034-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri: Nadhiri Kwa Asiye Allaah Ni Shirki

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الأَيْمَانِ وَالنُّذُوْرِ

 

Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri

 

034- Nadhiri Kwa Asiye Allaah Ni Shirki

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Nadhiri ni ‘ibaadah.  Haijuzu kuielekeza kwa asiye Allaah Ta’aalaa.  Yeyote atakayeielekeza kwa asiye Allaah, akaielekeza kwa Malaika mwenye hadhi kubwa kwa Allaah, au kwa Nabiy Mursal, au kwa walii katika mawalii akiwa hai au maiti, au kwa jua, au kwa mwezi na mfano wa hayo katika mambo wanayoyafanya waabudiaji masanamu, au waabudiaji makaburi na mfano wao, wakiamini kwamba hao au hivyo vitawadhuru au kuwanufaisha, au kuwakidhia haja zao, au kuwaondoshea matatizo yao, basi mtu huyu atakuwa amefanya dhambi kubwa kuliko yote, nalo ni kumshirikisha Allaah Ta’aalaa.  Haya ni sawa na yale Aliyoyaelezea Ta’aalaa katika Neno Lake:

 

"وَجَعَلُوا لِلَّـهِ مِمَّا ذَرَأَ مِنَ الْحَرْثِ وَالْأَنْعَامِ نَصِيبًا فَقَالُوا هَـٰذَا لِلَّـهِ بِزَعْمِهِمْ وَهَـٰذَا لِشُرَكَائِنَا ۖ فَمَا كَانَ لِشُرَكَائِهِمْ فَلَا يَصِلُ إِلَى اللَّـهِ ۖ وَمَا كَانَ لِلَّـهِ فَهُوَ يَصِلُ إِلَىٰ شُرَكَائِهِمْ ۗ سَاءَ مَا يَحْكُمُونَ".

 

136.  Na wamemfanyia Allaah fungu katika mimea na wanyama Aliyoumba. Wakasema:  Hili ni la Allaah kwa madai yao, na hili ni kwa ajili ya washirika wetu.  Basi yaliyokuwa kwa ajili ya washirika wao hayamfikii Allaah.  Na yaliyokuwa kwa ajili ya Allaah hufika kwa washirika wao.  Uovu ulioje wanayoyahukumu!  [Al-An’aam: 06].

 

 

Sheikh wa Uislamu amesema:  “ ‘Ulamaa wamekubaliana kwa sauti moja kwamba haijuzu kwa yeyote kuweka nadhiri kwa asiye Allaah, si kwa Nabiy wala kwa asiye Nabii, na kwamba hilo ni shirki isiyopasa kutekelezwa”. [Majmuw’ul Fataawaa (1/286)].

 

Na amesema (Rahimahul Laah):  “Ama nadhiri yake (yaani mja) kwa asiye Allaah kama kuweka nadhiri kwa masanamu, jua, mwezi, makaburi na mfano wa hayo, basi hilo ni sawa na kuapa kwa asiye Allaah katika viumbe”.

 

Al-Amiyr As-Swan-’aaniy (Rahimahul Laah) amesema:  “Ama nadhiri tuzijuazo katika wakati wetu wa sasa wanazoziweka watu kwa makaburi na wafu, hili halina makhitilafiano kabisa katika uharamu wake, kwa kuwa mweka nadhiri anaitakidi kwamba maiti aliyemo ndani yake ana uwezo wa kunufaisha na kudhuru, au kuleta kheri na kuondosha shari, au kumfariji mwenye maumivu na kumponya mgonjwa.  Na haya ndiyo hasa waliyokuwa wakiyafanya waabudiao miungu, nayo ni haramu kama ilivyo haramu kuyawekea nadhiri. 

 

Ni haramu pia kuyapa nafasi na uwanja mambo haya, kwani kufanya hivyo ni kuikubali shirki.  Aidha, ni lazima kuyakemea na kubainisha kwamba hayo ni katika maharamisho makubwa ambayo waabudiao masanamu na miungu walikuwa wakiyafanya zamani, na muda ukarefuka mpaka mema yakageuka munkari, na munkari yakawa mema.  Na hata kumekuwa kunafanywa minasaba kwa wapokeaji nadhiri za wafu, na wale wajao pale alipo maiti huandaliwa makaramu na kuchinjwa wanyama kwenye mlango wake.  Na haya ndiyo hasa waliyokuwa wakiyafanya waabudiji masanamu.  Innaa lil Laahi Wa Innaa Ilayhi Raaji’uwn.  Na watu wetu wamesoma mengi muhimu kuhusiana na haya katika tasnifu yenye anwani isemayo:  “Kuitwaharisha aqiydah kutokana na uchafu wa kumkana Allaah”.  [Subulus Salaam].

 

 

 

 

Share