009-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo Na Hukmu Za Kuangalia: Mavazi Na Mapambo Kwa Wanaume:Vivazi Vilivyokatazwa Kwa Wanaume Kuvivaa: Je, Ni Karaha Kwa Mwanaume Kuvaa Vazi Jekundu?
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ اللِّبَاسِ وَالزِّيْنَةِ وَأَحْكَامُ النَّظَرِ
Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo Na Hukmu Za Kuangalia
اللِّبَاسُ وَالزِّيْنَةُ للرِّجَالِ
Mavazi Na Mapambo Kwa Wanaume
009- Mavazi Na Mapambo Kwa Wanaume: Vivazi Vilivyokatazwa Kwa Wanaume Kuvivaa: Je, Ni Karaha Kwa Mwanaume Kuvaa Vazi Jekundu?:
‘Ulamaa wamekhitalifiana kwa kauli nyingi juu ya hukmu ya mwanaume kuvaa nguo nyekundu. Al-Haafidh amezidhibiti katika kauli saba ambazo zinaweza kuchujwa na kuwekwa katika kauli mbili:
Kauli ya kwanza: Ni karaha kuvaa nguo nyekundu, nayo ni madhehebu ya Hanafiy na Hanbali. Dalili zao ni:
1- Hadiyth ya Al-Baraa bin ‘Aazib: amesema:
"أَمَرَنَا النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ بِسَبْعٍ وَنَهَانَا عَنْ سَبْعٍ – فَذَكَرَ مِنْهَا- المَيَاثِرُ الحُمُرُ"
“Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuamuru mambo saba na ametukataza mambo saba -kati ya aliyoyakataza- ni matandiko myekundu (ya kukalia juu ya mnyama)”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5849) na Muslim (2066)].
Katika riwaayah ya Hadiyth ya ‘Imraan bin Haswiyn imekuja:
"نَهَى عَنْ مِيثَرَةِ الأُرْجُوَان"
“Amekataza tandiko la hariri la rangi nyekundu iliyokoza (la kukalia juu ya mnyama)”.
2- Yaliyosimuliwa toka kwa ‘Abdullaah bin ‘Umar aliyesema:
"مَرَّ عَلَى النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ رَجُلٌ عَلَيْهِ ثَوْبَانِ أَحْمَرَانِ فَسَلَّمَ عَلَيْهِ فَلَمْ يَرُدَّ النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم عَلَيْهِ"
“Mtu mmoja alipita mbele ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa amevaa nguo mbili nyekundu, akamsalimia, lakini Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakumjibu”. Lakini ni Dhwa’iyf. [Hadiyth Dhwa’iyf. Imekharijiwa na At-Tirmidhiy (2807) na Abu Daawuwd (4069)].
3- Mwanamke mmoja wa Baniy Asad amesema:
"كُنْتُ يَوْمًا عِنْدَ زَيْنَبَ امْرَأَةِ رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ وَنَحْنُ نَصْبُغُ ثِيَابًا لَهَا بِمَغْرَةٍ ، فَبَيْنَمَا نَحْنُ كَذَلِكَ إِذْ طَلَعَ عَلَيْنَا رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ ، فَلَمَّا رَأَى الْمَغْرَةَ رَجَعَ ، فَلَمَّا رَأَتْ ذَلِكَ زَيْنَبُ عَلِمَتْ أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَدْ كَرِهَ مَا فَعَلَتْ فَأَخَذَتْ فَغَسَلَتْ ثِيَابَهَا وَوَارَتْ كُلَّ حُمْرَةٍ ، ثُمَّ إِنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ رَجَعَ فَاطَّلَعَ ، فَلَمَّا لَمْ يَرَ شَيْئًا دَخَلَ"
“Nilikuwa siku moja kwa Zaynab mke wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Tulikuwa tunaitia nguo yake rangi kwa kutumia poda nyekundu. Na wakati tukiwa tunaendelea na shughuli hiyo, mara Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaingia. Alipoona poda nyekundu alirudi, hakuingia. Zaynab alipoona hivyo, akajua kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amechukia hayo anayoyafanya. Akaichukua nguo yake akaiosha hadi wekundu wote ukaondoka. Kisha Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alirejea tena, akachungulia, alipoona hakuna kitu, aliingia”. Hadiyth hii ni Dhwa’iyf. [Imekharijiwa na Abu Daawuwd (4071), Ibn Abiy ‘Aaswim katika Al-Aahaad (3096) na At-Twabaraaniy (24/25-57/185)].
4- Yaliyopokelewa Marfuw’an toka kwa Raafi’u bin Yaziyd Ath-Thaqafiy:
"إِنَّ الشَّيْطَانَ يُحِبُّ الحُمْرَةَ ، وَإِيَّاكُمْ وَالحُمْرَةَ وَكُلَّ ثَوْبٍ ذِيْ شُهْرَةٍ"
“Hakika shetani anapenda rangi nyekundu, basi tahadharini na wekundu na kila kivazi cha kutafutia umashuhuri”. Hii pia ni Dhwa’iyf. [At-Twabaraaniy ameikhariji katika Al-Awsatw (7708)].
Kauli ya pili: Inafaa kuvaa nguo nyekundu. Haya ni madhehebu ya Maalik na Shaafi’iy. Dalili zao ni:
1- Hadiyth ya Al-Baraa:
" كَانَ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ مَرْبُوعًا، وَقَدْ رَأَيْتُهُ فِي حُلَّةٍ حَمْرَاءَ مَا رَأَيْتُ شَيْئًا أَحْسَنَ مِنْهُ"
“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa na kimo cha wastani. Niliwahi kumwona akiwa amevaa vazi jekundu la juu na chini, sijapata kuona kitu kizuri zaidi kuliko yeye. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5848). Ina Hadiyth mwenza ya Jaabir iliyoko kwa At-Tirmidhiy (2811)].
2- Jaabir bin Samurah:
رَأَيْتُ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم فِي لَيْلَةٍ إِضْحِيَانٍ فَجَعَلْتُ أَنْظُرُ إِلَى رَسُولِ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم وَإِلَى الْقَمَرِ وَعَلَيْهِ حُلَّةٌ حَمْرَاءُ فَإِذَا هُوَ عِنْدِي أَحْسَنُ مِنَ الْقَمَرِ"
“Nilimwona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika usiku angavu wa mbalamwezi. Nikaanza kumwangalia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) huku nikiuangalia mwezi naye akiwa amevaa vazi jekundu, nikamwona kwa hakika ni mzuri kuliko mwezi. [Hadiyth Dhwa’iyf. Imekharijiwa na At-Tirmidhiy (2811), An-Nasaaiy katika Al-Kubraa (9640), Abu Ya’alaa (7477) na Al-Haakim (4/207)].
Wa kauli ya mwanzo wenye kusema ni karaha kuvaa nyekundu wamejibu wakisema kwamba vazi jekundu alilolivaa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) halikuwa jekundu lote, bali lilichanganyika na rangi nyingine.
Kauli Yenye Nguvu:
Ninaloliona mimi ni kuwa dalili za kundi la mwanzo wanaosema ni karaha kuvaa nyekundu, hazina nguvu. Kwa msingi huo, hakuna ubaya kuvaa nyekundu. Lakini, lau mtu ataacha kuvaa nyekundu iliyokoza ambayo haikuchanganyika na rangi yoyote, itakuwa bora na akiba zaidi ili kutoka nje ya duara la mvutano. Allaah Ndiye Mjuzi zaidi.