007-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo Na Hukmu Za Kuangalia: Mavazi Na Mapambo Kwa Wanaume:Vivazi Vilivyokatazwa Kwa Wanaume Kuvivaa: Kuvaa Hariri Safi Isiyochanganywa

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

 

كِتَابُ اللِّبَاسِ وَالزِّيْنَةِ  وَأَحْكَامُ النَّظَرِ

 

 Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo Na Hukmu Za Kuangalia 

 

 

اللِّبَاسُ وَالزِّيْنَةُ للرِّجَالِ 

Mavazi Na Mapambo Kwa Wanaume 

 

Alhidaaya.com 

 

 

 

007-  Mavazi Na Mapambo Kwa Wanaume: Vivazi Vilivyokatazwa Kwa Wanaume Kuvivaa:  Kuvaa Hariri Safi Isiyochanganywa:

 

 

 

Jumhuwr ya ‘Ulamaa -bali baadhi yao wamenukuu ‘Ijmaa- kwamba ni haramu kuvaa hariri safi kwa wanaume -isipokuwa kwa dharura- kutokana na Hadiyth zinazoeleza wazi kuhusu uharamu wa hilo.  Kati ya Hadiyth hizo ni:

 

1-  Hadiyth ya Anas, kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:  

 

"لاَ تَلْبَسُوا الْحَرِيرَ ، فَإِنَّهُ مَنْ لَبِسَهُ فِي الدُّنْيَا لَمْ يَلْبَسْهُ فِي الآخِرَة"

 

 “Msivae hariri, kwa sababu, mwenye kuivaa duniani, hatoivaa akhera”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5833) na Muslim (2069)].

 

Ni dhahiri kwamba kutoivaa akhera ni kinaya cha kutoingia mvaaji Peponi.  Kwani Allaah Ta’aalaa Amesema kuhusiana na watu wa Peponi:

 

"وَلِبَاسُهُمْ فِيهَا حَرِيرٌ"

 

“Na mavazi yao humo ni hariri”.  [Al-Hajji: 23].

 

2-  Hudhayfah bin Al-Yamaan:  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"لَا تَلْبَسُوا الْحَرِيرَ وَلَا الدِّيبَاجَ ، وَلَا تَشْرَبُوا فِي آنِيَةِ الذَّهَبِ وَالْفِضَّةِ ، وَلَا تَأْكُلُوا فِي صِحَافِهَا، فَإِنَّهَا لَهُمْ فِي الدُّنْيَا ، وَلَنَا فِي الْآخِرَةِ"

 

“Msivae hariri wala dibaji (brocade), na wala msinywee chombo cha dhahabu au fedha, na wala msilie katika sahani zake, kwani hizo ni zao hapa duniani, na za kwetu huko akhera”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5426) na Muslim (2067)].

 

3-  ‘Umar bin Al-Khattwaab:  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"إِنَّمَا يَلْبَسُ الْحَرِيرَ فِي الدُّنْيَا مَنْ لَا خَلَاقَ لَهُ فِي الْآخِرَة"

 

“Hakika si vinginevyo, anayevaa hariri hapa duniani, ni yule asiye na fungu lolote akhera”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5835) na Muslim (2068)].

 

4-  Abu Muwsaa Al-Ash-‘ariyy:  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: 

 

"حُرِّمَ لِبَاسُ الْحَرِيرِ وَالذَّهَبِ عَلَى ذُكُورِ أُمَّتِي وَأُحِلَّ لإِنَاثِهِمْ"

 

“Kuvaa hariri na dhahabu kumeharamishwa kwa wanaume wa umati wangu, lakini kwa wanawake wao kumehalalishwa”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Abu Daawuwd (4057), At-Tirmidhiy (1720), An-Nasaaiy (8/160) na Ibn Maajah (3595)].

 

Na kwa upande mwingine, baadhi ya watu wamenukuliwa wakisema kwamba ni halali wanaume kuvaa hariri.  Dalili zao ni:

 

1-  Hadiyth ya ‘Uqbah bin ‘Aamir,  amesema:

 

"أُهْدِيَ لِرَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَرُّوجُ حَرِيرٍ، فَلَبِسَهُ، ثُمَّ صَلَّى فِيهِ، ثُمَّ انْصَرَفَ فَنَزَعَهُ نَزْعًا شَدِيدًا كَالْكَارِهِ لَهُ ثُمَّ قَالَ : لاَ يَنْبَغِي هَذَا لِلْمُتَّقِينَ"

 

“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipewa zawadi ya “Farruji” la hariri, akalivaa, kisha akaswali nalo.  Alipomaliza kuswali, alilivua kwa  haraka sana kama vile amelichukia, kisha akasema:  Hili halifai kwa wamchao Allaah.”  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (375) na Muslim (2075)].

 

“Farruji” ni nguo iliyobana mikono na kiuno, na nyuma imepasuliwa.

 

Hili linajibiwa:  Kwamba alilivaa kabla ya kuharamishwa, kwani haiwezekani idhaniwe kuwa Rasuli anaweza kulivaa baada ya kuharamishwa, ni sawa iwe kwenye Swalaah au kwengineko. 

