033-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri: Vigawanyo Vya Nadhiri Na Ahkaam Zake: Kigawanyo Cha Pili

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الأَيْمَانِ وَالنُّذُوْرِ

 

Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri

 

 

033- Vigawanyo Vya Nadhiri Na Ahkaam Zake: Kigawanyo Cha Pili

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Ni nadhiri isiyo na utiifu kwa Allaah Ta’aalaa ndani yake.  Nadhiri hii iko aina mbili:

 

Aina Ya Kwanza: 

 

Isiyo na ma’aswiyah ndani yake kwa dhati yake yenyewe (yaani jambo la mubaah).

 

Akiweka nadhiri mtu kwa jambo lisilo ma’aswiyah na halina sifa ya utiifu wa kujikurubisha kwa Allaah, basi si wajibu kwake kulitekeleza.  Jumhuwr wanasema kwamba jambo kama hilo ni mubaah na haliingii kwenye duara la nadhiri.  Na hii ni kutokana na Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas aliyesema:

 

 

"بَيْنَمَا النَّبيُّ صلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسلَّم يخطُبُ إذا هُوَ بِرَجُلٍ قَائمٍ فِي الشَّمْسِ، فَسَأََلَ عَنْهُ، قَالُوْا: هذَا أَبُوْ إِسْرَائِيْلَ نَذَرَ أَنْ يَقُوْمَ وَلا يَقْعُدَ وَلا يَسْتَظِلَّ وَلا يَتَكلَّمَ وَيَصُوْمَ، قال: مُرُوهُ فَلِيَتَكَلَّمْ وليَِسْتَظِلَّ ولِيَقْعُدْ وليُتِمَّ صَوْمَهُ".

“Wakati Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa anakhutubu, mara akamwona mtu amesimama juani.  Akauliza nani huyo? Wakamwambia:  Huyu ni Abu Israaiyl, ameweka nadhiri kwamba atasimama tu na hatokaa, wala hatosimama kivulini, wala hatozungumza na amefunga. Akasema:  Mwamuruni azungumze, akae kivulini, aketi na aikamilishe Swawm yake”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (6704), Abu Daawuwd (3300), Ibn Maajah (2136) na wengineo].

 

Hadiyth inatubainishia kwamba lile aliloliwekea nadhiri ambalo ni kiini cha twa’a kama Swawm, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwamrisha alitimize kwa ajili ya kutekeleza nadhiri yake.  Ama yale ambayo ni mubaah yasiyo na twa’a ndani yake kama kuacha kuzungumza, au kutoketi chini, au kusimama kivulini,  hayo aliamuru aachane nayo na asiyatekeleze.

 

Lakini Ahmad anasema nadhiri ya jambo la mubaah inafungika, lakini mweka nadhiri huchaguzwa baina ya kuitekeleza au kutoitekeleza, na wakati huo ni lazima atoe kafara.

 

Mhakiki Swiddiyq Khan amekhitari kuwa nadhiri ya jambo mubaah hubeba kwa njia rasmi jina la nadhiri, na hivyo huingia chini ya ujumuishi ubebao amri ya kuitekeleza.  Amesema:  “Linalotilia nguvu hilo ni lile alilolikhariji Abu Daawuwd:

 

"أَنَّ امْرأةً قَالَتْ: يا رَسُوْلَ اللهِ، إنِّي نَذَرْتُ إِذَا انْصَرَفْتُ مِنْ غَزْوَتِكَ سَالِمًا أَنْ أَضْرِبَ عَلى رَأْسِكَ بِالدُّفِّ. فَقَالَ لَهَا: أَوْفِيْ بِنَذْرِكِ".

 

“Kwamba mwanamke mmoja alisema:  “Ee Rasuli wa Allaah! Mimi niliweka nadhiri nikupigie dufu mbele yako ukirudi salama toka vitani.  Rasuli akamwambia:  Tekeleza nadhiri yako”.   [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na At-Tirmidhiy (3690), Abu Daawuwd (3316), Ahmad (5/356) na Ibn Hibaan (4386)].

