004-An-Nisaa: Utangulizi Wa Suwrah
004-An-Nisaa: Utangulizi Wa Suwrah
Imeteremka: Madiynah isipokuwa Aayah namba (58) imeteremka Makkah baada ya Fat-h (Ukombozi wa) Makkah.
Idadi Za Aayah: 176
Jina La Suwrah: An-Nisaa
Imeitwa An-Nisaa (Wanawake), na inayodalilisha ni kutajwa katika Hadiyth zilizonukuliwa katika Fadhila, na pia kutajwa katika Aayah namba (1), (4) na nyenginezo. Rejea maelezo katika Faida.
Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:
1-Kuifanya jamii ya Kiislamu kuwa na mipango, na kujenga mahusiano yake, kuhifadhi haki, kuwahimiza watu juu ya Jihaad, na kubatwilisha madai ya kuuwawa Masiyh ‘Iysaa mwana wa Maryam. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]
2-Kuhifadhi haki za waliodhaifu katika jamii nao ni wanawake na yatima.
3-Kubainisha haki za warithi kwa kuwekwa nidhamu za mirathi kuhusu ugawaji wa mali zilizoachwa na aliyefariki.
4-Kuipa umuhimu Aqiydah na Tawhiyd Yake Allaah (سبحانه وتعالى), na kuzungumzia kadhia za imaan, na pia kuzipinga Aqiydah baatwil (potofu).
5-Kuwekwa wazi hoja za kuonyesha usahihi wa Unabiy wa Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم).
6-Kuweka hukmu za uadilifu katika kuhukumu baina ya watu, na kutimiza amana za watu.
7-Kutahadharishwa na wanafiki, na kutajwa baadhi ya sifa zao.
8-Kuongoza katika mambo ya familia, na kupangilia mahusiano kati ya wanandoa wawili, na kutatua matitzo kati yao.
9-Kuitilia umuhimu misingi ya kujenga Dola ya Kiislam, na vinavyoifanya dola kuwa imara na kupigana Jihaad katika Njia ya Allaah.
10-Kuipa umuhimu jambo la kuhifadhi damu za Waislamu na hukmu zake.
11-Kupinga ushirikina wa Manaswara wanaodai kuwa Nabiy ‘Iysaa (عليه السّلام) ni mwabudiwa au mwana wa Allaah.
Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:
1-Suwrah imefunguliwa kwa amri ya kumcha Allaah (سبحانه وتعالى), na kubainishwa kwamba wanaadam wote wanatokana na baba mmoja ambaye ni Aadam (عليه السّلام) na mama mmoja Hawaa. Na pia amri ya kuunga undugu wa uhusiano wa damu.
2-Imeelezwa hukmu na haki za wanawake kama mahari, na imeelezea haki za watoto yatima na jinsi ya kuzitunza mali zao.
3-Imebainishwa Sharia ya Allaah (سبحانه وتعالى) ya mirathi katika ugawaji wa mali aliyoacha aliyefariki kwa familia yake wakiwemo na wazazi.
4-Imebainishwa mambo mengi yanayohusu mahusiano ya mwanamke na mwanamume katika ndoa, miongoni mwa hayo ni: (i) Swala la usimamizi (ii) Uhalali wa kuoana (iii) Hukmu ya ruhusa kwa mwanamume kuoa zaidi ya mke mmoja hadi wake wanne, na pindi asipoweza kutimiza haki basi abakie na mmoja tu. (iv) Haki ya mwanamke katika heshima ya kibinaadam (v) mahari (vi) Uharamu wa kumtelekeza mwanamke (vii) Hukmu za kunyonyesha (viii) Maamrisho ya mema na kukemea mambo machafu (ix) Uhalali wa mahusiano na Watumwa wa kike na mengineyo.
5-Aayah namba (36) imekusanya haki kumi nazo ni: (i) Kumwabudu Allaah na kutokumshirikisha na chochote (ii) Kuwafanyia wazazi wawili ihsaan (iii) Haki za arhaam (jamaa wa uhusiano wa damu) (iv) Haki za yatima (v) Haki za masaakini (vi) Haki za jirani wenye uhusiano wa damu (vii) Haki za jirani wasiokuwa na uhusiano wa damu (viii) Haki za swahibu au rafiki (ix) Haki za msafiri aliyeishiwa masurufu (x) Haki za iliyowamiliki mikono ya kulia.
