01-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji: Chinjo La Kisharia: Taarifu Yake
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا
Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi
التَّذْكِيَةُ الشَّرْعِيَّةُ
Chinjo La Kisharia
01-Chinjo La Kisharia: Taarifu Yake:
"التَّذْكِيَةُ" katika lugha, ni “maswdar” (kiini) ya kitenzi "ذَكَّيْتُ الْحَيَوَانَ" (nimemchinja mnyama), na nomino ni "الذَّكَاةُ" (chinjo au kuchinja).
Ama katika istilahi, ni sababisho, au ni njia yenye kufikishia kuhalalika kumla mnyama wa nchi kavu kwa hiari.
Mahanafi wameielezea kama ni njia ya kisharia ya kubakia utwahara wa mnyama na uhalali wa kumla kama mnyama mwenyewe analiwa, na uhalali wa kunufaika na ngozi yake na nywele zake kama haliwi.
Ama Mahanbali, wao wameielezea "التَّذْكِيَةُ" kama ni kumchinja au kumdunga chini ya shingo mnyama ambaye imewezekana kumdhibiti na anayefaa kuliwa, mwenye kuishi nchi kavu, lakini asiwe nzige au mfano wake, kwa kukata koo na umio. Au ni kumjeruhi mnyama asiyewezekanika kumdhibiti kama itashindikana kukata koo na umio.
"التَّذْكِيَةُ" iko aina mbili, nazo ni "الذَّبْحُ" na "النَّحْرُ"
Taarifu Ya "الذَّبْحُ":
Katika lugha ina maana ya kupasua, nayo ndio maana asili. Kisha ikatumika katika kukata koo kutokea ndani kwenye maungio kati ya shingo na kichwa chini ya taya mbili.
Ama katika istilahi, neno hili lina maana nyingi. Kati ya maana hizo ni njia ya kufikia kuhalalika mnyama, ni sawa kwa kumkata shingoni, au chini ya shingo, kwa mnyama anayeweza kudhibitiwa, au kwa kuitoa roho ya mnyama asiyeweza kudhibitiwa kwa kumjeruhi sehemu yoyote mwilini mwake kwa kitu chenye ncha kali, au kwa kujeruhiwa na mnyama mwindaji aliyefunzwa. "الذَّبْحُ" inakuwa kwa wanyama wote isipokuwa kwa ngamia tu.
Taarifu Ya "النَّحْرُ":
Katika lugha ina maana ya sehemu ya juu ya kifua, au sehemu ya kidani, au kifua chote. Pia ina maana ya kudunga chini ya shingo ya mnyama.
Na katika istilahi, ni kudunga (kuchana kwa kisu) sehemu ya chini ya shingo ya mnyama, na hii inakuwa spesheli kwa ngamia tu.
Faida:
Kumkhusisha ngamia kwa "النَّحْرُ" (kumdunga), na wanyama wengineo kwa "الذَّبْحُ" (kuchinja), ni jambo linalopendeza kwa Jumhuwr, lakini si waajib. Kupendeza huko ni kwa kuwa Allaah Ta’aalaa Ametaja "النَّحْرُ" kwa upande wa ngamia pale Aliposema:
"فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ"
“Basi swali kwa ajili ya Rabb wako na chinja (dunga)”. [Al-Kawthar : 02].
Na kwa ng’ombe, mbuzi na kondoo Ametaja "الذَّبْحُ" Aliposema:
"إِنَّ اللَّـهَ يَأْمُرُكُمْ أَن تَذْبَحُوا بَقَرَةً"
“Hakika Allaah Anakuamuruni mchinje ng’ombe”. [Al-Baqarah : 67].
Na kwa kuwa asili katika kuchinja, ni kuangalia lile lenye unafuu zaidi kwa mnyama. Na lile litakalompumzisha na kumwepushia taabu, mateso na uchungu, ndilo bora na litakiwalo zaidi. Hivyo basi, la sahali zaidi kwa ngamia ni kumdunga kwa kuwa sehemu ya chini ya shingo yake haina nyama, wakati wanyama wengine nyama zao zimekusanyika kwenye shingo. Ng’ombe, mbuzi na kondoo, shingo zao zote hazitofautiani.