 

Na ikiwa kupiga dufu si jambo la mubaah, basi itakuwa ima ni makruhu au baya zaidi kuliko makruhu, na wala haliwi kamwe ni jambo la kujikurubisha kwa Allaah.  Na kama ni mubaah, basi hiyo ni dalili juu ya wajibu wa kutekeleza nadhiri ya jambo mubaah.  Na kama ni makruhu, basi kuruhusu kulitekeleza kunaonyesha kwamba kutekeleza jambo la mubaah ni bora zaidi.  Vile vile, kuwajibisha kafara kwa aliyeweka nadhiri ambayo hakuitaja, kunaonyesha juu ya wajibu wa kafara kwa jambo la mubaah kwa ubora zaidi.

 

Hivyo kwa ufupi, tunaweza kusema kuwa nadhiri ya jambo la mubaah, haitoki nje ya moja ya vigawanyo viwili:  Ima itekelezwe kama ni waajib, au kafara iwe waajib kama haikutekelezwa..”.   [Ar-Rawdhwatun Naddiyyah (uk. 177-178)].

 

Al-Bayhaqiy (Rahimahul Laah amesema (10/77):  “Inafanana kama vile Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam)  alimruhusu kupiga dufu kwa kuwa hilo ni jambo mubaah, na ndani yake kuna kuonyesha furaha ya kuonekana Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kurejea kwake salama, na si kwamba nadhiri ni wajibu kwa hilo.  Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”.

 

Ninasema:  “Lakini mushkil kidogo upo kwa aliyoyaeleza Al-Bayhaqiy (Rahimahul Laah).  Ni kwamba Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia (mwanamke huyo):

 

"إِنْ نَذَرْتِ فَافْعَلِيْ، وَإلَّا فَلاَ".

 

“Kama uliweka nadhiri, basi fanya, na kama sivyo, basi usifanye”.

 

 Na hii inaonyesha kwamba alimwamuru kufanya hilo ili atekeleze nadhiri yake.  Lakini inabakia kwamba mwanamke kupiga dufu mbele ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na hadhira ya Maswahaba wanaume si jambo linaloruhusiwa.  Na kwa muktadha huo, inaonyesha kwamba Hadiyth hii ni tukio maalum linalomhusu mtu mmoja tu bila kuwahusu wengineo, na haitakikani kulitolea dalili.  Na asili ni kwamba nadhiri inakuwa kwa jambo ambalo ndani yake kuna twa’a ya kujikurubisha kwa Allaah, nayo ni ‘ibaadah. Hivyo haiwi isipokuwa kwa lile ambalo Allaah Ta’aalaa Ameliamuru.

 

Linaloonekana ni kwamba mubaah huangaliwa: Ikiwa ni njia kwa jambo la waajib au la Sunnah, basi nadhiri hufungika nalo, na kama si hivyo, basi lililo sahihi ni kuwa nadhiri haifungiki nalo kama walivyosema Jumhuwr.  Allaah Ndiye Mjuzi zaidi”.

 

Aina Ya Pili:

 

Lililowekewa nadhiri liwe ni ma’aswiyah kwa dhati yake lenyewe (nadhiri ya ma’aswiyah).

 

Mtu akiweka nadhiri kwa jambo la ma’aswiyah kama kunywa pombe, au kuua nafsi iliyoharamishwa, au kuchinja juu ya kaburi, au kufunga safari kwenda kwa isiyo Misikiti Mitatu, au kutofanya usawa baina ya watoto wake, au kuwatukuza zaidi baadhi yao, au kuwanyima mirathi na mfano wa ma’aswiyah kama hayo, basi haya si waajib kwake kuyatekeleza, bali pia ni haramu.

 

1-  Toka kwa ‘Aaishah, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

 

"مَنْ نَذَرَ أَنْ يُطِيْعَ اللهَ فَلْيُطِعْهُ وَمَنْ نَذَرَ أَنْ يَعْصِيَ اللهَ فَلا يَعْصِهِ".

 

“Mwenye kuweka nadhiri kwamba atamtii Allaah, basi amtii, na mwenye kuweka nadhiri kwamba atamuasi Allaah, basi asimuasi”.  [Hadiyth Swahiyh].

 

2-  Toka kwa ‘Imraan bin Huswayn kwamba Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"لا وَفَاءَ لِنَذْرٍ فيْ مَعْصِيَةٍ، وَلَا وَفَاءَ لِنَذَرٍ فِيْمَا لا يَمْلِكُ العَبْدُ، أَوْ: ابْنُ آدَمَ".

