03-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji: Chinjo La Kisharia: Masharti Ya Kuchinja:
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا
Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi
التَّذْكِيَةُ الشَّرْعِيَّةُ
Chinjo La Kisharia
03-Chinjo La Kisharia: Masharti Ya Kuchinja:
Kuna masharti kadhaa ambayo ni lazima yawepo ili mnyama anayechinjwa awe halali kuliwa. Baadhi yake yanahusiana na mnyama mwenyewe, mengine yanahusiana na mchinjaji, na baadhi nyingine kwa zana ya kuchinjia.
Masharti Ya Mnyama Anayechinjwa
1- Awe hai wakati anapochinjwa. Mnyama mfu hachinjwi.
2- Kuchinjwa kwake kuwe ndio sababu ya kutoka roho yake, na si kutokana na sababu nyingine.
3- Asiwe amewindwa eneo la Al-Haram. Hili limeelezwa katika Kitabu cha Hijja kwamba ni marufuku kuwinda eneo la Al-Haram. Na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema kuhusiana na Makkah:
"فَلَا يُنَفَّرُ صَيْدُهَا"
“Wanyama wake hawasumbuliwi (wala kuwindwa)”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1349) na Muslim (1355)].