6-Kwenye mambo yanayohusu mali, Suwrah imezungumzia uharamu wa kula mali za watu kwa dhulma, na kuwatahadharisha watu na mambo hayo, na pia kuwahimiza watu watoe katika njia ya Allaah, na Ahadi ya Allaah (سبحانه وتعالى) kutoa adhabu kwa wanaofanya ubakhili au kuwaamrisha watu kufanya ubakhili.
7-Suwrah imebainisha hukmu nyingi za kisharia pamoja na kuweka wazi uwepesi wa Sharia, na kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Amewafanyia takhfifu (wepesi) Waja Wake, kwa kuchunga udhaifu wao, miongoni mwa hukmu hizo ni: (i) Hukmu za Mirathi (ii) Uharamu wa mlevi akiwa amelewa (iii) Wajibu wa kuoga Janaba kwa anayetaka kuswali (iv) Taratibu za Kutayammam na hukmu zake. (v) Mambo ya jinai kama kuua mtu na fidya pamoja na kubainisha heshima (uzito) ya damu ya Muumini, na malipo kwa ataemuua Muumini kwa makusudi. Na mengineyo.
8-Imebainishwa hukmu katika dola ya Kiislamu, ambao ni uadilifu, utii kwa Allaah na Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) na waliokuwa na mamlaka, na iwe marejeo ya waja inapotokea mizozo; ni Sharia za Allaah kwa kuridhia.
9-Kuna maelezo kuhusu wanafiki na fedheha zao, na kubainisha sifa zao na matendo yao mengi, na nafasi yao ya adhabu kesho Aakhirah, na kwamba wao watakuwa daraja ya chini kabisa motoni.
10-Miongoni mwa maudhui nyenginezo ni: (i) Amri ya kuwa watu wapigane katika njia ya Allaah kwa lengo la kutangaza Kalimah Tukufu ya Allaah, na imetaja fadhila zake kubwa kwa walioenda Jihaad kulinganisha na wasioenda, na inaweka wazi malipo makubwa ya kwenda katika Jihaad (ii) Kuwanusuru wanyonge katika Waumini (iii) Imebainisha baadhi ya hukmu zinazohitajika kuzifahamu kwa anaekwenda Jihaad ikiwemo: Muamala wake pamoja na wale wanaokuja kuomba amani, na hukmu ya Swalaatul-Khawf (Swalaah ya kuhofu katika vita) na kupunguza Swalaah wakiwa vitani.
11-Suwrah imehimiza watu kutenda mema, na kujipamba na tabia njema,
12-Suwrah imezungumzia pia kadhia ya watu kuhukumiana katika Uislamu kwa uadilifu bila ya kupendelea jamaa au tajiri, kutoa ushahidi kwa ajili ya Allaah, kama ulivyo, hata kama madhara yatarudi kwenye nafsi, au kwa wazazi, au kwa ndugu wa karibu, na wala wasifate matamanio ikawa sababu ya kuingia kwenye dhulma (iii) Kutekeleza amana (iv) Mahimizo juu ya Kuwafanyia wema viumbe, na kuchunga haki za wazazi, jirani na ndugu (v) Kuchunga hali za watu wenye mahitaji.
13-Kubainisha uadui wa asili kati ya shaytwaan na mwanaadamu, na jinsi shaytwaan alivyoahidi kuwapoteza baadhi ya waja.
14-Suwrah imehimiza (i) Kumuamini Allaah na Rusuli Wake, na Vitabu Vyake, na kuamini Siku ya Mwisho (ii) Kutekeleza ibaada kwa ajili ya Allaah Pekee na kubainisha uhatari wa ushirikina (iii) Kukataza kuwafanya makafiri kuwa marafiki badala ya Waumini (iv) Amri ya kuwa na taqwa na kushikamana na Dini Yake tukufu.
15-Suwrah imetaja sehemu fulani ya khabari za Manabii wa Allaah (سبحانه وتعالى) .
16-Suwrah imeelezea pia kuhusu Watu wa Kitabu na kubainisha baadhi ya upotevu wao, na adhabu na laana zilizowapata. Pia imetaja baadhi ya tabia yao ya kuvunja ahadi, na kuzikufuru (kuzipinga) Aayah za Allaah. Pia imeelezea miamala yao mibaya na Manabii wa Allaah, ambayo ilipelekea kuwauwa baadhi yao (Manabii), na wengine kuwazidishia sifa, kama walivyofanya kwa Nabiy ‘Iysaa bin Maryam (عليه السلام), na kauli yao ya Utatu.