 

“Hakuna kutekeleza nadhiri katika jambo la maasia, na wala hakuna kutekeleza nadhiri katika ambacho mja hakimiliki, au: mwanadamu”.  [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1641), Abu Daawuwd (3316), An-Nasaaiy (7/19) na Ibn Maajah (2124)].

 

3-  Toka kwa Thaabit bin Adh-Dhwahhaak (Radhwiya Allaah ‘anhu), amesema:

 

" نَذَرَ رَجُلٌ عَلَى عَهْدِ رَسُوْلِ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَنْ يَنْحَرَ إِبِلًا بِبُوَانَةَ، فَأَتَى النَّبيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَقَالَ: إِنِّي نَذَرْتُ أَنْ أَنْحَرَ إِبِلًا بِبُوَانَةَ: فَقَالَ النَّبيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: هَلْ كَانَ فِيهَا وَثَنٌ مِنْ أَوْثَانِ الْجَاهِلِيَّةِ يُعْبَدُ؟  قَالَ: لَا، قَالَ: هَلْ كَانَ فِيهِ عِيدٌ مِنْ أَعْيَادِهِمْ؟ قَالَ: لَا، قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: أوْفِ بِنَذْرِك فَإِنَّهُ لَا وَفَاءَ لِنَذْرٍ فِي مَعْصِيَةِ اللَّهِ وَلَا فِيمَا لَا يَمْلِكُ ابْنُ آدَمَ".

 

“Mtu mmoja wakati wa enzi ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliweka nadhiri ya kuchinja ngamia (eneo la) Buwaanah.  Akamjia Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:  Mimi niliweka nadhiri ya kuchinja ngamia Buwaanah.  Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuuliza: Je, kulikuweko huko kiabudiwa chochote kati ya viabudiwa vya enzi ya ujahili kinaabudiwa?  Akasema:  Hapana.  Akamuuliza: Je, kulikuwa kunafanyika sherehe yoyote kati ya sherehe zao?  Akasema: Hapana.  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:  Tekeleza nadhiri yako, kwani hakuna kutekeleza nadhiri katika kumwasi Allaah wala katika ambacho mwanadamu hakimiliki”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Abu Daawuwd (3313)].

 

Hapa kuna dalili wazi kwamba kuchinja katika mahala ambapo kulikuweko kiabudiwa kinachoabudiwa au mahala popote ambapo ilikuwa ikifanyika sherehe yoyote katika sherehe za kijahili (enzi kabla ya Uislamu) ni ma’aswiya kwa Allaah Ta’aalaa, na kwamba kwa hayo, haijuzu kuitekeleza nadhiri. Kuna Hadiyth nyingi tu zinazogusia hili.

 

·        Je, Ni Lazima Kafara Kwa Nadhiri Ya Ma’aswiyah?

 

‘Ulamaa wana kauli mbili kuhusu hili:

 

Kauli Ya Kwanza:

 

Hana kafara mwenye kuweka nadhiri ya ma’aswiyah.  Ni madhehebu ya Maalik, Ash-Shaafi’iy na riwaayah toka kwa Ahmad.  Dalili zao ni:

 

1-  Neno lake (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

 

"لا نَذرَ فِيْ مَعْصِيَةِ اللَّهِ".

“Hakuna nadhiri katika kumwasi Allaah”.  [Hadiyth Swahiyh].

 

Hivyo nadhiri haifungiki kwa ma’aswiyah.

 

2-  Neno lake Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

"وَمَنْ نَذَرَ أَنْ يَعْصِيَهُ فَلاَ يَعْصِهِ".

 

“Na aliyeweka nadhiri ya kumwasi (Allaah), basi asimwasi”.  [Hadiyth Swahiyh].

 

Na wala hakuamuru kafara.

 

3-  Hadiyth zilizotangulia:  Kuhusu mwanamke aliyeweka nadhiri ya kumchinja Al-‘Adhwbaa (ngamia wa Rasuli), na mwanaume aliyeweka nadhiri ya kutosimama kivulini au kutozungumza na mfano wa hayo.  Katika Hadiyth hizi, Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwaamuru kutotekeleza nadhiri zao, na hakuna kiashirio chochote ndani yake kuwa aliwalazimisha kutoa kafara.

