10-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo Na Hukmu Za Kuangalia: Kivazi Cha Mwanamke: Kivazi Cha Mwanamke Mbele Ya Maharimu Zake

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ اللِّبَاسِ وَالزِّيْنَةِ  وَأَحْكَامُ النَّظَرِ

 

 Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo Na Hukmu Za Kuangalia 

  

لِبَاسُ المَرْأَةِ

Kivazi Cha Mwanamke 

 

Alhidaaya.com 

 

 

 

 

010- Kivazi Cha Mwanamke Mbele Ya Maharimu Zake:

 

Kabla hatujaelezea sehemu ya mwili ambayo inajuzu kwa mwanamke kuiwacha wazi mbele ya maharimu zake, ingelipendeza kwanza tumjue mahram ni nani. 

 

Mahram ni kila mwanaume ambaye ni haramu kwake kumwoa mwanamke uharamu wa milele kutokana na kuwepo sababu halali ya kuzuia hilo.  Mahram huyu, anaruhusiwa kumwangalia mwanamke huyu, kukaa naye peke yake na kusafiri pamoja naye.  Tukisema “Uharamu wa milele”, tunamtoa nje ya duara hili dada ya mke, shangazi yake, khalati yake na mfano wao, kwani hawa uharamu wao ni wa muda.  [Sharhu Muslim cha An-Nawawiy (3/484)].

 

Allaah Ta’aalaa Anasema:

 

"وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا لِبُعُولَتِهِنَّ أَوْ آبَائِهِنّ"

 

“Na wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa kwa waume zao, au baba zao”.  [An-Nuwr: 31].

 

Aayah hii inaruhusu maharimu kuangalia sehemu za mapambo ya mwanamke, kwa kuwa dharura inalazimisha kuchanganyika, kuweko maingiliano, mapishano na matangamano ambayo huwafanya  waonane mara nyingi na waangaliane kutokana na ukaraba.  Isitoshe, fitnah baina yao iko mbali.

 

Katika aayah hii, Allaah Ta’aalaa Ameanza na waume kisha maharimu wengineo.  Maharimu hawa kiujumla ni hawa wafuatao:

 

1-  Baba na pia mababu, ni sawa wa upande wa baba au wa mama.

 

2-  Baba wa mke (baba mkwe).

 

3-  Watoto wao wa kiume na watoto wa kiume wa waume zao.  Hapa wanaingia pia wajukuu na kwenda chini.

 

4-  Makaka zake (ndugu zake wa kiume), ni sawa wawe wa tumbo moja baba na mama, au kwa baba tu, au kwa mama tu, na hata wakienda chini.

 

5-  Watoto wa kiume wa kaka au wa dada, kwa kuwa hawa ni makaka, wote ni ndugu.

 

6-  Maami (baba wadogo) na wajomba, hawa ni maharimu ingawa hawakutajwa katika Aayaah tukufu.  Jumhuwr ya ‘Ulamaa  wanasema kuwa hukmu ya hawa ni sawa na maharimu wengineo, na ushahidi wake ni Hadiyth ya ‘Aaishah:

 

"أَنَّ أَفْلَحَ أَخَا أَبِي الْقُعَيْسِ، جَاءَ يَسْتَأْذِنُ عَلَيْهَا وَهُوَ عَمُّهَا مِنَ الرَّضَاعَةِ بَعْدَ أَنْ أُنْزِلَ الْحِجَابُ قَالَتْ فَأَبَيْتُ أَنْ آذَنَ لَهُ فَلَمَّا جَاءَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَخْبَرْتُهُ بِالَّذِي صَنَعْتُ فَأَمَرَنِي أَنْ آذَنَ لَهُ عَلَىَّ"

 

“Kwamba kaka wa Aflah Al-Qu’ays ambaye ni ami yake kwa kunyonya, alikuja na kumbishia hodi baada ya kushuka Aayaah ya hijab ya kuwaamuru wake za Nabiy kuweka pazia wasionwe na wanaume.  ‘Aaishah anasema:  Nilikataa kumfungulia mlango.  Na alipokuja Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) nilimweleza jambo nililolifanya, naye akaniamuru nimfungulie mlango akija”.  [Al-Bukhaariy (5103) na Muslim (1445)].

 

7-  Maharimu wa kunyonya, na hawa pia hawakutajwa kwenye Aayah.  ‘Ulamaa pia wamekubaliana kuwa hawa ni kama maharimu wengineo, na hii ni kwa Hadiyth ya ‘Aaishah iliyotajwa hapo juu.

 

 

 

Share