07-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji: (Vinywaji) Haijuzu Kutumia Pombe Kama Dawa

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا

 

 Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi

 

Alhidaaya.com 

 

الأَشْرِبَةُ

 

Vinywaji 

 

 

007-  Vinywaji: Haijuzu Kutumia Pombe Kama Dawa:

 

Jumhuwr ya ‘Ulamaa wameharamisha kutumia pombe (au vyote nyenye kulewesha) kama dawa, bali pia wanaona kwamba mwenye kuinywa kama dawa, basi atapewa adhabu ya kisharia (hadd).  Uharamisho huu unatiliwa nguvu na haya yafuatayo:

 

1-  Hadiyth ya Twaariq bin Suwayd Al-Ju-’ufiy:

 

"أَنَّهُ سَأَلَ النَّبِيَّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ عَنِ الْخَمْرِ ، فَنَهَاهُ أَوْ كَرِهَ أَنْ يَصْنَعَهَا ، فَقَالَ إِنَّمَا أَصْنَعُهَا لِلدَّوَاءِ ، فَقَالَ :‏ ‏إِنَّهُ لَيْسَ بِدَوَاءٍ وَلَكِنَّهُ دَاءٌ"

 

 “Kwamba alimuuliza Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu hukmu ya pombe.  Rasuli akamkataza, au hakuonyesha kufurahishwa yeye kuitengeneza.  Akamwambia:  Ninaitengeneza kwa ajili ya dawa tu, na si kwa jinginelo.  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:  Hiyo si dawa, bali ni ugonjwa”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Muslim (1984)].

 

Sheikh wa Uislamu amesema:  “Maneno haya yanayogusia kuzuia kujitibu kwa kutumia pombe, ni jibu kwa aliyeruhusu.  Na vingine vilivyoharamishwa ni sawa na pombe kwa qiyaas, kinyume na waliotenganisha kati ya viwili hivi”.  [Majmuw’ul Fataawaa (21/568).  Angalia “Mukhtaswar Al-Fataawaa Al-Maswriyyah (uk 490)].

 

Ninasema:  “Itakubalika vipi kwa daktari Muislamu anayejua sharia, amwandikie mgonjwa dawa ambayo Rasuli wake ameielezea kama ni ugonjwa!!”

 

2-  Abu Hurayrah amesema:

 

"نَهَى رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ عَنِ الدَّوَاءِ الْخَبِيثِ"

 

“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza kutumia dawa mbaya hatarishi”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Abu Daawuwd (3870), Ibn Maajah (3459) na Ahmad (2/446)].

 

3-  Toka kwa Abud Dardaai:  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"إِنَّ اللَّهَ أَنْزَلَ الدَّاءَ وَالدَّوَاءَ ، وَجَعَلَ لِكُلِّ دَاءٍ دَوَاءً ، فَتَدَاوُوا وَلَا تداوَوْا بحرامٍ"

 

“Hakika Allaah Ameteremsha ugonjwa na dawa, na Ameuwekea kila ugonjwa dawa yake, basi jitibuni kwa dawa, na wala msijitibu kwa kilichoharamishwa”.  [Imekharijiwa na Abu Daawuwd (3874) na Al-Bayhaqiy (10/5).  Angalia “As-Swahiyhah (1633)].

 

Hadiyth hizi zinafahamisha kwamba ni haramu kujitibu kwa kutumia madawa yaliyoharamishwa kiujumla, na pombe kimahususi.  Lakini kama pataulizwa:  Kwa nini isitumike qaaidah ya:  “Dharura huhalalisha yaliyokatazwa” الضَّرُوْرِيَّاتُ تُبِيْحُ المحْظُوْرَاتِ" , tunasema:  Ni kwa mambo mawili:

 

La kwanza: 

 

Kujitibu kwa kutumia dawa hakuingii katika mlango wa dharura.  Na kwa mujibu wa Jumhuwr ya ‘Ulamaa, kutumia dawa si jambo la wajibu, bali hata Sheikh wa Uislamu amesema:  “Sijapata kumjua yeyote katika watangu wema aliyewajibisha kujitibu kwa dawa”.

 

Linalotilia nguvu maneno haya ni Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas kuhusu mwanamke mweusi aliyekwenda kwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:

 

"إِنِّي أُصْرَعُ ، وَإِنِّي أَتَكَشَّفُ ، فَادْعُ اللهَ تَعَالَى لي. قَالَ: إِنْ شِئْتِ صَبَرْتِ وَلَكِ الْجَنَّةُ ، وَإِنْ شِئْتِ دَعَوْتُ اللهَ تَعَالَى أَنْ يُعَافِيَك"

 

“Mimi nina kifafa, na ninafunukwa nguo (kikinijia), basi niombee kwa Allaah Ta’aalaa.  Akasema:  Ukitaka, unaweza kusubiri na utaipata Jannah, na ukitaka nitakuombea kwa Allaah Akuponye”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5652) na Muslim (2265)].

 

Lau kama kuyaondosha maradhi ni jambo la waajib, basi Rasuli asingemchaguza bibi huyo.   Na hili pia halipingani na amri ya kutumia dawa kwa ajili ya tiba.  Na kuoanisha kati ya haya mawili kunawezekana, tukisema kwamba kuacha kutumia dawa ni bora zaidi ikiwa mtu ataweza kuvumilia na kuwa na subira, lakini kama hawezi kufanya subira juu ya maradhi na ikawa ni dhiki kwake, basi kutumia dawa kutakuwa ni bora zaidi kwa kuwa ubora wa kuacha dawa umeshaondoka kwa kukosa subira.    [Ad-Duraariy Al-Mudhiy-at cha Ash-Shawkaaniy (uk. 393)].

 

La pili:

 

Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameshaeleza uharamu wa kujitibu kwa kilichoharamishwa kama ilivyotangulia.  Na Allaah Ndiye Mjuzi zaidi.

 

·        Angalizo:

 

Sindano ya ganzi (nusu kaputi) na mfano wake ambayo huondosha akili – kama haikupatikana ya kuchukua nafasi yake-, basi itajuzu kuitumia wakati wa dharura isiyoepukika katika shughuli za upasuaji.  [Al-Muntaqaa cha Al-Baajiy (3/149), Mughnil Muhtaaj (4/187), Kashful Qinaa’i (96), Al-Muhallaa (7/508) na Naylul Awtwaar (81/211)].

 

 

 

Share