04-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo Na Hukmu Za Kuangalia: Kivazi Cha Mwanamke: Masharti Ya Kivazi Cha Mwanamke Wa Kiislamu, Sharti La Tatu Na La Nne

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ اللِّبَاسِ وَالزِّيْنَةِ  وَأَحْكَامُ النَّظَرِ

 

 Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo Na Hukmu Za Kuangalia 

  

لِبَاسُ المَرْأَةِ

Kivazi Cha Mwanamke 

 

Alhidaaya.com 

 

 

 

004-Masharti Ya Kivazi Cha Mwanamke Wa Kiislamu, Sharti La Tatu Na La Nne:

 

Sharti la tatu:

 

Nguo iwe nzito isiyoonyesha rangi ya ngozi ya mwili.  Hii ni kwa Hadiyth iliyotangulia ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

"صِنْفَانِ مِنْ أَهْلِ النَّارِ لَمْ أَرَهُمَا: قَوْمٌ مَعَهُمْ سِيَاطٌ كَأَذْنَابِ الْبَقَرِ يَضْرِبُونَ بِهَا النَّاسَ ، وَنِسَاءٌ كَاسِيَاتٌ عَارِيَاتٌ مُمِيلَاتٌ مَائِلَاتٌ رُؤُوْسُهُنَّ كَأَسْنِمَةِ الْبُخْتِ الْمَائِلَةِ ، لَا يَدْخُلْنَ الْجَنَّةَ وَلَا يَجِدْنَ رِيحَهَا ، وَإِنَّ رِيحَهَا لَتُوجَدُ مِنْ مَسِيرَةِ كَذَا وَكَذَا"

 

Sampuli mbili za watu wa motoni sijaziona bado:  Watu wenye mijeledi mithili ya mikia ya ng’ombe wanawapiga nayo watu (bila haki), na wanawake waliovaa lakini kiuhalisia wako uchi, wanawashawishi wenzao kuwa kama wao (au kuwasisimua wanaume), na wanatembea kwa maringo wakipindisha mabega yao, vichwa vyao ni kama nundu za ngamia zilizoinama.  Hao hawaingii Peponi na hawatoipata harufu yake, na kwa hakika harufu yake inasikika toka mwendo kadha wa kadha”.  [Swahiyh Muslim (2128)].

 

Wanaokusudiwa hapa ni wanawake wanaovaa nguo nyepesi zinazoonyesha mwili badala ya kuusitiri, au nguo fupi, au zenye kubana mwili, wao kwa jina wamevaa, lakini kiuhalisia wako uchi.

 

Sharti la nne:

 

Nguo iwe pana, isiwe inabana ikaonyesha mikatiko ya mwili wake. 

 

Usaamah bin Zayd  anahadithia: 

 

"كَسَانِي رَسُولُ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قُبْطِيَّةً كَثِيفَةً كَانَتْ مِمَّا أَهْدَاهَا دِحْيَةُ الْكَلْبِيُّ، فَكَسَوْتُهَا امْرَأَتِي، فَقَالَ لِي رَسُولُ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: " مَا لَكَ لَمْ تَلْبَسِ الْقُبْطِيَّةَ؟ " قُلْتُ: يَا رَسُولَ اللهِ، كَسَوْتُهَا امْرَأَتِي. فَقَالَ لِي رَسُولُ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: (مُرْهَا فَلْتَجْعَلْ تَحْتَهَا غِلَالَةً، إِنِّي أَخَافُ أَنْ تَصِفَ حَجْمَ عِظَامِهَا"                        

 

“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alinivalisha  “qubtwiyyah” zito ambalo alikuwa amepewa zawadi na Dihyatul Kalbiyy, nami nikamvisha mke wangu.  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliponiona akaniambia:  Vipi? Mbona hukuvaa “qubtwiyyah”? Nikamwambia:  Ee Rasuli wa Allaah, nimemvalisha mke wangu.  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaniambia:  Mwamuru avalie ndani yake nguo nyingine, kwani nahofia “qubtwiyyah” litaonyesha mifupa yake ilivyo”.   [Ahmad (5/205) kwa Sanad Layyin.  Ina Hadiyth mwenza kwa Abu Daawuwd (4116) ambayo kwayo inafanywa Hadiyth Hasan].

 

“Qubtwiyyah” ni vazi la zamani la Kimisri.  

 

Kwa dada zetu wa Kiislamu katika zama zetu za leo, tunapenda kuwaambia kwamba haitoshi ukasitiri tu nywele zako na shingo yako, kisha bila kujali baada ya hapo, ukavaa nguo za kubana na fupi zisizovuka nusu muundi.  Na jueni kwamba haitoshi kuvaa soksi kwenye miundi miwili iliyo wazi.  Jilazimisheni kuwa na pupa ya kukamilisha sitara kama Alivyoamuru Allaah Ta’aalaa na kuwaiga pia wanawake wenzenu waliohamia mwanzo Madiynah (Muhaajiraat) wakati ilipoteremka amri ya kuteremsha shungi zao.  Hapo hapo walipasua mitandio yao wakajifunika nayo.  Na sisi hatuwatakeni mpasue nguo zenu zozote, bali tunawatakeni mrefushe nguo zenu na mzitanue ili ziwe ni kivazi chenye kusitiri mwili wote ambao Allaah Amewaamuru kuusitiri.  [Ni maneno ya Al-‘Allaamah Al-Albaaniy kuhusu jilibabu].

 

 

 

Share