaliyosuniwa. Au ajilazimishe mwenyewe kufanya jambo la waajib kama nadhiri itafungamana na sifa mahsusi kama kuweka nadhiri ya kuswali Swalaah mwanzo wa wakati wake na mfano wa hilo.
Na ama lau ataweka nadhiri kwa jambo la waajib kama kuwa ataswali Swalaah tano za faradhi, au atafunga Swawm ya Ramadhwaan na mfano wa faradhi kama hizo, basi hakuna athari yoyote kwa nadhiri yake, kwa kuwa Allaah kuwajibisha hayo ni kukubwa zaidi ya yeye kujiwajibishia kwa nadhiri yake.
Na hapo nyuma kidogo tumeeleza kwamba nadhiri ya kujikurubisha kwa Allaah (nadhiri ya twa’a) ina picha mbili. Ya kwanza ni nadhiri isiyofungamanishwa na manufaa yoyote (nadhiri huria). Hii inafaa kisharia mtu kujiwekea na kuitekeleza. Na ya pili ni nadhiri iliyofungamanishwa na maslaha kwa mweka nadhiri. Hii inakuwa na picha ya kutaka badali na kuisimamisha ‘ibaadah juu ya sharti ya kupatikana lengo kusudiwa. Nadhiri hii imekatazwa mtu kuiweka.
· Hukmu Ya Kutekeleza “Nadhiri ya Twa’a”
Nadhiri ya twa’aa kwa aina zake mbili “Al-Mutwlaq” (isio ainishi) na “Al-Mu’allaq” (fungamanishwa), ni waajib kwa mweka nadhiri kuitekeleza kutokana na Qur-aan, Hadiyth na ‘Ijmaa. [Majmuw’u Fataawaa Shaykhil Islaam].
Baadhi ya dalili kuhusiana na hili zimetajwa nyuma. Kati yake ni:
1- Kauli Yake Ta’aalaa:
"ثُمَّ لْيَقْضُوا تَفَثَهُمْ وَلْيُوفُوا نُذُورَهُمْ"
29. Kisha wajisafishe taka zao na watimize nadhiri zao. [Al-Hajj: 29].
Na hii ni amri ya kutekeleza nadhiri, nayo inahukumia ulazima.
2- Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa Amewalaumu wale wanaoweka nadhiri na kisha wasizitekeleze Akisema:
وَمِنْهُم مَّنْ عَاهَدَ اللَّـهَ لَئِنْ آتَانَا مِن فَضْلِهِ لَنَصَّدَّقَنَّ وَلَنَكُونَنَّ مِنَ الصَّالِحِينَ﴿٧٥﴾ فَلَمَّا آتَاهُم مِّن فَضْلِهِ بَخِلُوا بِهِ وَتَوَلَّوا وَّهُم مُّعْرِضُونَ﴿٧٦﴾ فَأَعْقَبَهُمْ نِفَاقًا فِي قُلُوبِهِمْ إِلَىٰ يَوْمِ يَلْقَوْنَهُ بِمَا أَخْلَفُوا اللَّـهَ مَا وَعَدُوهُ وَبِمَا كَانُوا يَكْذِبُونَ﴿٧٧﴾
75. Na miongoni mwao wako waliomuahidi Allaah (kuwa): Akitupa katika Fadhila Zake, bila shaka tutatoa Swadaqah, na bila shaka tutakuwa miongoni mwa Swalihina. 76. Alipowapa katika Fadhila Zake; walizifanyia ubakhili, na wakakengeuka huku wakipuuza. 77. Basi Akawapatilizia unafiki katika nyoyo zao mpaka Siku watakayokutana Naye kwa sababu ya kumkhalifu kwao Allaah yale waliyomuahidi, na kwa sababu ya kukadhibisha kwao. [At-Tawbah 75-77)].
3- Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"مَنْ نذَرَ أنْ يُطِيْعَ اللهَ فَلْيُطِعْهُ"
“Mwenye kuweka nadhiri kwamba atamtii Allaah, basi amtii”. [Hadiyth Swahiyh. Imetajwa nyuma].
4- ‘Umar alimwambia Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
"إِنِّي نَذَرْتُ فِي الْجَاهِلِيَّةِ أَنْ أَعْتَكِفَ لَيْلَةً فِي الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ. قَالَ :" أَوْفِ بِنَذْرِكَ ".
