005-Al-Maaidah: Utangulizi Wa Suwrah
005-Al-Maaidah: Utangulizi Wa Suwrah
Imeteremka: Madiynah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.
Idadi Za Aayah: 120
Jina La Suwrah: Al-Maaidah
Suwrah imeitwa Al-Maaidah (Meza Ya Chakula), na inayodalilisha ni kutajwa katika Hadiyth zilizonukuliwa katika Fadhila, na pia kutajwa katika Aayah namba (112).
Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:
1-Amri ya kutaka watu kutekeleza ahadi, na tahadhari ya watu kujifananisha na Ahlul-Kitaab juu ya kutotekeleza ahadi. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]
2-Msisitizo juu ya kuhifadhi ahadi na kuzitekeleza.
3-Kubainishwa sharia nyingi.
4-Kuweka mpangilio wa mahusiano juu ya Waislamu wao kwa wao, na juu ya Waislamu na wasiokuwa Waislamu.
Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:
1-Suwrah imefunguliwa kwa Maamrisho ya Allaah (سبحانه وتعالى) kwa Waumini, ya kutimizia ahadi zilizotiliwa mkazo, za kuamini sharia za Dini na kuzifuata, na kutekeleza ahadi wanazopeana Waumini katika biashara na mengineyo. Na uharamisho wa kuwinda katika hali ya Ihraam. Pia maamrisho ya kutokuvuka mipaka ya Allaah na alama Alizoziwekea hiyo mipaka Yake. Na mengineyo yanayohusiana na manaasik ya Hajj. Na ikabainishwa uhalali wa kula nyama za wanyama wa mifugo ambao ni ngamia, ng’ombe, mbuzi na kondoo, isipokuwa wale ambao Allaah (سبحانه وتعالى) Amewaelezea kuwaharamishia, ambao ni mfu, damu, nyama ya nguruwe na wengineo kutokana na sababu kadhaa zilizotjawa katika Aayah namba (3).
2-Kisha ikafuatilia amri ya kutowaogopa makafiri, bali Waumini wamwogope Allaah na kwamba Yeye Allaah (سبحانه وتعالى) Ameshawakamilishia Dini Tukufu ya Uislamu, na kuwatimizia Neema Zake kwa Waumini kwa kuwatoa kwenye giza la ujahili na kuwapeleka kwenye nuru ya imaan, na kwamba Amewaridhia kwamba Uislamu ndio Dini, basi Waumini washikamane nayo imara wala wasiiache.
3-Waumini wamebainishiwa kula vilivyo vizuri, na kutaja Jina la Allaah (سبحانه وتعالى) katika kuchinja mnyama. Na uhalali wa kula vyakula vya Ahlul-Kitaab na uhalali wa kuwaoa wanawake wao, na uharamisho wa uzinifu.
4-Imebainishwa hukmu ya kutia wudhuu na hukmu ya tayammum katika hali kadhaa kama janaba, ugonjwa, safari na katika kumaliza haja msalani, na kwamba hayo ni kutokana na Neema Zake Allaah (سبحانه وتعالى) kutaka kuwatwaharisha Waumini ili wapate kumshukuru.
5-Waumini wameamrishwa wawe wasimamizi wa haki kwa ajili ya kuzitafuta Radhi za Allaah. Wawe mashahidi kwa uadilifu, wala kusiwapelekee kuwachukia watu kuacha kufanya uadilifu, na kwamba wafanye uadilifu hata baina ya maadui na vipenzi kwa daraja moja sawasawa. Na tahadhari ya kudhulumu.
6-Imethibitishwa kwamba Hukmu sahihi ni ya Allaah (سبحانه وتعالى) Pekee, na hakuna hukmu nzuri kuliko hukmu ya Allaah, pamoja na kubainisha kuwa kuhukumiwa na hukmu ya Allaah ni wajibu, na kuziacha hukumu zisizokuwa Zake.
