06-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji: (Vinywaji) Pombe Ikigeuka Siki
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا
Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi
الأَشْرِبَةُ
Vinywaji
006- Vinywaji: Pombe Ikigeuka Siki:
1- Pombe ikigeuka yenyewe kuwa siki bila ya mtu kukusudia kuichechusha, basi siki hiyo, bila makhitilafiano yoyote kati ya Fuqahaa, inakuwa halali kuitumia. Ni kwa Hadiyth ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
"نِعْمَ الْإِدَامُ الْخَلُّ"
“Kitowezeo bora kabisa ni siki”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (2051), At-Tirmidhiy (1829), An-Nasaaiy (3796) na Abu Daawuwd (3820)].
Ugeukaji wa kuwa siki unajulikana kwa kubadilika ladha ya pombe ambayo ni chungu kuwa na ladha ya tindi kali.
2- Ikiwa pombe itageuzwa siki kwa kutiwa kitu ndani yake kama siki, kitunguu au chumvi, au ikawashiwa moto pembeni yake, kwa hili, ‘Ulamaa wamekhitilafiana katika kauli mbili kuhusu hukmu yake:
[Al-Muhallaa (7/433), Al-Badaai’u (5/114), Al-Qawaaniynul Fiqhiyyah (34), Al-Mughniy (9/145) na Naylul Awtwaar (8/214)].
Kauli ya kwanza:
Haijuzu kuigeuza siki, na siki yenyewe si halali kuitumia. Ni kauli ya ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhwiya Allaah ‘anhu). Pia ni madhehebu ya Shaafi’iy na Hanbali, na riwaayah iliyonukuliwa toka kwa Maalik. Dalili zao ni:
1- Ni kwamba kuigeuza siki ni sawa na kuikumbatia pombe kwa njia ya kujinufaisha, na hii ni kinyume na Amri ya Allaah Aliyetutaka tujiepushe na tujiweke mbali nayo katika Neno Lake:
"فَاجْتَنِبُوهُ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ"
“Basi jiepusheni nayo, mpate kufaulu”. [Al-Maaidah: 90]
2- Hadiyth ya Anas:
"سُئِلَ النَّبِيُّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ عَنِ الْخَمْرِ تُتَّخَذُ خَلاًّ ، فَقَالَ: لاَ "
“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa kuhusu kuitumia pombe ili kutengenezea siki, akasema: Hapana”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1984) na wengineo].
Na katika tamshi:
"أَنَّ أَبَا طَلْحَةَ ، سَأَلَ النَّبِيَّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ عَنْ أَيْتَامٍ وَرِثُوا خَمْرًا ، قَالَ: "أَهْرِقْهَا" . قَالَ: أَفَلاَ نَجْعَلُهَا خَلاًّ ؟ قَالَ: "لاَ".ٍ
“Kwamba Abu Twalha alimuuliza Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu mayatima waliorithi pombe. Rasuli akamwambia: Imwage. Akamuuliza: Kwa nini basi tusiifanye siki? Akasema: Hapana”. [Imekharijiwa na Abu Daawuwd (3675) na Ahmad (3/119)].
Katazo hili linahukumia haramisho. Lau kama ingelikuweko njia ya kuibadilisha ili iweze kutumika kwa manufaa, basi isingelijuzu kuimwaga, lakini pia Rasuli angeliwaelekeza kwa umahususi jambo hilo la kuibadilisha na hususan wakizingatiwa hao ni mayatima ambao ni haramu mtu kufanya lolote la kudhuru mali yao.
3- Mtu mmoja alimuuliza Ibn ‘Abbaas kuhusu pombe inayotengenezwa kutokana na maji ya zabibu, Ibn ‘Abbaas akamwambia:
"أَهْدَى رَجُلٌ لِرَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ رَاوِيَةَ خَمْرٍ ، فَقَالَ لَهُ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: " أَمَا عَلِمْتَ أَنَّ اللَّهَ حَرَّمَهَا؟" . قَالَ لاَ . فَسَارَّهُ رَجُلٌ إِلَى جَنْبِهِ . فَقَالَ لَهُ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ َ: "بِمَ سَارَرْتَهُ؟" . فَقَالَ: "أَمَرْتُهُ أَنْ يَبِيعَهَا" . فَقَالَ لَهُ رَسُولُ اللَّهِ َ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: "إِنَّ الَّذِي حَرَّمَ شُرْبَهَا حَرَّمَ بَيْعَهَا " . فَفَتَحَ الرَّجُلُ الْمَزَادَتَيْنِ حَتَّى ذَهَبَ مَا فِيهِمَا"
“Mtu mmoja alimpa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) zawadi ya kiriba cha pombe. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: Je, hujui kwamba Allaah Ameiharamisha? Akasema hapana. Mtu pembeni yake akamnong’oneza. Rasuli akamuuliza: Umemnong’oneza nini? Akasema: Nimemwamuru aiuze. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: Hakika Yule Aliyeharamisha kuinywa, Ameharamisha (pia) kuiuza”. Mtu yule akayafungulia magudulia mawili mpaka yakabakia matupu”. [Hadiyth Swahiyh. Imetajwa nyuma].