17-Suwrah imekhitimshwa kwa kubainishwa hukmu ya al-kalaalah (Mirathi ya mtu asiyekuwa na wazazi wala watoto). Rejea Faida:
Fadhila Za Suwrah:
1-Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Alilia Pindi Ibn Mas’uwd (رضي الله عنه) Alipomsomea Aayah Namba (41):
عَنْ عَبْدِ اللَّهِ قَالَ قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم " اقْرَأْ عَلَىَّ ". قَالَ قُلْتُ أَقْرَأُ عَلَيْكَ وَعَلَيْكَ أُنْزِلَ قَالَ " إِنِّي أَشْتَهِي أَنْ أَسْمَعَهُ مِنْ غَيْرِي ". قَالَ فَقَرَأْتُ النِّسَاءَ حَتَّى إِذَا بَلَغْتُ فَكَيْفَ إِذَا جِئْنَا مِنْ كُلِّ أُمَّةٍ بِشَهِيدٍ وَجِئْنَا بِكَ عَلَى هَؤُلاَءِ شَهِيدًا . قَالَ لِي " كُفَّ ـ أَوْ أَمْسِكْ ـ ". فَرَأَيْتُ عَيْنَيْهِ تَذْرِفَانِ.
Amesimulia ‘Abdullaah bin Mas‘uwd (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) aliniambia: “Nisomee!” Nikamwambia: Ee Rasuli wa Allaah! Nikusomee na hali (Qur-aan) imeteremshwa kwako? Akasema: “Naam! Lakini mimi napenda kusikia wengine wakiisoma.” Nikasoma Suwratun-Nisaa mpaka nilipofikia Aayah:
فَكَيْفَ إِذَا جِئْنَا مِن كُلِّ أُمَّةٍ بِشَهِيدٍ وَجِئْنَا بِكَ عَلَىٰ هَـٰؤُلَاءِ شَهِيدًا ﴿٤١﴾
“Basi itakuwaje Tutakapoleta kutoka kila ummah shahidi, na Tukakuleta (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kuwa shahidi juu ya hawa?”
Akasema: “Inatosha, simama hapo.” Nikaona macho yake yanamiminika machozi. [Al-Bukhaariy, Muslim na wengineo]
2-Zimo Aayah Tano Zinazofurahisha Kuliko Dunia Na Yaliyomo Ndani Yake:
عن عبدِ اللهِ بن مَسعودٍ رضِي اللهُ عنه، قال: إنَّ في النِّساء لخمسَ آياتٍ، ما يسرُّني بهنَّ الدُّنيا وما فيها، وقد علِمتُ أنَّ العلماء إذا مرُّوا بها يعرفونها: إِنْ تَجْتَنِبُوا كَبَائِرَ مَا تُنْهَوْنَ عَنْهُ نُكَفِّرْ عَنْكُمْ سَيِّئَاتِكُمْ وَنُدْخِلْكُمْ مُدْخَلًا كَرِيمًا ، وقوله تعالى: إِنَّ اللَّهَ لَا يَظْلِمُ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ وَإِنْ تَكُ حَسَنَةً يُضَاعِفْهَا وَيُؤْتِ مِنْ لَدُنْهُ أَجْرًا عَظِيمًا، وقوله تعالى: إِنَّ اللَّهَ لَا يَغْفِرُ أَنْ يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَلِكَ لِمَنْ يَشَاءُ ، وقوله تعالى وَلَوْ أَنَّهُمْ إِذْ ظَلَمُوا أَنْفُسَهُمْ جَاؤُوكَ فَاسْتَغْفَرُوا اللَّهَ وَاسْتَغْفَرَ لَهُمُ الرَّسُولُ لَوَجَدُوا اللَّهَ تَوَّابًا رَحِيمًا ، وقوله تعالى: وَمَنْ يَعْمَلْ سُوءًا أَوْ يَظْلِمْ نَفْسَهُ ثُمَّ يَسْتَغْفِرِ اللَّهَ يَجِدِ اللَّهَ غَفُورًا رَحِيمًا