7-Kuweka msisitizo juu ya ‘Aqiydah ya Al-Walaa wa Al-Baraa (Kupendana na kuchukiana kwa ajili ya Allaah), na kutilia mkazo juu ya kuwapenda Waumini, pamoja na kutahadharisha juu ya kuwapenda makafiri.
8-Kupangilia mahusiano ya Waislamu wao kwa wao, na Waislam na Mayahudi na Manaswara.
9-Suwrah imebainisha hukumu nyingi za kisharia na kuziweka wazi. Miongoni mwa hizo ni: Hukmu zinazoelezea mambo ya ibaada na miamala, mikataba, kuchinja, kuwinda, kuhirimia Hajj, ndoa ya Ahlul-Kitaab, hukumu ya kuua na kufanya ufisadi katika ardhi, hukmu ya mwizi, hukmu ya mtu ambaye anakaribia kufariki, kuwashuhudisha Waumini waaminifu wawili kuandika wasia wake. Na hukmu nyenginezo.
10-Suwrah imekusanya baadhi ya visa kikiwemo (i) Kisa cha Baniy Israaiyl na Nabiy Muwsaa (عليه السلام) kuwataka watu wake waingie ardhi tukufu iliyotakaswa ambayo ni Bayt Al-Maqdis, na ukaidi wa wao wa kutokumtii Rasuli wao kuingia mji huo, isipokuwa watu wawili waliomkhofu Allaah. Ikatajwa adhabu za hao walioasi amri ya Rasuli wao. (ii) Kisa cha watoto wawili wa Nabiy Aadam; mmoja wao aliyemuua mwenzake, kisha alipokuwa hakujua la kumfanya, Allaah (سبحانه وتعالى) Akamteremshia kunguru, akawa anafukua shimo katika ardhi ili amzike kunguru mwenzake, ikawa ni fundisho la mwana wa Aadam kutambua kumsitiri na kumzika nduguye aliyemuua. (iii) Kisa cha Wahabashi waliomiminikwa na machozi baada ya kusikia Aayah za Allaah (سبحانه وتعالى), na wakayakinika kwamba Kauli hizo ni haki zilizoteremshwa kutoka kwa Allaah. (iv) Kisa cha Maidah (Meza ya Chakula kutoka mbinguni).
11-Onyo na makemeo kwa mwenye kuritadi. Pia wamekemewa Wanazuoni wa Ahlul-Kitaab kutokuwakataza watu wao wanaotenda madhambi.
12-Wamelaaniwa Mayahudi waliompachika sifa mbaya Allaah (سبحانه وتعالى) kwamba Mkono wa Allaah Umefungwa, na hivyo wamemaanisha kuwa Allaah (سبحانه وتعالى) Amewafanyia ubakihili kwa kuwabania na kutokuwapanulia rizki. Walisema hilo wakati walipopatwa na ukame na ukosefu wa mvua. Allaah (سبحانه وتعالى) Akawaahidi kufarikiana wao kwa wao na kuchukiana mpaka Siku ya Qiyaamah.
13-Kubainisha hali za Ahlul-Kitaab na ile sifa yao ya kuvunja ahadi pamoja na kuvibadilisha Vitabu vya Allaah (سبحانه وتعالى) vilivyoteremshwa, na kujadili baadhi ya itikadi zao potovu, ambazo ni: Kusema kuwa Allaah Ana mwana, na kupinga Unabii wa Muhammad.
14-Allaah (سبحانه وتعالى) Amemthibitisha Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) kutokana na wanaomkanusha Unabii wake, na kumuamrisha anedelea kubalighisha Risala ya Allaah wala asirudi nyuma.
15-Imebainishwa kufru za Manaswara kumsingizia Allaah (سبحانه وتعالى) kwamba Nabiy Iysaa (عليه السّلام) ni mwanawe, na itikadi yao ya utatu. Allaah (سبحانه وتعالى) Akawabainisha hoja za wazi kabisa kwamba Nabiy Iysaa (عليه السّلام) na mama yake ni waja Wake Aliowaumba ambao wanakula na kunywa. Akawataka watubie Kwake ili Awaghufurie kwani Yeye ni Mwingi wa Kughufuria Mwenye Kurehemu.
