09-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo Na Hukmu Za Kuangalia: Kivazi Cha Mwanamke: Mwanamke Kuvaa Suruali
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ اللِّبَاسِ وَالزِّيْنَةِ وَأَحْكَامُ النَّظَرِ
Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo Na Hukmu Za Kuangalia
لِبَاسُ المَرْأَةِ
Kivazi Cha Mwanamke
009- Kivazi Cha Mwanamke: Mwanamke Kuvaa Suruali:
Suruali ni mtihani mbaya zaidi uliowakumba wanawake wengi (Allaah Awahidi). Ingawa suruali zao zinasitiri uchi, lakini wakati huo huo zinakuwa zikitoa umbile la mwanamke kwa picha ya kuchemsha matamanio ya wanaume na hususan zinapokuwa na rangi tofauti, miundo na aina. Na dada zetu wa Kiislamu, bila shaka mmeshajua kwamba miongoni mwa shuruti za hijabu ya kisharia ni isiwe nguo yenye kubana mwili kiasi cha kuonyesha maungo ya kuvutia ya mwili. Imekuwa suruali kwa sasa ndio yenye uchochezi na fitnah zaidi kuliko nguo fupi, ima kwa kuwa kwake inabana sana, au kwa kuwa sawa na rangi ya ngozi ya mwili kiasi cha kuonekana kama hakuvaa kitu. Huu ni uovu mbaya ulioenea, na kwa ajili hiyo, haifai mwanamke kuvaa suruali isipokuwa kama atamvalia mumewe lakini kwa sharti kwamba isifanane na ya wanaume, na wala asitoke nayo mbele ya maharimu zake wala watu ajinabi. Pamoja na hayo yote, hakuna ubaya akivaa suruali ndani ya abaya linalomsitiri, kwani itamsitiri asionekane mwili na hususan wakati anapopanda gari na mfano wake. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.
Je, Mwanamke Anaruhusiwa Kuvaa Viatu Vya Visigino Virefu?
Ibn Mas-‘uwd amesema:
"كَانَ الرِّجَالُ وَالنِّسَاءُ في بَنِيْ إِسْرَائِيْلَ يُصَلُّونَ جَمِيْعًا، فَكَانَتِ المَرْأَةُ لَهَا الخَلِيْلُ تَلْبَسُ القَالِبَيْنِ تَطُوْلُ بِهِمَا لِخَلِيْلِهَا، فَأُلْقِيَ عَلَيْهِنَّ الحَيْضُ". فَكَانَ ابنُ مَسْعُودِ يَقُوْلُ: "أَخْرِجُوهُنَّ حَيْثُ أَخْرَجَهُنَّ اللهُ"
“Wanaume na wanawake wa Kinabiy Israaiyl walikuwa wanaswali wote kwa pamoja. Akawa mwanamke mwenye mpenzi wake anavaa viatu vya mbao vya soli ndefu vinavyomfanya aonekane mrefu kwa mpenzi wake. Na kwa sababu hiyo, wakateremshiwa hedhi.” Na akawa Ibn Mas-‘uwd anasema: “Wawekeni nyuma pale ambapo Allaah Amewaweka”. [Muswannafu ‘Abdulrazzaaq (5115) na Sanad yake ni Swahiyh].
Linaloonekana kuhusiana na visigino virefu ni kwamba ikiwa mwanamke atavaa ili achomoze kwa wanaume na wanaume wapate kumwona, basi itakuwa ni haramu, kwa kuwa viatu hivyo vya visigino virefu katika hali hii, vitakuwa ndiyo sababu ya uharibifu na uenezaji wa maasia. [Jaami’u Ahkaamin Nisaa (4/434)].
Ninasema: “Kuongezea na haya, kuvaa viatu vya visigino virefu kunaufanya mwendo wa mwanamke na miondoko yake kuwa yenye kuvutia macho ya wanaume, mbali na sauti yake ambayo pia inawababaisha. Na kwa msingi huu, mwanamke hatakiwi avae viatu hivi anapotoka nyumbani kwake”.