Amesimulia ‘Abdullaah Bin Mas’uwd (رضي الله عنه): Hakika katika An-Nisaa, kuna Aayah tano ambazo ni bora kwangu kulikoni dunia na yaliyomo ndani yake, na najua kwamba ‘Ulamaa wanapozipitia huzitambua. Nazo ni:
إِن تَجْتَنِبُوا كَبَائِرَ مَا تُنْهَوْنَ عَنْهُ نُكَفِّرْ عَنكُمْ سَيِّئَاتِكُمْ وَنُدْخِلْكُم مُّدْخَلًا كَرِيمًا ﴿٣١﴾
“Mkijiepusha na madhambi makubwa mnayokatazwa Tutakufutieni madhambi yenu madogo na Tutakuingizeni katika mahali patukufu.” [An-Nisaa (4:31)]
إِنَّ اللَّـهَ لَا يَظْلِمُ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ ۖ وَإِن تَكُ حَسَنَةً يُضَاعِفْهَا وَيُؤْتِ مِن لَّدُنْهُ أَجْرًا عَظِيمًا ﴿٤٠﴾
“Hakika Allaah Hadhulumu hata uzito au chembe (kama atomu). Na ikiwa ni amali njema Huizidisha na Hutoa kutoka Kwake ujira mkuu kabisa.” [An-Nisaa (4:40)]
إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ ۚ وَمَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدِ افْتَرَىٰ إِثْمًا عَظِيمًا ﴿٤٨﴾
“Hakika Allaah Haghufurii kushirikishwa, lakini Anaghufuria yasiyokuwa hayo kwa Amtakae. Na yeyote atakayemshirikisha Allaah basi kwa yakini amezua dhambi kuu kabisa.” [An-Nisaa (4:48)]
وَمَا أَرْسَلْنَا مِن رَّسُولٍ إِلَّا لِيُطَاعَ بِإِذْنِ اللَّـهِ ۚ وَلَوْ أَنَّهُمْ إِذ ظَّلَمُوا أَنفُسَهُمْ جَاءُوكَ فَاسْتَغْفَرُوا اللَّـهَ وَاسْتَغْفَرَ لَهُمُ الرَّسُولُ لَوَجَدُوا اللَّـهَ تَوَّابًا رَّحِيمًا﴿٦٤﴾
“Na Hatukutuma Rasuli yeyote ila atiiwe kwa Idhini ya Allaah. Na lau wao pale walipojidhulumu nafsi zao wangelikujia (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) wakamwomba Allaah maghfirah na Rasuli akawaombea maghfirah, basi wangelimkuta Allaah Ni Mwingi wa Kupokea Tawbah, Mwenye Kurehemu.” [An-Nisaa (4:64)]
وَمَن يَعْمَلْ سُوءًا أَوْ يَظْلِمْ نَفْسَهُ ثُمَّ يَسْتَغْفِرِ اللَّـهَ يَجِدِ اللَّـهَ غَفُورًا رَّحِيمًا ﴿١١٠﴾
“Na atakayetenda ovu au akajidhulumu nafsi yake, kisha akamwomba Allaah maghfirah, basi atamkuta Allaah Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu.” [An-Nisaa (4:110)]
[Imepokewa na Sa’iyd bin Manswuur katika Sunan (4/1297), Atw-Twabaraaniy (9/250), (9069), na Al-Haakim (3194). Al-Haythamiy amesema katika Majma’ Az-Zawaaid (7/14): Watu wake ni watu wa Sahih]
3-Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Aliisoma Katika Qiyaamul-Layl:
عن حُذيفةَ بن اليمانِ، قال: صلَّيتُ مع النبيِّ صلَّى اللهُ عليه وسلَّمَ ذاتَ ليلةٍ، فافتتَحَ البقرةَ، فقلتُ: يركع عند المئةِ، ثم مضى، فقلتُ: يصلي بها في ركعةٍ، فمضى، فقلتُ: يركع بها، ثم افتتح النساءَ فقرأها، ثم افتتح آلَ عمرانَ فقرأها، يقرأ مُترسِّلًا .