16-Wamelaaniwa waliokufuru katika Bani Israaiyl kwa maasi yao na kufanya uadui na kufanya ufisadi na udhalimu. Na pia kuridhia kwao kwa maasi na kutokukataza kwao maovu yoyote yaliyokuwa yakitendwa.
17-Imebainishwa hukmu ya kafara ya kiapo na tahadharisho la kuapa ovyo ovyo.
18-Uharamisho wa pombe, kamari, masanamu, kupiga ramli, na imebainishwa hukmu ya mwisho ya ulevi ambayo ni kukoma jambo hilo, na tahadhari ya shaytwaan na uadui wake kwa mwanaadam na uchochezi wake wa kumuingiza katika maasi hayo.
19-Imebainishwa itikadi potofu ya washirikina waliyoyazua ya kuacha kunufaika na baadhi ya wanyama wa mifugo na kuwafanya ni wa masanamu. Na ukaidi wao wa kushikilia kufuata ujahili wa baba zao
20-Imetajwa neema za Allaah (سبحانه وتعالى) juu ya Nabiy ‘Iysaa (عليه السّلام) Alizomjaalia kumuumba bila ya baba tokea utoto wake, na uwezo aliojaaliwa wa kufanya miujiza kadhaa, na kumfundisha kuandika na kusoma, kumfundisha Tawraat na Injiyl na kadhaalika.
21-Suwrah imekhitimishwa kwa kutajwa kisa cha wafuasi wa Nabiy ‘Iysaa (عليه السّلام) kutaka wateremshiwe Al-Maaidah (Meza ya Chakula) kutoka mbinguni wayakinike na iwe ushahidi wao wa ukweli wa Nabiy wa. Nabiy ‘Iysaa (عليه السّلام) aliwaombea kwa Allaah (سبحانه وتعالى) ombi lao hilo na walitimiziwa, wakateremshiwa Al-Maaidah kutoka mbinguni. Kisha Allaah (سبحانه وتعالى) Akatawatahadharisha kuwaadhibu pindi wakikanusha Tawhiyd Yake. Kisha Allaah (سبحانه وتعالى) Akathibitisha malipo mema ya maisha ya kudumu katika Jannah kwa waliompwekesha na waliokuwa wakweli katika niya zao, kwa maneno na matendo yao, na kuwaridhia na kuwajaalia mafanikio makubwa.
Fadhila Za Suwrah:
Ni Suwrah ya mwisho kuteremshwa ila wamekhitilafiana Salaf kuhusu hili. Baadhi ya riwaaya zinasema kuwa ni Suwrah ya mwisho kuteremshwa kama Hadiyth ifuatayo:
عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ عَمْرٍو، قَالَ آخِرُ سُورَةٍ أُنْزِلَتْ سُورَةُ الْمَائِدَةِ . قَالَ أَبُو عِيسَى هَذَا حَدِيثٌ حَسَنٌ غَرِيبٌ
Amesimulia ‘Abdullaah bin ‘Amrw: Suwrah ya mwisho kuteremshwa ni Al-Maaidah. [At-Tirmidhiy na amesema: Hii ni Hadiyth Hasan Ghariyb]
Riwaaya nyenginezo zimetajwa ni Suwrah An-Naswr kama walivyopokea Imaam Al-Bukhaariy na Muslim. Na riwaaya nyenginezo zimetajwa At-Tawbah. Na Allaah Mjuzi zaidi.
Faida:
Suwrah imeitwa Al-Maaidah (Meza Ya Chakula) kwa kutajwa wafuasi wa Nabiy ‘Iysaa (عليه السّلام) walipomtaka awape dalili itayojulisha ukweli wa Unabii wake, na iwe kama sikukuu kwao, basi wakataka Allaah (سبحانه وتعالى) Ateremshe meza ya chakula kutoka mbinguni. Na hakika Allaah (سبحانه وتعالى) Aliteremsha meza ya chakula kama walivyotaka. Rejea Aayah (112-115).