04-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji: Chinjo La Kisharia: Masharti Ya Mchinjaji
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا
Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi
التَّذْكِيَةُ الشَّرْعِيَّةُ
Chinjo La Kisharia
04-Chinjo La Kisharia: Masharti Ya Mchinjaji
1- Awe na akili zake timamu. Ni sawa akiwa mwanaume au mwanamke, aliye baleghe au asiye baleghe kama ni mpambanuzi. Chinjo la mwendawazimu au mtoto asiye na akili halifai, na pia mlevi. Kwa kuwa kusudio la kuchinja na kulitaja Jina la Allaah halitoki toka kwa mtu asiye na akili. Hii ndio kauli ya Jumhuwr.
Ibn Hazm amesema: “Chinjo la asiye baleghe halifai. Chinjo hilo ni sawa na la mwendawazimu na mlevi, kwa kuwa si wao wanaosemeshwa na kauli ya sharia katika Neno Lake Ta’aalaa:
"إِلَّا مَا ذَكَّيْتُمْ"
“Isipokuwa mliyewahi kumchinja kihalali (kabla ya kufa)”. [Al-Maaidah : 03]…kwa kuwa wao si wakalifishwa”.
(2) Awe Muislamu, au mtu wa Kitabu (Myahudi au Mnaswara). Chinjo la mwabudu masanamu na viumbe, au mmajusi haliswihi. Hili limekubaliwa na Fuqahaa wote. Sababu ni kuwa asiye Muislamu, halitaji na wala hana habari kabisa na Jina la Allaah, bali mpagani hulitaja jina la asiye Allaah, au huchinja kwa ajili ya masanamu au viabudiwa vyao. Na Allaah Ta’aalaa Amesema:
"حُرِّمَتْ عَلَيْكُمُ الْمَيْتَةُ ...... وَمَا ذُبِحَ عَلَى النُّصُبِ"
“Mmeharamishiwa nyamafu…………. na waliochinjwa kwa ajili ya ‘ibaadah ya waabudiwa”. [Al-Maaidah : 03].
Na mmajusi halitaji Jina la Allaah wakati anachinja.
Ama watu wa Kitabu (Mayahudi na Manaswara), mnyama wanaomchinja watu hawa ni halali kuliwa kutokana na Kauli Yake Ta’aalaa:
"وَطَعَامُ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ حِلٌّ لَّكُمْ"
“Na nyama iliyochinjwa na waliopewa Kitabu ni halali kwenu”. [Al-Maaidah: 05].
Ibn ‘Abbaas amesema: Makusudio ya "طَعَامُهُمْ" katika Aayah hii, ni nyama iliyochinjwa na watu hao, yaani "ذَبَائِحُهُمْ".
Kauli hii inatiliwa nguvu kwa kusema, lau usingelikuwa muradi wa "طَعَامُهُمْ" (chakula chao) kuwa kwa maana ya "ذَبَائِحُهُمْ" (nyama iliyochinjwa na wao), basi kutajwa kwa kuainishwa Watu wa Kitabu hapa kusingelikuwa na maana yoyote, kwa kuwa vyakula vinginevyo vya makafiri wote visivyo nyama ni halali.
Angalizo:
Nyama Ya Myahudi Au Mnaswara Ni Halali Kama Haikujulikana Kwamba Ameitajia Jina Lisilo La Allaah Ta’aalaa
Kama ataitajia jina lisilo la Allaah kama kusema: Kwa jina la masihi, au bikira, au sanamu, basi hailiwi. Na hii ni kwa Neno Lake Ta’aalaa katika kubainisha vilivyoharamishwa:
"وَمَا أُهِلَّ لِغَيْرِ اللَّـهِ بِهِ"
“Na kilichotajiwa asiyekuwa Allaah katika kuchinjwa kwake”. [Al-Maaidah : 03].
3- Asiwe ni mwenye kuhirimia (Hajji) akichinja mawindo ya nchi kavu
Ni haramu kwa aliyehirimia Hajji kujihusisha na mawindo ya nchi kavu, ni sawa kwa kuwinda, au kuchinja, au kuua. Ni haramu pia kwake kumwelekeza mwenzake asiye kwenye Ihraam sehemu alipo mnyama, au kumwashiria upande aliko, kama lilivyobainishwa hili katika Kitabu cha Hijja.