Amesimulia Hudhayfah Bin Al-Yamaani (رضي الله عنه) asemaye: “Niliswali na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) usiku mmoja, akafungua kwa Al-Baqarah nikadhani atarukuu katika Aayah mia (100) za mwanzo, naye akapitiliza. Nikadhani ataimaliza Suwrah yote katika rakaa moja, naye akapitiliza. Nikadhani atarukuu kabla hajaimaliza, kisha akaianza An-Nisaa akaisoma, kisha akaingia Aal-‘Imraan, akaisoma, naye akaisoma kwa utuvu na kwa kituo.” [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (772), An Nasaaiy (1664) na Abu Daawuud (874)]
Faida:
1-Suwrah Kuitwa An-Nisaa:
Sababu nyenginezo za Suwrah kuitwa An-Nisaa (Wanawake), ni kutokana hukmu nyingi zinazohusu wanawake, wakiwemo wake na mabinti. Na imeitwa An-Nisaa kwa sababu zama za Jaahiliyyah (kabla ya Uislamu), wanawake walidhulumiwa mno kwa kunyimwa haki zao. Mfano haki za wake na haki za mirathi. Na kuonewa huko kulikuwa hadi kwamba mume akifariki, basi mke anarithiwa kama zinavyorithiwa mali, kisha huyo anayemrithi humfanya mwanamke huyo atakavyo kama ilivyotajwa katika Asbaab-Nuzuwl (Sababu Za Kuteremshwa) Aayah namba (19). Hivyo basi walidharauliwa mno na wakakosa hadhi katika jamii. Na dhulma zao zilipindukia mipaka hadi kwamba ilikuwa, pindi anapozaliwa mtoto wa kike, huuliwa kwa kuzikwa mzima mzima. Rejea An-Nahl (16:58-59), At-Takwiyr (81:8-9).
Pia imeitwa An-Nisaa (Wanawake) kwa sababu ya kukariri neno la An-Nisaa, ambalo limetajwa kwa umoja na likiwa limeegemezwa kwenye neno lingine, na kwa jambo linalotambulika kuwa kitu chochote kikitajwa sana hiyo inajulisha umuhimu wa hicho kitu. [Tafsiyr Ibn Uthaymiyn – Suwrah An-Nisaa (1/8), Al-Itqaan fiy ‘Uluwmil-Qur-aan cha Imam Swuyutwiy (1/197-198).
Miongoni mwa Aayah zilizotajwa An-Nisaa ni Aayah (3-4), (19), (22), (24), (32), (34) na nyenginezo.
2-Kuhusu Al-Kalaalah (Mirathi ya mtu asiyekuwa na wazazi wala watoto):
عَنْ مَعْدَانَ بْنِ، أَبِي طَلْحَةَ أَنَّ عُمَرَ بْنَ الْخَطَّابِ، خَطَبَ يَوْمَ جُمُعَةٍ فَذَكَرَ نَبِيَّ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم وَذَكَرَ أَبَا بَكْرٍ ثُمَّ قَالَ إِنِّي لاَ أَدَعُ بَعْدِي شَيْئًا أَهَمَّ عِنْدِي مِنَ الْكَلاَلَةِ مَا رَاجَعْتُ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم فِي شَىْءٍ مَا رَاجَعْتُهُ فِي الْكَلاَلَةِ وَمَا أَغْلَظَ لِي فِي شَىْءٍ مَا أَغْلَظَ لِي فِيهِ حَتَّى طَعَنَ بِإِصْبَعِهِ فِي صَدْرِي وَقَالَ " يَا عُمَرُ أَلاَ تَكْفِيكَ آيَةُ الصَّيْفِ الَّتِي فِي آخِرِ سُورَةِ النِّسَاءِ " . وَإِنِّي إِنْ أَعِشْ أَقْضِ فِيهَا بِقَضِيَّةٍ يَقْضِي بِهَا مَنْ يَقْرَأُ الْقُرْآنَ وَمَنْ لاَ يَقْرَأُ الْقُرْآنَ .
Imesimuliwa Ma’daan Bin Abiy Twalhah Al-Ya’muriyy, amesema: ‘Umar Bin Al-Khattwaab (رضي الله عنه) alikhutubia Siku ya Ijumaa, akamtaja Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) na akamtaja Abu Bakr, kisha akasema: Hakika sitoacha chochote kilicho muhimu zaidi kama jambo la al-kalaalah, na hakuna jambo nililolirejea rejea zaidi kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) kama nilivyolirejea jambo la al-kalaalah, na hakuwahi kunisisitiza kwenye jambo lolote kama alivyonisisitiza kwenye al-kalaalah, mpaka alininipiga kifuani kwa vidole vyake, na akasema: “Ee ‘Umar! Hivi haikutoshi wewe Aayah (176) iliyoteremka katika Swawyf (majira ya joto) ambayo iko mwishoni mwa Suwrah An-Nisaa?” ‘Umar akasema: Hakika kama nitaishi, nitatoa hukmu ya kuhusu al-kalaalah, kiasi kwamba kila mtu atakayesoma au asiyesoma Qur-aan ataweza kuihukumu. [Muslim (1617)]