4- ‘Umar (Radhwiya Allaah ‘anhu) alipanda mimbari akasema:
"لا تَأْ كُلْ خَلاًّ مِنْ خَمْرٍ أُفْسِدَتْ ، حَتَّى يَبْدَأَ اللهُ تَعَالَى إِفْسَادَهَا ، وذلِكَ حِيْنَ طَابَ الخَلُّ ، وَلَا بَأْسَ عَلَى امْرِئٍ أَصَابَ خَلاًّ مِنْ أَهْلِ الْكِتَابِ أَنْ يَبْتَاعَهُ ما لَمْ يَعْلَمْ أَنَّهُمْ تَعَمَّدُوا إِفْسَادَهَا"
“Usile siki itokanayo na pombe iliyochachuliwa mpaka Allaah Aichachue (ichachuke yenyewe). Na hakuna ubaya kwa mtu kununua siki kama ataipata kwa Watu wa Kitabu (Ahlul Kitaab) madhali hakujua kwamba waliichachua (pombe yake) kwa makusudi”. [Imekharijiwa na Abu ‘Ubayd katika “Al-Amwaal” (uk. 104)].
Kauli hii imetangaa kwa watu, kwa kuwa ni tangazo la hukmu kwa watu juu ya mimbari, na hakuna yeyote aliyeipinga.
Kauli ya pili:
Inajuzu kuichechusha, na siki yake ni halali kuila. Ni madhehebu ya Hanafiy, kauli yenye nguvu kwa Wamaalik, ni kauli pia ya Abu Muhammad bin Hazm. Dalili zao ni:
1- Kuichechusha ni kuitengeneza ili iweze kufaa na kutumika, na hili linaruhusika kwa kuchukulia qiyaas cha kuisafisha ngozi ya mnyama kwa madawa, na kwa kufanya hivyo ngozi inatwaharika na inafaa kuitumia.
2- Yaliyosimuliwa kwa njia Marfuw’u -kuhusiana na ngozi ya kondoo mfu-:
"إنَّ دِبَاغَهَا يُحِلُّهُ كَمَا يُحِلُّ الخَلُّ الخَمْرَ"
“Hakika kuisafisha kwa madawa kunaihalalisha kama siki inavyohalalisha pombe”. Lakini Hadiyth hii ni Dhwa’iyf, nayo imekharijiwa na Ad-Daaraqutwniy (4/266).
3- Yaliyosimuliwa kwa njia Marfuw’u:
"خَيْرُ خَلِّكُمْ، خَلُّ خَمْرِكُمْ"
“Siki yenu iliyo bora zaidi, ni siki ya pombe yenu”. Hii pia ni Dhwa’iyf. Imekharijiwa na Al-Bayhaqiy katika “Al-Ma-’arifah. Angalia “Naswbur Raayah (4/311).
4- Ni kwa ujumuishi wa neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
"نِعْمَ الْإِدَامُ الْخَلُّ"
“Kitowezeo bora kabisa ni siki”. [Hadiyth Swahiyh. Imetajwa nyuma kidogo].
Katika Hadiyth hii, Rasuli hakutofautisha kati ya pombe inayochechuka yenyewe kuwa siki na pombe inayochechushwa.
5- Kwa kuwa kuigeuza kuwa siki kunaondosha sifa inayoifanya isifae, na kuifanya pombe kuwa na sifa ya kufaa, au kukifanya kitu kiwe kinafaa ni jambo linaloruhusika, kwa kuwa kunafanana na kuimwaga pombe.
· Kauli yenye nguvu:
Linaloonekana ni kuwa dalili za kundi la kwanza ndizo zenye nguvu zaidi. Na kwa muktadha huo, ni haramu kuichechusha pombe ili iwe siki. Lakini ikiwa mtu atapewa zawadi siki iliyotengenezwa, basi hakuna ubaya kwake kuitumia, kwa kuwa sifa ya ubovu inakuwa ishaondoka. Lakini pamoja na hivyo, haijuzu kwake kuinunua, kwa kuwa atakuwa anasaidia jambo la dhambi, na Allaah Amesema:
"وَتَعَاوَنُوا عَلَى الْبِرِّ وَالتَّقْوَىٰ ۖ وَلَا تَعَاوَنُوا عَلَى الْإِثْمِ وَالْعُدْوَانِ ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۖ إِنَّ اللَّـهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ"
“Na shirikianeni katika wema na taqwa, na wala msishirikiane katika dhambi na uadui. Na Mcheni Allaah, hakika Allaah Ni Mkali wa Kuakibu”. [Al-Maaidah: 02].
Ama pombe iliyogeuka yenyewe na kuwa siki, hii haina ubaya kuinunua au kuitumia, kama ilivyotangulia. Na Allaah Ndiye Mjuzi zaidi.