04-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji: Kuwinda Na Hukmu Zake: Masharti Ya Mnyama Au Ndege Anayetumiwa Kuwinda Ili Akikamatacho Kiwe Halali Kuliwa

 

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا

 

 Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi

  

الصَّيْدُ وَأَحْكَامُهُ

 

Kuwinda Na Hukmu Zake

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

04-Kuwinda Na Hukmu Zake: Masharti Ya Mnyama Au Ndege Anayetumiwa Kuwinda Ili Akikamatacho Kiwe Halali Kuliwa

 

Sharti La Kwanza:  Awe amepata mafunzo ya kuwinda

 

Allaah Ta’aalaa Amesema:

 

"وَمَا عَلَّمْتُم مِّنَ الْجَوَارِحِ مُكَلِّبِينَ تُعَلِّمُونَهُنَّ مِمَّا عَلَّمَكُمُ اللَّـهُ ۖ فَكُلُوا مِمَّا أَمْسَكْنَ عَلَيْكُمْ وَاذْكُرُوا اسْمَ اللَّـهِ عَلَيْهِ"

 

“Na mlivyowindiwa na wanyama na ndege wakali mliowafundisha kiweledi, na mnawafunza katika ambayo Allaah Amekufunzeni. Basi kuleni walichokukamatieni, na mkitajie Jina la Allaah”.  [Al-Maaidah : 04].

 

Mnyama aliyekamilika kimafunzo ni lazima awe na mambo matatu:

 

(a) Akiamuriwa kwenda kukamata anakwenda hapo hapo.

(b) Akiamuriwa kuacha anaacha hapo hapo.

(c) Akikamata mnyama hali chochote.

 

Akiyatimiza haya kwa majaribio kadhaa, basi anakuwa ni mhitimu kwa mujibu wa mazoea ya watu.  Majaribio haya yasipungue matatu kwa mujibu wa madhehebu ya Ash-Shaafi’iy na Hanbal.

 

Ikiwa mnyama huyu mwindaji atakula sehemu ya mnyama aliyemkamata, basi si halali.  Ni kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa ‘Adiyy bin Haatim:  

 

ِذَا أَرْسَلْتَ كِلاَبَكَ الْمُعَلَّمَةَ وَذَكَرْتَ اسْمَ اللَّهِ، فَكُلْ مِمَّا أَمْسَكْنَ عَلَيْكَ وَإِنْ قَتَلَتْ ، إِلاَّ أَنْ يَأْكُلَ الْكَلْبُ فَلَا تَأْكُلْ، فَإِنِّي أَخَافُ أَنْ يَكُونَ إِنَّمَا أَمْسَكَهُ عَلَى نَفْسِهِ"

 

“Ukiwaachilia mbwa wako waliopata mafunzo wakamate, na ukalitaja Jina la Allaah (wakati wa kuwaachilia), basi kula walichokukamatia hata kama watamuua mnyama, isipokuwa kama mbwa atakula (sehemu ya kiwindwa) basi hapo usimle mnyama huyo, kwani mimi ninachelea kuwa atakuwa amejikamatia mwenyewe”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imetajwa nyuma kidogo].

 

Angalizo:

 

Ikiwa mbwa asiye na mafunzo atakamata mnyama na mwindaji akamkuta mnyama yungali hai, halafu akamchinja chinjo la kisharia, basi mnyama huyo ni halali kuliwa vile vile.  Na hii ni kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipomwambia Abu Tha-’alabah Al-Khushaniy:

 

"وَمَا صِدْتَ بِكَلْبِكَ غَيْرِ الْمُعَلَّمِ فَأَدْرَكْتَ ذَكَاتَهُ فَكُلْ"

 

“Na ulichokiwinda kwa kumtumia mbwa wako asiye na mafunzo na ukawahi kukichinja, basi kula”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5478) na Muslim (1532)].

 

Sharti La Pili:  Mwindaji alitaje Jina la Allaah wakati anapomwamuru kwenda kukamata.