 

2-  Hadiyth ya Al-Mis-war bin Makhramah kwamba:

 

"أَنَّهَا قُدِّمَتْ لِلنَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَقْبِيَةٌ ، فَذَهَبَ هُوَ وَأَبُوْهُ إِلَى النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ لِشَيْءٍ مِنْهَا ، فَخَرَجَ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ وَعَلَيْهِ قُبَاءٌ مِنْ دِيْبَاجٍ مُزَرَّرَةٌ بِالذَّهَبِ، فَقَالَ :‏"‏يَا مَخْرَمَة ،خَبَأْنَا هَذَا لَكَ‏" ، وَجَعَلَ يُرِيْهِ مَحَاسِنَهُ ، وَقَالَ: أَرَضِيَ مَخْرَمَةٌ؟‏‏

 

“Kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliletewa majoho kadhaa ya hariri.  Akaenda yeye (Mis-war) na baba yake kwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ili kuambulia chochote katika majoho hayo.  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akatoka akiwa amevaa joho fupi la hariri lenye vifungo vya dhahabu.  Akasema:  Ee Makhramah! Tumekuwekea hili”.  Akaanza kumuonyesha lilivyo zuri, na akauliza:  Makhramah amelifurahia?  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (3127), Al-Bayhaqiy (3/273) na At-Twahaawiy (4/243)].

 

Hadiyth hii inajibiwa:  Kwamba Hadiyth nyingine ziko wazi katika kuharamisha, juu ya msingi wa kwamba hakuna mvutano kuwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anavaa hariri, kisha uharamisho ukawa ni mwisho wa mambo mawili.  [Ahkaamul ‘Awrat cha Musaa’id Al-Faalih (uk. 183)].

 

·        Kiasi Cha Hariri Kinachoruhusiwa Katika Nguo

 

Mwanaume anaruhusiwa kuvaa nguo ikiwa na mstari wa hariri wa kiasi cha vidole vinne na chini ya hapo kwa mujibu wa kauli ya Jumhuwr ya ‘Ulamaa.  Ni kwa Hadiyth ya Abu ‘Uthmaan:.

 

"كَتَبَ إِلَيْنَا عُمَرُ وَنَحْنُ بِأَذْرَبِيجَانَ : أَنَّ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ نَهَى عَنْ لُبْسِ الْحَرِيرِ إِلاَّ هَكَذَا ، وَصَفَّ لَنَا النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ إِصْبَعَيْهِ‏.‏ وَرَفَعَ زُهَيْرٌ الْوُسْطَى وَالسَّبَّابَةَ‏"

 

‘Umar bin Al-Khattwaab alituandikia barua tukiwa Azerbaijan isemayo:  “Kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza kuvaa hariri isipokuwa kwa kiasi hiki, na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaashiria vidole vyake viwili”.  Na Zuhayr akanyanyua cha kati na cha shahada.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5829) na Muslim (2069)]. 

 

Na katika tamko la Muslim:

 

"نَهَى عَنْ لُبْسِ اَلْحَرِيرِ إِلَّا مَوْضِعَ إِصْبَعَيْنِ، أَوْ ثَلَاثَةٍ، أَوْ أَرْبَعَةٍ"

 

“Amekataza kuvaa hariri isipokuwa kwa kiasi cha vidole viwili, au vitatu, au vinne”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Muslim (2069)]. 

 

Ikiwa kiasi cha hariri katika nguo kitazidi vidole vinne, basi itakuwa ni haramu.

 

·        Inaruhusiwa Kuvaa Hariri Wakati Wa Dharura

[Ibn ‘Aabidiyna (5/224), Al-Khurashiy (1/252), Al-Majmuw’u (4/440), Al-Mughniy (2/306) na Zaadul Ma’aadiy (3/103)].

 

Jumhuwr ya ‘Ulamaa -kinyume na Wamaalik na riwaayah toka kwa Ahmad- wamejuzisha kuvaa hariri wakati wa dharura kama katika hali ya ugonjwa, au kuwashwa ngozi na mfano wake.  Ni kwa Hadiyth ya Anas aliyesema:

 

"رَخَّصَ النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم لِلزُّبَيْرِ وَعَبْدُ الرَّحْمنِ في لُبْسِ الحَرِيْرِ لِحَكَّةٍ بِهِمَا"

 

“Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwaruhusu Zubayr na ‘Abdulrahmaan kuvaa hariri kutokana na upele uliokuwa ukiwasumbua”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5839) na Muslim (2076)]. 

 

Kwa upande wa Wamaalik, wao wanasema kwamba haijuzu kuvaa hariri kwa ajili ya upele na mfano wake, na kwamba ruksa hiyo ilikuwa mahsusi kwa Maswahaba hao wawili tu (Radhwiya Allaah ‘anhumaa)!!

 

Lililo sahihi ni kauli ya Jumhuwr, kwa kuwa asili ni kutohusisha watu pasi na wengine, na ruksa inapotolewa kwa baadhi ya watu kwa sababu fulani, basi ruksa hiyo itavuka kwenda kwa kila ambaye imepatikana kwake sababu hiyo, kwa kuwa hukmu inaenea kwa kuenea sababu yake.  Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

 

 

·        Hairuhusiwi Kutandika Hariri

 

Hudhayfah amesema: 

 

"نَهَانَا النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَنْ نَشْرَبَ فِي آنِيَةِ الذَّهَبِ وَالْفِضَّةِ وَأَنْ نَأْكُلَ فِيهَا ، وَعَنْ لُبْسِ الْحَرِيرِ وَالدِّيبَاجِ وَأَنْ نَجْلِسَ عَلَيْهِ"

 

“Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametukataza kunywea au kulia chombo cha dhahabu au fedha, na kuvaa au kukalia hariri na dibaji (brocade).  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5837)].

 

Haya ndiyo waliyosema Jumhuwr -kinyume na Abu Haniyfah-, kwa kuwa sababu ya kuharamisha kuvaa ipo pale pale katika kukalia, na kwa kuwa pia kuvaa kukiharamishwa -nalo ni jambo la lazima kwa mtu- basi jinginelo linastahiki uharamu zaidi.  Na hii ni hukmu inayowahusu wanaume tu.  Ama wanawake, wao inajuzu kuvaa. 

 

 

 

Share