Hivyo basi, chochote atakachokichinja aliyehirimia katika mawindo ya nchi kavu, basi kinakuwa ni mfu, hakifai kuliwa. Vile vile kinakuwa mfu alichokichinja mtu asiye katika ihraam kwa kuelekezewa na aliyehirimia au kuashiriwa wapi alipokuwa mnyama. Allaah Ta’aalaa Anasema:
"يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَقْتُلُوا الصَّيْدَ وَأَنتُمْ حُرُمٌ"
“Enyi walioamini! Msiue mawindo na hali mko katika ihraam”. [Al-Maaidah: 95].
Na Neno Lake:
"وَحُرِّمَ عَلَيْكُمْ صَيْدُ الْبَرِّ مَا دُمْتُمْ حُرُمًا"
“Na mmeharamishiwa mawindo ya nchi kavu madamu mtakuwa katika ihraam”. [Al-Maaidah : 96].
Angalizo:
Lililoharamishwa kwa aliye kwenye ihraam kuchinja, ni mnyama pori anayewindwa tu. Ama wanyama wa kufugwa kama kuku, mbuzi, kondoo na ngamia, hawa hakatazwi, anaweza kuchinja tu. Uharamu ni kwa mnyama pori tu anayewindwa. Ama wengineo, hao wanaingia kiujumla ndani ya wigo wa uhalali. Na hili limekubaliwa na madhehebu yote.
4- Alitaje Jina la Allaah wakati wa kuchinja akikumbuka
Kama atafanya kusudi kutolitaja nailhali anaweza kulitamka, basi mnyama huyo hafai kuliwa kwa mujibu wa kauli ya Jumhuwr. Ama aliyesahau, au akiwa ni bubu, mnyama ataliwa. Allaah Ta’aalaa Amesema:
"وَلَا تَأْكُلُوا مِمَّا لَمْ يُذْكَرِ اسْمُ اللَّـهِ عَلَيْهِ وَإِنَّهُ لَفِسْقٌ"
“Na wala msile katika ambavyo halikutajwa Jina la Allaah (wakati wa kuchinjwa), kwani huo ni ukiukaji wa utiifu kwa Allaah”. [Al-an’aam : 121].
Na kwa Hadiyth ya Raafi’u bin Khadiyj kwamba Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"مَا أَنْهَرَ الدَّمَ وَذُكِرَ اسْمُ اللَّهِ فَكُلْ"
“(Ukichinjia) chochote chenye kuchuruzisha damu sambamba na kutajwa Jina la Allaah, basi kula”. [Hadiyh Swahiyh. Imetajwa nyuma kidogo].
Na kwa ajili hii, Jumhuwr wameshurutisha ulazima wa kulitaja Jina la Allaah wakati wa kuchinja kwa aliyekumbuka hilo na kuwa na uwezo wa kutamka. Lakini Ash-Shaafi’iy anasema kuwa hilo ni jambo linalopendeza (mustahabbu) na si waajib kutokana na Hadiyth ya ‘Aaishah:
"أنَّ قَوْمًا قَالُوْا للنَّبِيِّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وآلهِ وَسَلَّمَ: إِنَّ قَوْمَنَا يْأتُوْنَنَا بِلَحْمٍ لا نَدْرِيْ أَذُكِرَ اسْمُ اللهِ عَلَيْهَ أَمْ لاَ؟ فَقَالَ: سَمُّوْا عَلَيْهِ أَنْتُمْ وَكُلُوا. قَالَتْ: وَكَانُوْا حَدِيْثِي عَهْدٍ بِالْكُفْرِ"
“Kwamba watu fulani walimwambia Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam: Hakika watu wetu wanatuletea nyama ambazo hatujui kama zimetajiwa Jina la Allaah au la. Rasuli akawaambia: Zitajieni nyinyi na kisha zileni”. Akasema ‘Aaishah kwamba watu hao walikuwa bado ndio wametoka kwenye ukafiri. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (2057) na wengineo].
Na lau kama kulitaja Jina la Allaah ni sharti, basi nyama isingelihalalika pamoja na kuweko shaka ya kuwepo kwake, kwa kuwa shaka ndani ya sharti, ni shaka kwa lile lililoshurutishiwa.