 

Ni kwa ujumuishi wa Neno Lake Ta’aalaa:

 

"وَلَا تَأْكُلُوا مِمَّا لَمْ يُذْكَرِ اسْمُ اللَّـهِ عَلَيْهِ"

 

“Na wala msile katika ambavyo halikutajwa Jina la Allaah (wakati wa kuchinjwa)”.  [Al-An’aam: 121].

 

Na kwa Neno Lake ‘Azza wa Jalla pia:

 

"فَكُلُوا مِمَّا أَمْسَكْنَ عَلَيْكُمْ وَاذْكُرُوا اسْمَ اللَّـهِ عَلَيْهِ"

 

“Basi kuleni walichokukamatieni, na mkitajie Jina la Allaah”.  [Al-Maaidah : 04].

 

Na pia kwa Hadiyth ya ‘Adiyy bin Haatim:  Amesema Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

"إذَا أَرْسَلْتَ كَلْبَكَ وَذَكَرْتَ اسْمَ اللهِ فَكُلْ"

 

“Ukimwachilia mbwa wako (kukamata), na ukalitaja Jina la Allaah, basi kula”. [Hadiyth Swahiyh.  Imetajwa nyuma kidogo].

 

Na katika Hadiyth ya Abu Tha-‘alabah, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"وَمَا صِدْتَ بِكَلْبِكَ الْمُعَلَّمِ فَذَكَرْتَ اسْمَ اللهِ فَكُلْ "

 

“Na ulichokiwinda kwa kumtumia mbwa wako aliyefunzwa na ukalitaja Jina la Allaah, basi kula”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imetajwa nyuma kidogo].

 

Sharti La Tatu:  Mbwa mwingine asishirikiane na mbwa wake

 

Toka kwa ‘Adiyy bin Haatim, amesema:

 

"قُلْتُ يَا رَسُوْلَ اللهِ ، أُرْسِلُ كَلْبِيْ وَأُسَمِّيْ ، فَأَجِدُ مَعَهُ عَلَى الصَّيْدِ كَلْباً آخَرَ لَمْ أُسَمِّ عَلَيْهِ ، وَلا أَدْرِيْ أَيُّهُمَا أَخَذَ ، قَالَ: لا تَأْكُلْ ، إِنَّمَا سَمَّيْتَ عَلى كَلْبِكَ وَلَمْ تُسَمِّ عَلَى الآخَرِ"

 

“Nilisema:  Ee Rasuli wa Allaah!  Ninamtuma mbwa wangu na kulitaja Jina la Allaah, halafu nakuja kumkuta mbwa mwingine ambaye sikumtajia Jina la Allaah amekamata pamoja naye mnyama, na sijui ni yupi kati yao aliyekamata mwanzo. Akasema:  Usile.  Wewe kiuhakika ulilitaja Jina la Allaah kwa mbwa wako, na wala hukulitaja kwa mwingine”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imetajwa nyuma kidogo].

 

Sharti La Nne:  Mbwa amjeruhi mnyama aliyemkamata

 

Kama mbwa atamkaba koo na kumbana pumzi, au akamuua kwa kishindo cha kumgonga, basi kiwindwa si halali.  Ni kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

"مَا أَنْهَرَ الدَّمَ وَذُكِرَ اسْمُ اللَّهِ فَكُلْ إِلاَّ بِسِنٍّ أَوْ ظُفْرٍ"

 

“Chochote chenye kumwagisha damu (ya mnyama), na Jina la Allaah likatajwa, basi kula, isipokuwa mfupa au kucha (hivi havifai kutumika kama kichinjio)”. [Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5503) na Muslim (1986)].

 

Faida:

 

Ya Kwanza:  Inajuzu kufuga mbwa kwa ajili ya kuwinda, kuchunga mifugo na ulinzi

 

Toka kwa ‘Abdullaah bin Mughaffal, amesema:

 

"أّمَرَ رَسُوْلُ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ بِقَتْلِ الكِلَابِ ، ثُمَّ قَالَ : مَا بَالُهُمْ وَبَالُ الكِلاَبِ ، ثُمَّ رَخَّصَ فِيْ كَلْبِ الصَّيْدِ وَكَلْبِ الغَنَمِ"

 

“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliamuru mbwa wauawe, kisha baadaye akasema:  Yanawahusu nini wao na mambo ya mbwa (waachane nao sasa, inatosha)?  Halafu akaruhusu (kumiliki) mbwa wa kuwinda na mbwa wa mifugo”.  [Imekharijiwa na Muslim (280), An-Nasaaiy (67), Abu Daawuwd (74) na Ibn Maajah (3200)].

