013-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo Na Hukmu Za Kuangalia: Mavazi Na Mapambo Kwa Wanaume: Adabu Za Kuvaa

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

 

كِتَابُ اللِّبَاسِ وَالزِّيْنَةِ  وَأَحْكَامُ النَّظَرِ

 

 Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo Na Hukmu Za Kuangalia 

 

 

 

 

اللِّبَاسُ وَالزِّيْنَةُ للرِّجَالِ 

Mavazi Na Mapambo Kwa Wanaume 

 

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

013-  Mavazi Na Mapambo Kwa Wanaume:  Adabu Za Kuvaa:

 

 

 

1-  Kuwa na hima ya kuvaa vivazi vizuri kwa mwenye uwezo

 

Al-Ahwasw alimnukulu baba yake akisema:

 

"أَتَيْتُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ وَعَلَى ثَوْبٌ دُونٌ ، فَقَالَ لِي: أَلَكَ مَالٌ؟ قُلْتُ: نَعَمْ. قَالَ: مِنْ أَيِّ الْمَالِ؟ قُلْتُ: مِنْ كُلِّ الْمَالِ قَدْ أَعْطَانِي اللَّهُ منَ الإِبلِ وَالْبَقَرِ وَالْخَيْلِ وَالرَّقِيقِ. قَالَ: فَإِذَا آتَاكَ اللَّهُ مَالًا فَلْيُرَ أَثَرُ نِعْمَةِ اللَّهِ عَلَيْكَ وَكَرَامَتِهِ"

 

“Nilimwendea Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) nikiwa nimevaa nguo duni.  Akaniuliza:  Je, una mali?  Nikasema:  Na’am.  Akauliza:  Ni mali ya aina gani?  Nikasema:  Ni za aina zote, Allaah Ameniruzuku ngamia, ng’ombe, farasi na watumwa.  Akasema:  Allaah Akikuruzuku mali, basi athari ya Neema ya Allaah ionekane kwako pamoja na na Hisani Yake”.   [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Abu Daawuwd (4063) na An-Nasaaiy (5224).  Ina Hadiyth wenza toka kwa ‘Abdullaah bin ‘Amri, Abu Hurayrah, ‘Imraan bin Haswiyn, Ibn Mas-‘uwd na wengineo].

 

Na Allaah Amesema:

 

قُلْ مَنْ حَرَّمَ زِينَةَ اللَّـهِ الَّتِي أَخْرَجَ لِعِبَادِهِ وَالطَّيِّبَاتِ مِنَ الرِّزْقِ ۚ قُلْ هِيَ لِلَّذِينَ آمَنُوا فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا خَالِصَةً يَوْمَ الْقِيَامَةِ

 

“Sema:  Nani aliyeharamisha Mapambo ya Allaah ambayo Amewatolea Waja Wake na vilivyo vizuri katika riziki?  Sema:  Hivyo ni kwa ajili ya wale walioamini katika uhai wa dunia; makhsusi (kwa Waumini) Siku ya Qiyaamah”.  [Al-A’araaf: 32].

 

Kuvaa nguo nzuri haimaanishi mtu ana kibri.  Toka kwa Ibn Mas-‘uwd:  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

 "لاَ يَدْخُلُ الْجَنَّةَ مَنْ كَانَ فِي قَلْبِهِ مِثْقَالُ ذَرَّةٍ مِنْ كِبْرٍ ‏ ‏.‏ قَالَ رَجُلٌ:  إِنَّ الرَّجُلَ يُحِبُّ أَنْ يَكُونَ ثَوْبُهُ حَسَنًا وَنَعْلُهُ حَسَنَةً ‏.‏ قَالَ ‏: إِنَّ اللَّهَ جَمِيلٌ يُحِبُّ الْجَمَالَ ، الْكِبْرُ بَطَرُ الْحَقِّ وَغَمْطُ النَّاسِ"

 

“Haingii Peponi mtu ambaye ndani ya moyo wake kuna kibri cha uzito wa sisimizi.  Mtu mmoja akasema:  Je ikiwa mtu anapenda nguo zake kuwa nzuri na viatu vyake kuwa vizuri?.  Akasema:  Hakika Allaah Ni Mzuri, Anapenda vitu vizuri, lakini kibri ni kuikataa haki na kudharau watu”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Muslim (91), Abu Daawuwd (4092) na wengineo].

 

2-   Asinunue mtu mavazi ya ziada bila kuhitajia

 

Allaah Ta’aalaa Amesema:

 

يَا بَنِي آدَمَ خُذُوا زِينَتَكُمْ عِندَ كُلِّ مَسْجِدٍ وَكُلُوا وَاشْرَبُوا وَلَا تُسْرِفُوا ۚ إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الْمُسْرِفِينَ ﴿٣١﴾

 

31.  Enyi wana wa Aadam!  Chukueni mapambo yenu katika kila Masjid.  Na kuleni na kunyweni, na wala msifanye israfu.  Hakika Yeye (Allaah) Hapendi wanaofanya israfu.  [Al-A’araaf: 31].

 

Na Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"كُلُوا وَاشْرَبُوا وَتَصَدَّقُوا وَالْبَسُوا مَا لم يُخَالِطْهُ إِسْرَافٌ وَلَا مَخِيْلَة"ٌ

 

“Kuleni, kunyweni, toeni sadaka na vaeni, mradi tu isiwepo israfu wala majivuno ndani yake”.  [Hadiyth Hasan.  Al-Bukhaariy ameifanya Mu’allaq kwenye Kitabu Cha Mavazi, na An-Nasaaiy kaifanya Mawswuul (2559) na Ibn Maajah kwa Sanad Hasan].