“Mimi nilikuwa nimeweka nadhiri wakati wa ujahili ya kukaa ‘itikafu usiku mmoja ndani ya Al-Masjid Al-Haraam”. Rasuli akamwambia: Basi tekeleza nadhiri yako”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy 2042) na Muslim (1656)].
5- Imetajwa nyuma kidogo Hadiyth ya ‘Imraan bin Huswayn inayogusia lawama kwa watu watakaokuja baada ya karne bora ambao wataweka nadhiri na wasizitekeleze: "ثُمَّ يَجِيءُ قَوْمٌ، يَنْذِرُونَ ولا يَفُونَ،"
· Mtu Akiweka Nadhiri Kwa Jambo Asiloliweza, Au Akashindwa Kutekeleza Nadhiri:
Aliyeweka nadhiri ya kufanya jambo la kujikurubisha kwa Allaah, basi ni lazima aitekeleze nadhiri yake ikiwa ataweza kama ilivyotangulia. Akishindwa kuitekeleza, au aliloliwekea nadhiri kulifanya ni jambo ambalo hawezi kulifanya, basi si lazima kulitekeleza. Na hii ni kwa dalili zifuatazo:
1- Toka kwa Anas bin Maalik:
أنَّ رَسُوْلَ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ رَأَى رَجُلاً يُهَادَى بيْنَ اثْنَيْنِ، فَقَالََ: مَا هذَا؟ قَالُوا: نَذَرَ أنْ يَمْشِيَ إِلى الْبَيْتِ، فَقَالَ: إنَّ اللَّهَ عَزَّ وَجَلَّ لَغَنِيٌّ عَنْ تَعْذِيبِ هذا نَفْسَهُ. ثُمَّ أَمَرَهُ فَرَكِبَ".
“Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwona mtu mmoja (kikongwe sana) akiegemezwa mabegani kati ya watu wawili. Akauliza: Mbona hivi? Wakasema: Ameweka nadhiri ya kutembea hadi nyumbani. Akasema: Hakika Allaah ‘Azza wa Jalla Hana haja ya mtu huyu kujitesa mwenyewe. Akamwamuru apande (mnyama), akapanda”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy 1865) na Muslim (1642)].
2- Toka kwa ‘Uqbah bin ‘Aamir (Radhwiya Allaah ‘anhu):
"أَنَّ أُخْتَهُ نَذَرَتْ أَنْ تَمْشِيَ إِلى الْبَيْتِ الْحَرَامِ حَافِيَةً غَيْرَ مُخْتَمِرَةٍ، فذَكَرَ ذَلِكَ لِرَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَقَالَ: "مُرْ أُخْتَك فَلْتَرْكَبْ، وَلْتَخْتَمِرْ، وَلْتَصُمْ ثَلاَثَةَ أَيَّامٍ " .
“Kwamba dada yake aliweka nadhiri ya kutembea pekupeku na kichwa wazi bila mtandio hadi Al-Baytul Haraam. Akalieleza hilo kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Rasuli akamwambia: Mwamuru dada yako apande, ajifunike kichwa, na afunge siku tatu”. [Isnaad yake ni Layyin. Imekharijiwa na At-Tirmidhiy (1544), An-Nasaaiy (3815), Ibn Maajah (2134), Ad-Daaramiy (2334) na Ahmad (16668-16709-16735) kupitia kwa ‘Abdillaah bin Maalik toka kwa ‘Uqbah bin ‘Aamir. Katika Sanad yake yuko ‘Ubaydul Laah bin Zahr ambaye ni mdhaifu. Imekharijiwa pia na At-Twabaraaniy (17/324) toka kwa Abu Tamiym Al-Jayshaaniy toka kwa ‘Uqbah, na Sanad yake ni Dhwa’iyf].
Na katika riwaayah toka Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas kuhusiana na kisa hichi:
"فَمُرْها فَلْتَرْكَبْ وَلْتُكفِّرْ "
“Basi mwamuru (dada yako) apande na atoe kafara”. [Isnaad yake ni Layyin. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (3295), Ahmad (2685), Ibn Khuzaymah (3046-3047) na Ibn Hibaan (4384) kupitia kwa Shurayk toka kwa Muhammad bin ‘Abdul Rahmaan toka kwa Kurayb toka kwa Ibn ‘Abbaas. Na katika baadhi ya riwaayah kuna nyongeza isemayo: (تُكَفِّرُ عَنْ يَمِيْنِهَا) “Atolee kafara yamini yake”.
