02-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji: Chinjo La Kisharia: Hukmu Ya Kuchinja Na Hikmah Ya Kushurutishwa Kwake
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا
Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi
التَّذْكِيَةُ الشَّرْعِيَّةُ
Chinjo La Kisharia
02-Chinjo La Kisharia: Hukmu Ya Kuchinja Na Hikmah Ya Kushurutishwa Kwake:
Kuchinja ni sharti ya kuhalalisha kuliwa mnyama ambaye ni halali kuliwa kisharia, na kunufaika naye kwa njia zote. Allaah Ta’aalaa Amesema:
"وَلَا تَأْكُلُوا مِمَّا لَمْ يُذْكَرِ اسْمُ اللَّـهِ عَلَيْهِ وَإِنَّهُ لَفِسْقٌ"
“Na wala msile katika ambavyo halikutajwa Jina la Allaah (wakati wa kuchinjwa), kwani huo ni ukiukaji wa utiifu kwa Allaah”. [Al-An’aam : 121].
Raafi’u bin Khadiyj alimwambia Rasuli:
"إِنَّا لاَقُو الْعَدُوِّ غَدًا وَلَيْسَتْ مَعَنَا مُدًى قَالَ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ : " أَعْجِلْ أَوْ أَرْنِي مَا أَنْهَرَ الدَّمَ وَذُكِرَ اسْمُ اللَّهِ فَكُلْ لَيْسَ السِّنَّ وَالظُّفُرَ وَسَأُحَدِّثُكَ أَمَّا السِّنُّ فَعَظْمٌ وَأَمَّا الظُّفُرُ فَمُدَى الْحَبَشَةِ"
“Sisi kesho tunapambana na adui, na hatuna visu (vya kuchinjia). Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: Chinja haraka au kuwa makini (unaponoa), (ukichinjia kwa) chochote chenye kuchuruzisha damu sambamba na kutajwa Jina la Allaah, basi kula isipokuwa jino au kucha, na nitakueleza (sababu ya hilo). Ama jino, hilo ni mfupa, na ama kucha, hizo ni kisu cha Wahabeshi (wanachinja kwa kutumia kucha zao)”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5543) na Muslim (1968)].
Hadiyth hii inatupa faida kwamba kumwagika damu ya mnyama sambamba na kutajwa Jina la Allaah wakati wa kuchinjwa, ni sharti la kuhalalika kuliwa nyama yake.
Ama hikmah ya kuwa kuchinja ni lazima, ni kwamba uharamu wa kumla mnyama anayeliwa utabaki madhali damu yake iko ndani ya mwili wake, na damu hii haitoki mwilini mwake ila kwa kuchinjwa. Kadhalika, sharia imekuja kwa ajili ya kuhalalisha kwa njia maalum vyote vizuri vya halali. Allaah Ta’aalaa Amesema:
"يَسْأَلُونَكَ مَاذَا أُحِلَّ لَهُمْ ۖ قُلْ أُحِلَّ لَكُمُ الطَّيِّبَاتُ"
“Wanakuuliza wamehalalishiwa nini? Sema: Mmehalalishiwa vilivyo vizuri”. [Al-An’aam : 04].
Na Anasema tena:
"وَيُحِلُّ لَهُمُ الطَّيِّبَاتِ وَيُحَرِّمُ عَلَيْهِمُ الْخَبَائِثَ"
“Na anawahalalishia vilivyo vizuri na anawaharamishia vilivyo vibaya”. [Al-A’araaf : 157].
Na nyama hiyo haiwi salama au yenye manufaa mema ila kwa kumwagika damu ya mnyama na kutoka nje ya mwili wake, ima kwa kuchinjwa "ذَبْحً" au kwa kudungwa chini ya shingo "نَحْرٌ". Na kwa sababu hii, mfu umeharamishwa, kwa kuwa damu chafu bado ipo ndani ya mwili wa mnyama.
Hikma nyinginezo za kuchinja mnyama ni kuiweka mbali shirki na matendo ya washirikina, kukipambanua kinacholiwa na mwanadamu na kile kinacholiwa na wanyama wakali, lakini pia mwanadamu akumbuke Ukarimu wa Allaah kwake kwa kumruhusu kuua na kutoa roho ya mnyama ili aweze kumla na kunufaika naye kiujumla baada ya kufa.