 

3-  Kuomba du’aa wakati wa kuvaa nguo mpya

 

Abu Sa’iyd Al-Khudriyy amesema:

 

"كَانَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ إِذَا اسْتَجَدَّ ثَوْبًا سَمَّاهُ بِاسْمِهِ عِمَامَةً أَوْ قَمِيصًا أَوْ رِدَاءً ، ثُمَّ يَقُولُ : اللَّهُمَّ لَكَ الْحَمْدُ أَنْتَ كَسَوْتَنيهِ ، أَسْأَلُكَ خَيْرَهُ وَخَيْرَ مَا صُنِعَ لَهُ ، وَأَعُوذُ بِكَ مِنْ شَرِّهِ وَشَرِّ مَا صُنِعَ لَهُ"

 

“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anapopata nguo mpya huipa jina lake, ikiwa kilemba au kanzu au shuka ya juu, kisha husema:  Ee Allaah!  Ni Yako himdi, Wewe Ndiye Umenivisha, nakuomba kheri yake na kheri iliyotengenezewa, na najilinda Kwako na shari yake na shari iliyotengenezewa”.  [Hasan Lishawaahidihi.  Imekharijiwa na Abu Daawuwd (4020), At-Tirmidhiy (1767), na An-Nasaaiy (1382).  Ina Hadiyth mwenza inayoizatiti].

 

4-  Kuanza kuvaa kwa upande wa kulia

 

‘Aaishah amesema:

 

"كَانَ اَلنَّبِيُّ ‏صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ ‏يُعْجِبُهُ اَلتَّيَمُّنُ فِي تَنَعُّلِهِ، وَتَرَجُّلِهِ، وَطُهُورِهِ، وَفِي شَأْنِهِ كُلِّهِ"

 

“Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kulikuwa kunampendeza kuanza kwa kulia akivaa viatu, akichana nywele, akijitwaharisha, na katika mambo yake yote”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (426) na Muslim (268)].

 

 

5-  Asitembee mtu kwa kiatu kimoja

 

Abu Hurayrah:  “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"لَا يَمْشِي أَحَدُكُمْ فِي نعلٍ واحدةٍ ، لِيَنْعَلْهُمَا جَمِيعًا ،  أَوْ لِيُحْفِيَهُمَا جَمِيعًا"

“Mmoja wenu asitembee kwa kiatu kimoja.  Ima avivae vyote viwili, au avivue vyote viwili”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5855) na Muslim (2097)].

 

“Mmoja wenu asitembee kwa kiatu kimoja.  Ima avivae vyote viwili, au avivue vyote viwili”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5855) na Muslim (2097)].

 

 

 

 

Ukaraha katika katazo hili -na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi- ni kwa ajili ya kuepuka mtu kuonekana wa kipekee, kwa kuwa kitendo hiki huvuta macho ya watu, na Rasuli amekataza kuvaa kivazi cha kuonekana mtu wa kipekee (cha umashuhuri).  Kitu chochote kinachomfanya mhusika wake kuonekana tofauti na wengine, basi kinastahiki kuepukwa.

 

6-  Mtu asilale chali na kuweka mguu mmoja juu ya mwingine kama hajavaa suruali ya ndani

 

Jaabir bin ‘Abdillaah:  “Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

 "لاَ يَسْتَلْقِيَنَّ أَحَدُكُمْ ثُمَّ يَضَعُ إِحْدَى رِجْلَيْهِ عَلَى الأُخْرَى"

 

“Asilale kabisa chali mmoja wenu kisha akaweka mguu wake mmoja juu ya mwingine”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Muslim (2099)].  

 

Wakati wa katazo hili unakuwa pale mtu anapokuwa hajavaa ndani suruali ya kusitiri uchi wake.  Abu Sa’iyd amesema:

 

"نَهَى رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَنْ يَحْتَبِيَ الرَّجُلُ فِي ثَوْبٍ وَاحِدٍ ، لَيْسَ عَلَى فَرْجِهِ مِنْهُ شَىْءٌ"

 

“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza mtu kukaa kikao cha “ihtibaa” akiwa na nguo moja tu, na hana chochote cha kusitiri utupu wake”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (367), An-Nasaaiy (5340), na Abu Daawuwd (3377).  Iliyoko kwa Al-Bukhaariy imetoka kwa Abu Hurayrah, na iliyoko kwa Muslim imetoka kwa Jaabir].

 

“Ihtibaa” ni kunyanyua mtu miguu yake miwili wakati amekaa, akaambatisha mapaja yake na tumbo lake na kifua, kisha akaizungushia nguo, au akaiviringisha mikono yake miwili au kishali.

 

Ama ikiwa amevaa nguo ya ndani ya kusitiri utupu wake, basi hakuna ubaya.  Imepokelewa toka kwa ‘Abdullaah bin Zayd kwamba:

 

"رَأَى رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ مُسْتَلْقِيًا فِي الْمَسْجِدِ وَاضِعًا إِحْدَى رِجْلَيْهِ عَلَى الأُخْرَى"

 

“Alimwona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa amelala chali Msikitini huku ameweka mguu wake mmoja juu ya mwingine”.   [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (475) na Muslim (2100)].

 

 

Share