03-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo Na Hukmu Za Kuangalia: Kivazi Cha Mwanamke: Masharti Ya Kivazi Cha Mwanamke Wa Kiislamu, Sharti La Pili

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ اللِّبَاسِ وَالزِّيْنَةِ  وَأَحْكَامُ النَّظَرِ

 

 Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo Na Hukmu Za Kuangalia 

  

لِبَاسُ المَرْأَةِ

Kivazi Cha Mwanamke 

 

Alhidaaya.com 

 

 

 

003-Masharti Ya Kivazi Cha Mwanamke Wa Kiislamu, Sharti La Pili:

 

Sharti la pili:

 

Vazi lenyewe lisiwe ni pambo.  Ni kwa Neno Lake Ta’aalaa:

 

"وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا"

 

“Na wala wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa yale yanayodhihirika”.  [An-Nuwr: 31].

 

Hii kwa ujumuishi wake, ni pamoja na nguo ya juu ikiwa ina mapambo yenye kuvuta macho ya wanaume.

 

Na kwa neno lake Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

"ثَلاَثَةٌ لاَ تَسْأَلْ عَنْهُمْ‏: رَجُلٌ فَارَقَ الْجَمَاعَةَ وَعَصَى إِمَامَهُ فَمَاتَ عَاصِيًا ، وَأَمَةٌ أَوْ عَبْدٌ أَبِقَ مِنْ سَيِّدِهِ فَمَاتَ ، وَامْرَأَةٌ غَابَ عَنْهَا زَوْجُهَا ، قدْ كَفَاهَا مَؤُونَةَ الدُّنْيَا فَتَبَرَّجَتْ بَعْدَهُ، فَلاَ تَسْأَلْ عَنْهُمْ‏"

 

“Watatu, usiwaulizie (adhabu inayowasubiri):  Ni mtu aliyetengana na umoja (wa nduguze Waislamu), akamwasi kiongozi wake na akafa akiwa mwasi, na kijakazi au mtumwa aliyetoroka kisha akafa, na mwanamke ambaye mumewe yuko mbali naye nailhali amemtosheleza mahitaji yake yote ya maisha, kisha akajishaua nyuma yake.  Hao usiwaulizie”.   [Fat-hul Bayaan (7/274)].

 

Makusudio ya kuamrishwa kuvaa jilbabu ni kuficha pambo la mwanamke, hivyo haiwezekani kiakili jilbabu lenyewe liwe ni pambo.

 

Angalizo:

 

Baadhi ya wanawake wanaowajibika kidini, wanadhani kwamba vazi lolote lisilo jeusi, basi linakuwa ni pambo.  Dhana hii ni kosa kwa sababu mbili:

 

Ya kwanza:  Kwa neno lake Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

 طِيبُ الْمَرْأَة ما ظَهَرَ لَوْنُهُ وَخَفِيَ رِيْحُهُ"

 

“Mafuta mazuri kwa mwanamke ni yale ambayo rangi yake inaonekana lakini harufu yake haisikiki.”  [Hadiyth Hasan Bitwuruqih.  Imekharijiwa na At-Tirmidhiy (2788) na Abu Daawuwd (2174)].

 

Ya pili:  Wanawake Maswahaba walizoeleka kuvaa nguo za rangi zisizo nyeusi.  Yafuatayo yanathibitisha hili:

 

1-  Hadiyth ya ‘Ikrimah:

 

"أَنَّ رِفَاعَةَ، طَلَّقَ امْرَأَتَهُ، فَتَزَوَّجَهَا عَبْدُ الرَّحْمَنِ بْنُ الزَّبِيرِ، قَالَتْ عَائِشَةُ وَعَلَيْهَا خِمَارٌ أَخْضَرُ‏.‏ فَشَكَتْ إِلَيْهَا، وَأَرَتْهَا خُضْرَةً بِجِلْدِهَا، فَلَمَّا جَاءَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَتْ عَائِشَةُ: مَا رَأَيْتُ مِثْلَ مَا يَلْقَى الْمُؤْمِنَاتُ، لَجِلْدُهَا أَشَدُّ خُضْرَةً مِنْ ثَوْبِهَا"