 

Ama kufuga na kulea mbwa kwa sababu zingine zisizo hizi tajwa, hilo halifai. Toka kwa Abu Hurayrah, kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"مَنِ اقْتَنَى كَلْبًا لَيْسَ بِكَلْبِ صَيْدٍ، وَلَا مَاشِيَةٍ وَلَا أَرْضٍ، فَإِنَّهُ يَنْقُصُ مِنْ أَجْرِهِ قِيْرَاطَانِ كُلَّ يَوْمٍ"

 

“Yeyote mwenye kulea au kufuga mbwa ambaye si mbwa wa kuwinda, au wa kuchunga mifugo, au wa kulinda ardhi, basi hupungua kila siku mafungu mawili katika (jumla ya) thawabu zake.”  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5480) na Muslim (1574)]. 

 

Ya Pili:  Je, inafaa kuwinda kwa kutumia mbwa mweusi ti ti ti?

 

Huyu ni mbwa ajulikanaye kwa Kiarabu kama "الْكَلْبُ الأَسْوَدُ الْبَهِيْمُ", ambaye ni mweusi mwili wake wote bila hata chembe ya doa jeupe.  Mbwa huyu Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameamuru auawe.

 

Jaabir bin ‘Abdullaah amesema:

 

"أَمَرَنَا رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ بِقَتْلِ الْكِلَابِ حَتَّى إِنَّ الْمَرْأَةَ تَقْدَمُ منَ الْبَادِيةِ بِكَلْبِهَا فَنَقْتُلَهُ ، ثُمَّ نَهَى رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ عَنْ قَتْلِهَا وَقَالَ : عَلَيْكُمْ بِالْأَسْوَدِ الْبَهِيمِ ذِي النُّقْطَتَيْن فَإِنَّهُ شَيْطَان"

 

“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alituamuru kuwaua mbwa, hata ikawa mwanamke anakuja tokea majangwani na mbwa wake nasi tunamuua.  Kisha baadaye Rasuli akakataza kuwaua, na akasema:  Muueni tu mweusi mwenye vitone viwili, kwa sababu huyo ni shaytwaan”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Muslim (1572) na Abu Daawuwd (2846)].

 

Na juu ya msingi huu, Imaam Ahmad, Ibn Hazm na Ahlu Adh-Dhwaahir wengineo wanasema kuwa haifai mbwa mweusi kuwinda, kwa kuwa kilichowajibu kukiua ni haramu kukilea na kukipa mafunzo, na kwa hivyo ilichokiwinda na kukikamata, si halali kuliwa.  Si hivyo tu, bali Rasuli amemwita mbwa huyo shaytwaan, mbali na kuwa ni ruksa kula kiwindwa kilichouliwa, lakini hakihalalishwi na kilichoharamishwa kama ruksa nyinginezo.

 

Kundi la Masalaf wakiwemo Al-Hasan, An-Nakh’-iy, Qataadah na Is-haaq wamekirihisha kuwinda na mbwa huyo.

 

Lakini akina Abu Haniyfah, Maalik na Ash-Shaafi’iy, wao wamejuzisha kuwinda na mbwa mweusi ti ti ti.  Na hii ni kwa ujumuishi wa dalili zilizotangulia nyuma kuhusiana na kujuzu kuwinda kwa kutumia mbwa mwenye mafunzo, na dalili hizo hazikuainisha mbwa fulani bila wengineo, bali mbwa kiujumla (muhimu tu awe amepata mafunzo).

 

Ninasema:  “Ninaloliona kuwa na nguvu zaidi ni kuwa haijuzu kuwinda na mbwa mweusi ti ti ti.  Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”.

                                                 

 

Share