Katika riwaayah nyingine pia:
"فأمرَها النَّبيُّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَنْ تَرْكَبَ وَتُهْديَ هَدْيًا"
“Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwamuru apande na atoe mnyama wa kuchinjwa (Haram)”. [Isnaad yake ni Swahiyh. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (3296 – 3303), Ad-Daaramiy (2335), Ahmad (2027 – 2032 – 2165 – 2691 – 17125), Ibn Khuzaymah (3045), Al-Bayhaqiy (10/79) na At-Twabaraaniy (11/308)].
Na nyingine:
"فَلْتَرْكَبْ وَلْتُهْدِ بَدَنَةً"
“Basi apande na atoe ngamia (wa kuchinjwa)”. [Angalia iliyotangulia].
Na katika riwaayah nyingine:
"لَمْ يَذْكُرْ هَدْيًا وَلا كَفَّارَةً"
“Hakutaja mnyama wa kuchinjwa wala kafara”. [Imekharijiwa na Abu Daawuwd (3304), Al-Bayhaqiy (10/79), At-Twabaraaniy katika Al-Awsatw (9380), Ahmad (6653) na wengineo kupitia baadhi ya Sanad zilizotangulia lakini zimetiliwa nguvu].
3- Toka kwa ‘Uqbah bin ‘Aamir, kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"كَفَّارَةُ النَّذْرِ كَفَّارَةُ اليَمِينِ".
“Kafara ya nadhiri, ni kafara ya yamini”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1645), At-Tirmidhiy (1528) na An-Nasaaiy (3832)].
Kwa Hadiyth hizi na nyinginezo, ‘Ulamaa wamekhitalifiana kuhusu linalomlazimu aliyeweka nadhiri kwa jambo asiloliweza ikiwa atashindwa kulifanya. Ni kama mtu aliyeweka nadhiri ya kusafiri kwenda kuhiji kwa miguu halafu akashindwa. Wamekhitalifiana katika kauli zifuatazo:
[Fat-hul Qadiyr (3/173), Al-Majmuw’u (8/494), Al-Mughniy (10/74), Al-Inswaaaf (11/149), Al-Kaafiy cha Ibn ‘Abdil Barr (1/458), Jaami’ul ‘Uluwmi walhikami (uk. 309-310) na Majmuw’u Al-Fataawiy (35/327)].
Kauli Ya Kwanza: Halazimiwi Chochote
Ni kwa ubayana wa Kauli Yake Ta’aalaa:
"لَا يُكَلِّفُ اللَّـهُ نَفْسًا إِلَّا وُسْعَهَا"
286. Allaah Hakalifishi nafsi yoyote ila kwa kadiri ya uwezo wake. [Al-Baqarah: 02].
Na Kauli Yake Subhaanah:
"فَاتَّقُوا اللَّـهَ مَا اسْتَطَعْتُمْ"
16. Basi mcheni Allaah muwezavyo. [At-Taghaabun: 064].
Na Kauli Yake ‘Azza wa Jalla:
"رَبَّنَا وَلَا تُحَمِّلْنَا مَا لَا طَاقَةَ لَنَا بِهِ"
286. Rabb wetu! Usitutwike tusiyoyaweza. [Al-Baqarah: 02].
Na kauli yake (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
"فإذَا أَمَرْتُُكُمْ بِشَيْءٍ فأْتُوا مِنْهُ مَا اسْتَطَعْتُمْ"
“Na nikiwaamuruni kitu chochote, basi fanyeni kwa kadiri mnavyoweza”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (7288) na Muslim (1337)].
Hii ni kauli ya Ash-Shaafi’iy, na riwaayah toka kwa Ahmad na Al-Awzaa’iy.
Kauli Ya Pili: Ni Lazima Afanye Kafara Ya Yamini
Ni kwa Hadiyth ya ‘Uqbah bin ‘Aamir iliyotajwa nyuma. Na kwa neno la Rasuli kwa ‘Uqbah kuhusiana na dada yake:
"فَمُرْها فَلْتَرْكَبْ وَلْتُكفِّرْ "
“Basi mwamuru (dada yako) apande (kipando) na atoe kafara”.