 

“Kwamba ‘Rifa’at alimpa talaka mkewe na ‘Abdulrahmaan bin Az-Zubayr akamwoa.  Bi ‘Aaishah anaeleza kwamba bi huyo alikuja kwake akiwa na mtandio wa kijani, akamshtakia na kumwonyesha alama za kijani kwenye ngozi yake (kutokana na kipigo).  Na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuja, ‘Aaishah alimwambia:  Sijapata kuona mfano wa mateso yanayowapata Waumini wanawake, ngozi yake imekuwa kijani kuliko mtandio wake”.  [Al-Bukhaariy (5825)].

 

2-  Hadiyth ya Ummu Khaalid bint Khaalid:

 

"أُتِيَ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ بِثِيَابٍ فِيهَا خَمِيصَةٌ سَوْدَاءُ صَغِيرَةٌ ، فَقَالَ: ‏مَنْ تَرَوْنَ نَكْسُو هَذِهِ؟ ‏فَسَكَتَ الْقَوْمُ ، قَالَ: ‏ائْتُونِي بِأُمِّ خَالِدٍ‏‏.‏ فَأُتِيَ بِهَا تُحْمَلُ فَأَخَذَ الْخَمِيصَةَ بِيَدِهِ فَأَلْبَسَهَا وَقَالَ: ‏ أَبْلِي وَأَخْلِقِي ‏"‏‏.‏ وَكَانَ فِيهَا عَلَمٌ أَخْضَرُ أَوْ أَصْفَرُ فَقَالَ: يَا أُمَّ خَالِدٍ هَذَا سَنَاهْ‏‏،  وَسَنَاهْ بِالْحَبَشِيَّةِ حَسَنٌ‏"

 

“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliletewa nguo likiwemo vazi dogo jeusi la khamiyswa, halafu akasema:  Mnaona tumvishe nani hili?  Watu wakanyamaza.  Akasema:  Basi nileteeni Ummu Khaalid.  Akaletewa akiwa amebebwa, akalichukua vazi akamvisha kwa mkono wake, kisha akamwombea du’aa akimwambia: Ulivae na uishi nalo muda mrefu lichakae hadi ulishone. Na vazi lilikuwa na mistari kijani au njano.  Halafu akamwambia:  Ee Ummu Khaalid!  Hili ni “sanah”, na “sanah” kwa Kihabeshi ni zuri, (yaani ni vazi zuri limekupendeza)”.  [Al-Bukhaariy (5823)].

 

3-  Al-Qaasim kasema: 

 

"أَنَّ عَائِشَةَ كَانَتْ تَلْبَسُ الثِّيَابَ الْمُعَصْفَرَةَ وَهِيَ مُحْرِمَةٌ" 

 

“ ’Aaishah alikuwa anavaa nguo ya rangi ya kinjano akiwa amehirimia”.  [Ibn Abiy Shaybah (8/372) kwa Sanad Swahiyh].

 

Ninasema:

 

1-  Ilivyo ni kwamba nguo ambayo yenyewe ni pambo, ni ile iliyofumwa kwa rangi mbalimbali, au yenye nakshi za rangi ya dhahabu au silva, inayovuta macho ya akina baba na kuyazimua.

 

2-  Vazi jeusi ndilo bora zaidi kwa wanawake na lenye sitara zaidi, nalo ndilo vazi la wake wa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama alivyoeleza Bibi ‘Aaishah kwenye Hadiyth kuhusiana na yeye kuonwa na Swafwaan ambapo anasema:

 

"فَرَأَى سَوَادَ إِنْسَانٍ نَائِمٍ"

“Akaona weusi wa kiwiliwili cha mtu aliyelala”.

 

Na pia Hadiyth nyingine ya ‘Aaishah kuhusu kutoka kwa wanawake wa Ki-Answaar, anasema: 

 

"كَأَنَّ عَلى رُؤُوسِهِنَّ الغِرْبِانُ"

 

“Kana kwamba kuna kunguru juu ya vichwa vyao”.  [Swahiyh Muslim (2128)].

 

 

 

Share