 

Kauli Ya Pili:

 

Ni lazima atoe kafara.  Ni madhehebu ya Abu Haniyfah, Ath-Thawriy na riwaayah nyingine toka kwa Ahmad.  Ni kauli iliyosimuliwa toka kwa Ibn Mas-‘uwd, Ibn ‘Abbaas, Jaabir, ‘Imraan bin Huswayn na Samurah bin Jundub (Radhwiya Allaah ‘anhum).  Dalili za wenye kauli hii:

 

1-  Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaah ‘anhu), Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"النَّذْرُ نَذْرَانِ، فَمَا كَانَ لِلهِ كَفَّارتُهُ الْوَفاءُ، وَمَا كَانَ لِلشَّيْطَانِ فَلا وَفَاءَ فِيْهِ، وَعَلَيْهِ كَفَّارَةُ يَمِيْن".

 

“Nadhiri ni nadhiri mbili.  Inayokuwa kwa ajili ya Allaah, kafara yake ni kuitekeleza.  Na inayokuwa kwa ajili ya shaytwaan basi haitekelezwi, na ni juu yake kafara ya yamini”.  [Hadiyth Hasan.  Imekharijiwa na Ibn Al-Jaaruwd (935), na kupitia Sanad yake Al-Bayhaqiy (1072).  Abu Daawuwd amekhariji mfano wake (3322) kupitia Sanad nyingine toka kwa Ibn ‘Abbaas.  Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh katika As-Swahiyhah (479)].

 

2- Hadiyth ya ‘Aaishah, Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"لاَ نَذْرَ فِيْ مَعْصِيَةِ اللهِ، وَكَفَّارَتُهَ كَفَّارةُ يمينٍ".

 

“Hakuna nadhiri katika kumwasi Allaah, na kafara yake ni kafara ya yamini”. [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh.  Imekharijiwa na Abu Daawuwd (3290), At-Tirmidhiy (1524), An-Nasaaiy (2/145) na Ibn Maajah.  Angalia Al-Irwaa (2590)].

 

Lenye Nguvu:

 

Hakuna shaka kwamba dalili za Hadiyth hizi mbili zina nguvu zaidi kuliko dalili za Hadiyth zilizotolewa na kundi la kwanza, kwani kafara kwenye Hadiyth hizo imenyamaziwa bila kutajwa.  Hivyo Hadiyth za kundi la pili zinatangulizwa kwa kuwa zimethibitisha kafara.  Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

 

·        Akiweka Nadhiri Ambayo Hakuitaja

 

Mtu akiweka nadhiri ambayo hakuiainisha au hakuitaja kama kusema: “Nimejiwekea nadhiri kwa Allaah”, basi ni lazima atoe kafara ya yamini.  Ni kwa  neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa sallam) toka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaah ‘anhu):

 

"مَنْ نَذَرَ نَذْراً لَمْ يُسَمِّهِ، فَكَفَّارَتُهُ كَفَّارَةُ يَمِينٍ، وَمَنْ نَذَرَ نَذْراً فِي مَعْصِيَةٍ، فَكَفَّارَتُهُ كَفَّارَةُ يَمِينٍ، وَمَنْ نَذَرَ نَذْراً لَا يُطِيقُهُ، فَكَفَّارَتُهُ كَفَّارَةُ يَمِين" .

 

“Mwenye kuweka nadhiri ambayo hakuitaja, basi kafara yake ni kafara ya yamini.  Na mwenye kuweka nadhiri katika ma’aswiyah, basi kafara yake ni kafara ya yamini.  Na mwenye kuweka nadhiri asiyoiweza, basi kafara yake ni kafara ya yamini”.  [Imekharijiwa na Ibn Abiy Shaybah (4/173) ikiwa mawquwf. Pia imekharijiwa na Abu Daawuwd (3322)].

 

Imehadithiwa mfano wake ikiwa marfuw’u katika Hadiyth ya ‘Uqbah bin ‘Aamir kwa tamko lisemalo:

 

"كَفَّارَةُ اَلنَّذْرِ [إِذَا لَمْ يُسَمِّ ] كَفَّارَةُ يَمِينٍ" .

 

“Kafara ya nadhiri (kama haikutajwa) ni kafara ya yamini”.  Lakini Hadiyth hii ni Dhwa’iyf.  [Ni Dhwa’iyf kwa nyongeza hii (kama haikutajwa).  Imekharijiwa na Abu Daawuwd (2324), At-Tirmidhiy (1528), na An-Nasaaiy (7/26).  Angalia Al-Irwaa (2586)].

 

 

 

Share