Dalili nyingine waliyoitoa kwamba kulitaja Jina la Allaah ni jambo mustahabbu na si waajib ni kwamba Allaah Ta’aalaa Ametuhalalishia nyama za Ahlul Kitaab, na watu hawa wanakuwa hawalitaji Jina la Allaah wakati wa kuchinja. Na wakajibu kuhusu Kauli Yake Ta’aalaa katika Aayah ya 121 ya Suwrat Al-An’aam:
"وَلَا تَأْكُلُوا مِمَّا لَمْ يُذْكَرِ اسْمُ اللَّـهِ عَلَيْهِ وَإِنَّهُ لَفِسْقٌ"
“Na wala msile katika ambavyo halikutajwa Jina la Allaah (wakati wa kuchinjwa), kwani huo ni ukiukaji wa utiifu kwa Allaah”… ya kwamba muradi wake ni wale wanyama ambao wametajiwa jina lisilo la Allaah, kwa maana wanyama waliochinjwa kwa ajili ya masanamu, kwa dalili ya Kauli Yake Ta’aalaa katika Aayah ya 3 ya Suwrat Al-Maaidah:
"وَمَا أُهِلَّ لِغَيْرِ اللَّـهِ بِهِ"
“Na kilichotajiwa asiyekuwa Allaah katika kuchinjwa kwake”. Na muktadha wa Aayah unaonyesha hilo, kwani Allaah Kasema hapo:
"وَإِنَّهُ لَفِسْقٌ"
“kwani huo ni ukiukaji wa utiifu kwa Allaah”. Na hali ambayo ndani yake kunakuweko ukiukaji wa utiifu kwa Allaah, ni huko kutajwa asiyekuwa Allaah kama Alivyosema kwenye Aayah ya 145 ya Suwrat Al-An’aam:
"أَوْ فِسْقًا أُهِلَّ لِغَيْرِ اللَّـهِ بِهِ"
“au kilichochinjwa kinyume na utiifu kwa Allaah kwa kutajiwa asiyekuwa Allaah”.
5- Asilitaje jina la asiye Allaah wakati wa kuchinja
Makusudio ya hili ni kumtukuza asiye Allaah, ni sawa kwa kunyanyua sauti au bila sauti. Mchinjaji asiyelitaja Jina la Allaah mnyama wake anakuwa si halali kuliwa kwa itifaki ya ‘Ulamaa wote. Ni kwa Neno Lake Ta’aalaa:
"حُرِّمَتْ عَلَيْكُمُ الْمَيْتَةُ وَالدَّمُ وَلَحْمُ الْخِنزِيرِ وَمَا أُهِلَّ لِغَيْرِ اللَّـهِ بِهِ"
“Mmeharamishiwa nyamafu, na damu, na nyama ya nguruwe, na kilichotajiwa asiyekuwa Allaah katika kuchinjwa kwake”. [Al-Maaidah : 03].
Kuchinja kwa asiye Allaah ni haramu kutokana na Hadiyth ya Abu At-Twufayl aliyesema: ‘Aliyy (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ)aliulizwa:
"أَخَصَّكُمْ رَسُوْلُ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وآلِهِ وَسَلَّمَ بِشَيْءٍ؟ فَقَالَ : مَا خَصَّنَا رَسُوْلُ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وآلِهِ وَسَلَّمَ بِشَيْءٍ لَمْ يَعُمَّ بِهِ النَّاسَ كَافَّةً إِلاَّ مَا كَانَ فِي قِرَابِ سَيْفِي هّذَا ، قَالَ : فَأَخْرَجَ صَحِيْفَةً مَكْتُوْبٌ فِيْهَا : لَعَنَ اللهُ مَنْ ذَبَحَ لِغَيْرِ اللهِ ، وَ لَعَنَ اللهُ مَنْ سَرَقَ مَنَارَ الأَرْضِ ، وَلَعَنَ اللهُ مَنْ لَعَنَ وَالِدَيْهِ ، وَلَعَنَ اللهُ مَنْ آوَى مُحْدِتًا"
“Je, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekukhusuni kwa jambo lolote (ambalo hakuwaambia watu)? Akasema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakutukhusu kwa jambo lolote ambalo hakuwaenezea habari yake watu wote isipokuwa kilichomo ndani ya ala ya upanga wangu huu. Akatoa karatasi ambayo imeandikwa ndani yake: Allaah Amlaani aliyechinja kwa asiye Allaah, na Allaah Amlaani aliyebadili mipaka ya ardhi (ili adhulumu), na Allaah Amlaani aliyemlaani mzazi wake, na Allaah Amlaani aliyempa hifadhi mzushi”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1978)].