03-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji: (Vinywaji) Chochote Chenye Kulewesha Ni Pombe

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا

 

 Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi

 

 

الأَشْرِبَةُ

 

Vinywaji 

 

Alhidaaya.com

 

 

 

003-  Vinywaji: Chochote Chenye Kulewesha Ni Pombe:

 

Jumhuwr ya ‘Ulamaa wakiwemo Watu wa Madiynah na Hijaaz, Ahlul Hadiyth, Mahanbali, na baadhi ya Mashaafi’iy, wanaona kwamba kila kinacholewesha, basi ni pombe kihakika, ni sawa kiwe kimetengenezwa kutokana na zabibu, au tende, au ngano, au shayiri au mada nyinginezo.  [Ibn ‘Aabidiyna (5/277), Al-Mudawwanah (6/261), Ad-Dusuwqiy (4/353), Ar-Rawdhwah (10/168) na Al-Mughniy (9/159)].

 

Dalili zao ni:

 

1-  Kauli ya Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

"كُلُّ مُسْكِرٍ حَرَامٌ ، إِنَّ عَلَى اللَّهِ عَهْدًا لِمَنْ يَشْرَبُ الْمُسْكِرَ أَنْ يَسْقِيَهُ مِنْ طِينَةِ الْخَبَالِ . قَالُوا: يَا رَسُولَ اللَّهِ وَمَا طِينَةُ الْخَبَالِ؟ قَالَ: عَرَقُ أَهْلِ النَّارِ أَوْ عُصَارَةُ أَهْلِ النَّار"

 

“Kila kinacholewesha ni haramu.  Na kwa hakika Allaah Amemwekea ahadi mwenye kunywa chenye kulewesha kwamba Atamnywesha “Twiynatul Khabaal”.  Wakauliza ni nini  “Twiynatul Khabaal?”.  Akasema:  Ni jasho la watu wa motoni, au ni usaha wa watu wa motoni.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Muslim (2002), An Nasaaiy (8/327) na Ahmad (3/321)].

 

Na katika tamko la Muslim:

 

"كُلُّ مُسْكِرٍ خَمْرٌ، وَكُلُّ خَمْرٍ مُسْكِرٍ ‏"

 

“Chochote chenye kulewesha ni pombe, na pombe yoyote inalewesha”. 

 

2-  ‘Umar amesema: 

 

"نَزَلَ تَحْرِيمُ اَلْخَمْرِ وَهِيَ مِنْ خَمْسَةٍ: مِنَ اَلْعِنَبِ ، وَالتَّمْرِ ، وَالْعَسَلِ ، وَالْحِنْطَةِ ، وَالشَّعِيرِ.‏ وَالْخَمْرُ: مَا خَامَرَ اَلْعَقْلَ"

 

“Kuharamishwa pombe kulishuka ikiwa inatengenezwa kutokana na mali ghafi tano: Zabibu, tende, asali, ngano na shayiri.  Na khamr (pombe), ni kile kinachoziba akili”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5581) na Muslim (3032)].

 

3-  Ni kwa kuwa iliposhuka Aayaah ya kuharamisha pombe, Maswahaba – ambao ndio wenye kuielewa vizuri lugha yao- walifahamu kwamba chochote kinachoitwa pombe, basi kinaingia ndani ya marufuku hiyo, na hapo ndipo walipomwaga pombe zote zilizotengenezwa kwa tende kavu (tamr) na “rutwab”, kwa kuwa pombe iliharamishiwa Madiynah, na Madiynah hakukuwa na zabibu.  Hawakuwa wakinywa kingine chochote zaidi ya kilichotengenezwa kwa “busr” (tende mbichi) na tende kavu, huku tukizingatia kuwa pombe (khamr) imeitwa hivyo, kwa kuwa inafunika akili, inaipoteza na inaiziba, na hivyo ikahusisha kila chenye kulewesha.   

 

Tunda la mtende lina awamu tano.  “Twal-‘u”, “Balah”, “Busr”, “Rutwab”, na hatimaye “Tamr” ambapo huwa limekomaa barabara na kuwa ngumu. 

 

Na Mashaafi’iy wengi, wanafunzi wa Abu Haniyfah na baadhi ya Wamaalik, wanaona kwamba pombe ni ile yenye kulewesha, lakini iwe imetengenezwa kutokana na maji ya zabibu yanapochachuka, ni sawa yawe yametiwa siagi au la.

 

·        Faida Mbili:

 

Faida ya kwanza:  Kama kingi kinalewesha, basi kidogo chake pia ni haramu.

 

Hili limekubaliwa na Jumhuwr ya ‘Ulamaa wote.  Ni kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

 "كُلُّ مَا أَسْكَرَ حَرَامٌ ، وَمَا أَسْكَرَ الْفَرْقُ فَمِلْءُ الْكَفِّ مِنْهُ حَرَامٌ "

 

“Kila kinacholewesha ni haramu.  Na chochote chenye kulewesha kwa kiasi cha ratili 120, basi hata kwa kiasi cha kujaza kiganja kwacho pia ni haramu”.   [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Abu Daawuwd (3687) na At-Tirmidhiy (1928)].

 

Faida ya pili:  Kila chenye kuondosha akili, basi ni pombe.

 

Ni kwa neno la ‘Umar:   "وَالْخَمْرُ: مَا خَامَرَ اَلْعَقْلَ"  Na khamr (pombe), ni kile kinachoziba akili”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imetajwa nyuma kidogo].

 

Vinavyoingia hapa ni pamoja na hashishi, afyuni, heroin, bangi na mfano wake katika mihadarati.  Vyote hivyo ni haramu kwa Ijmaa ya Fuqahaa kwa Hadiyth ya Ummu Salamah:

 

"أَنَّ النَّبِيَّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وسَلَّمَ نَهَى عَنْ كُلِّ مُسْكِرٍ وَمُفَتِّرٍ "

 

“Kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza kila chenye kulewesha, na kila chenye kupoozesha nguvu za viungo vya mwili”.  [Isnaad yake ni dhwa’iyf.  Imekharijiwa na Abu Daawuwd (3686) na Ahmad (6/254)].

 

Sheikh wa Uislamu amesema:  “Hashishi hii kavu ni haramu, nayo inalewesha.  Na wanaoitumia ni watu wasiojali maasi wala dhambi, kwa sababu ina handasi na inavuruga akili, na kinywaji kinacholewesha kinafanana nayo katika hilo.  Pombe nayo humchemsha mtu akaweza kufanya lolote na kuwa mgomvi, na hashishi hii huleta mpoozo wa viungo vya mwili na udhaifu”.

 

Kisha akaendelea kusema:  “Na mwenye kuihalalisha na akadai kwamba ni halali, basi mtu huyo atatubishwa.  Kama atatubu, basi ataachiwa, na akikataa, basi atauliwa kwa kuwa ameritadi.  Kwani kila chenye kuidhuru akili, basi hicho ni haramu kwa Ijmaa ya Waislamu”.  [Majmuw’ul Fataawaa.  Angalia:   Ibn ‘Aabidiyna (6/457), Subulus Salaam (4/1322) na Az Zawaajir cha Al-Haythamiy (1/172)].

                                   

Share