05-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji: Chinjo La Kisharia: Masharti Ya Zana Ya Kuchinjia

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا

 

 Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi

 

 التَّذْكِيَةُ الشَّرْعِيَّةُ

 

Chinjo La Kisharia

 

Alhidaaya.com 

 

 

 

05-Chinjo La Kisharia: Masharti Ya Zana Ya Kuchinjia

 

 

Zana ya kuchinjia ina masharti mawili:

 

1-  Iwe yenye kukata.  Ni sawa ikiwa chuma au kinginecho, au kali au butu, muhimu iwe inakata.  Kwa kuwa makusudio ya kuchinja ni kukata mishipa miwili ya damu ya shingoni, umio na koromeo, pamoja na damu kububujika.

 

 

2-  Isiwe mfupa au kucha.  Ni kwa Hadiyth ya Raafi’u bin Khadiyj aliyesema:  “Nilimwambia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam:

 

"إِنَّا لاَقُو الْعَدُوِّ غَدًا وَلَيْسَتْ مَعَنَا مُدًى ، قَالَ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ : ‏"‏ مَا أَنْهَرَ الدَّمَ وَذُكِرَ اسْمُ اللَّهِ فَكُلْ لَيْسَ السِّنَّ وَالظُّفُرَ ، أَمَّا السِّنُّ فَعَظْمٌ ، وَأَمَّا الظُّفُرُ فَمُدَى الْحَبَشَةِ"

 

“Sisi kesho tunapambana na adui, na hatuna visu (vya kuchinjia).  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:  (Ukichinjia kwa) chochote chenye kuchuruzisha damu, sambamba na kutajwa Jina la Allaah, basi kula isipokuwa jino au kucha.   Ama jino, hilo ni mfupa, na ama kucha, hizo ni kisu cha Wahabeshi (wanachinja kwa kutumia kucha zao)”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imetajwa nyuma].

 

Kuchinja Kwa Ala Au Mashine Za Umeme

Tumesema punde kidogo kuwa ala ya kuchinjia ni lazima iwe inakata, na isiwe mfupa au kucha.  Na hakuna shaka yoyote kwamba mashine za umeme ni kali na zenye kasi katika kufanikisha shughuli ya uchinjaji, na kwa hivyo zina masharti yote yatakikanayo, hivyo zinafaa sana kwa kazi hii.

 

Na hapa kuna swali la kidadisi:  Mashine hizi kutokana na ukali wake na uharaka, zinaweza kukata kabisa kichwa cha mnyama na kukitenganisha na mwili wake. Je, hili linaweza kuwa tatizo?

 

Tunasema:  Hili linafaa.  Hii ni kauli ya Imaam Ahmad, Abu Haniyfah na Ath-Thawriy ambao wanasema kuwa hapa inakuwa imekusanyika kukata kile chenye kubakisha uhai wa mnyama (kichwa) pamoja na chinjo, hivyo inakuwa ni halali.  Na mashine hizi ni kali mno na zinakikata kichwa mara moja.  Hivyo haifikiriki mnyama kufa na roho yake kutoka bila ya kukatwa mishipa ya damu ya shingo yake.

 

 

Share