04-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji: (Vinywaji) Kunywa Pombe Kwa Aliyelazimika

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا

 

 Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi

 

 

الأَشْرِبَةُ

 

Vinywaji 

 

 

Alhidaaya.com 

 

 

 

 

004- Vinywaji: Kunywa Pombe Kwa Aliyelazimika:

 

[Al-Muhallaa (7/426), Fat-hul Qadiyr (9/28), Ad-Dusuwqiy (4/353) na Mughnil Muhtaaj]

 

Kuharamishwa pombe kama tulivyoeleza nyuma, kunakuwa katika hali ya kawaida.  Lakini ikiwa katika hali ya kulazimika, hapo mtu ataruhusiwa kunywa pombe lakini kwa mujibu wa vipimo vya kisheria vinavyohalalisha vilivyoharamishwa.  Ni kama dharura ya kubanwa na kiu kikali ambapo mtu anahofia kufa (na hana maji), au kukabwa na kitu kooni, au kulazimishwa.  Mtu huyo aliyelazimika atakunywa kwa kiasi cha kuondoka tatizo tu.  Allaah Ta’aalaa Anasema:

 

"وَقَدْ فَصَّلَ لَكُم مَّا حَرَّمَ عَلَيْكُمْ إِلَّا مَا اضْطُرِرْتُمْ إِلَيْهِ"

 

Na ilhali Ameshafasilisha waziwazi kwenu yale Aliyokuharamishieni isipokuwa vile mlivyofikwa na dharura navyo.”  [Al-An’aam: 119].

 

Hapa Allaah Ta’aalaa Ameondosha uharamisho wa vya haramu vilivyofasiliwa katika hali ya dharura.  Amesema ni vyote (vinahalalika katika hali hiyo), na wala Hakuainisha kimoja nje ya vingine.  Hivyo haifai kulifanyia umahususi hili.

 

Wamaalik wamekataza kunywa pombe ili kuondosha kiu.  Wanadai kwamba haiondoshi kiu, bali inaongeza joto na ukavu kooni.  Madai yao haya yanajibiwa wakiambiwa kwamba imethibiti kwamba walevi wengi makafiri na watu wasiojali mafundisho ya dini, hawanywi kabisa maji pamoja na kunywa kwao pombe. 

 

Kwa hali yoyote, Aayah hii ni jumuishi kama tulivyosema, na haijuzu kuzuia pombe isinywewe wakati mtu anapohofia kufa kwa kiu.  Linalokatazwa ni kuinywa kwa ajili ya kuondosha kiu cha kawaida, na kama si kiu cha kawaida, basi haijuzu kuzuia (ili kuokoa maisha) kama alivyosema Sheikh wa Uislamu.  [Angalia: Majmuw’ul Fataawaa (14/471)].

 

 

 

Share