Haya ni madhehebu ya Ahmad na Ath-Thawriy. Ni chaguo pia la Sheikh wa Uislamu.
Kauli Ya Tatu: Ni Lazima Afunge Siku Tatu
Ni riwaayah toka kwa Ahmad.
Kauli Ya Nne: Ni Lazima Atoe Ngamia (au Ng’ombe)
Ni kauli ya Mashaafi’iy.
Kauli Ya Tano: Atoe Mnyama Wa Kuchinjwa (Haram)
Ni kauli sahihi zaidi kwa Mashaafi’y, ni riwaayah toka kwa Ahmad, na ni kauli ya Mahanafiy na Al-Layth.
Wanenaji wa kauli tatu za mwisho, wote wametegemea riwaayah kati ya riwaayah za kisa kilichotangulia cha dada wa ‘Uqbah bin ‘Aamir.
Kauli Ya Sita: Haimtoshelezi Kupanda, Bali Atahiji Mwaka Ufuatao, Ambapo Atatembea Mwendo Aliopanda, Na Atapanda Mwendo Aliotembea, Na Ni Lazima Atoe Ngamia (au Ng’ombe) Wa Kuchinjwa.
Ni kauli ya Maalik.
· Kauli Yenye Nguvu:
Ninaloliona mimi baada ya kuzitafiti Asaaniyd za Hadiyth hii ni kuwa riwaayah yenye nguvu zaidi kwa upande wa Sanad, ni riwaayah ya kutoa kafara kwa mnyama wa kuchinjwa (au ngamia, ng’ombe). Kisha inafuatiwa na riwaayah ya (Kufunga siku tatu).
Halafu ikanidhihirikia kuwa lenye nguvu zaidi kwa upande wa “Diraayah” (uhakika wa riwaayah na wapokezi wake) ni kuwa atalazimika kafara ya yamini. Na hii ni kwa haya yafuatayo:
1- Ni kwamba riwaayah ya kutoa ngamia au mnyama wa kuchinjwa (Haram) ambayo ndiyo imara zaidi kwa upande wa Sanad, inaweza kutiwa dosari kutokana na aliyoyaeleza Al-Haafidh katika Al Fat-h (11/589) ya kwamba At-Tirmidhiy amenukuu toka kwa Al-Bukhaariy kuwa kasema “Haiswihi kutaja mnyama wa kuchinjwa katika Hadiyth ya ‘Uqbah bin ‘Aamir”. Al-Bayhaqiy (10/80) amenukuu vile vile.
2- Ni kwamba riwaayah ya kufunga haikinzani na riwaayah isemayo: “Na atoe kafara”, na “Na atoe kafara ya yamini yake”, kwani kufunga siku tatu ni moja kati ya vipengele vya kafara ya yamini kama ilivyotangulia.
3- Ni kwamba hili ndilo lenye kuafikiana na Hadiyth ya ‘Uqbah bin ‘Aamir mwenyewe –naye ndiye aliyemuulizia dada yake-, ni kuwa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"كَفَّارَةُ النَّذْرِ كَفَّارَةُ اليَمِينِ".
“Kafara ya nadhiri, ni kafara ya yamini”.
Huenda yeye ameifupisha toka fatwa ya Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika hali ya dada yake.
4- Ni kwamba Ihraam haimwajibishii mtu kutembea, hivyo si waajib kuchinja mtu akiacha kutembea.
5- Ni kwamba kusema kuwa inamwajibikia kafara ya yamini, usemi huu utafaa ikiwa nadhiri haihusiani na Hijjah kutokana na Hadiyth iliyotangulia. Na haiingii akilini kusemwa kuwa kila aliyeweka nadhiri kisha asiweze kuitekeleza atoe ngamia wa kuchinjwa! Allaah Ndiye Mjuzi zaidi.
Kiufupi Kwa Muhtasari: Mwenye kuweka nadhiri ya kufanya jambo jema la utiifu kwa Allaah kisha akashindwa kulitekeleza, basi halazimikiwi kulifanya bali ni lazima afanye kafara ya yamini.