11-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo Na Hukmu Za Kuangalia: Kivazi Cha Mwanamke: Ni Kiasi Gani Cha Mwili Wake Ambacho Mwanamke Anaweza Kukiachilia Mbele Ya Maharimu Wake?

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ اللِّبَاسِ وَالزِّيْنَةِ  وَأَحْكَامُ النَّظَرِ

 

 Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo Na Hukmu Za Kuangalia 

  

لِبَاسُ المَرْأَةِ

Kivazi Cha Mwanamke 

 

Alhidaaya.com 

 

 

 

011-Ni Kiasi Gani Cha Mwili Wake Ambacho Mwanamke Anaweza Kukiachilia Mbele Ya Maharimu Wake?

 

‘Ulamaa wana kauli mbili mashuhuri kuhusiana na hili:

 

Ya kwanza:   Maharimu wanaruhusiwa kuangalia mwili wote wa mwanamke isipokuwa sehemu iliyo kati ya kitovu na magoti.  Hii ni kauli ya madhehebu ya Jumhuwr.  Dalili ni:

 

1-   Neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

"..وَإِذَا أَنْكَحَ أَحَدُكُمْ عَبْدَهُ أَوْ أَجِيْرَهُ فَلَا يَنْظُرَنَّ مِنْ عَوْرَتِهِ، فَإِنَّ مَا أَسْفَلَ مِنْ سُرَّتِهِ إِلَى رُكْبَتَيْهِ من عَوْرَتِهِ"

 

“Na anapomwozesha mmoja wenu mtumwa wake au mtumishi wake, basi asiangalie sehemu yoyote ya uchi wake, kwa kuwa sehemu iliyo chini ya kitovu chake hadi kwenye magoti yake ni uchi wake”.  [Ahmad (2/187) na Abu Daawuwd (495) kwa Sanad Hasan].

 

Hadiyth hii ingawa inawahusu wanaume ila ni kwamba wanawake ni ndugu moja na wanaume.

 

2-  Hadiyth ya Abuu Salamah:

 

"دَخَلْتُ أَنَا وَأَخُو عَائِشَةَ عَلَى عَائِشَةَ فَسَأَلَهَا أَخُوهَا عَنْ غُسْلِ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ، فَدَعَتْ بِإِنَاءٍ نَحْوًا مِنْ صَاعٍ، فَاغْتَسَلَتْ وَأَفَاضَتْ عَلَى رَأْسِهَا، وَبَيْنَنَا وَبَيْنَهَا حِجَابٌ‏"

 

“Niliingia mimi pamoja na kaka yake ‘Aaishah kwa ‘Aaishah.  Kaka yake akamuuliza namna Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anavyofanya ghuslu (ya janaba).  Akaagiza aletewe maji kwenye chombo cha kiasi cha pishi, akaoga na kisha akajimiminia juu ya kichwa chake huku kikiweko kizuizi kati yetu na yeye”.  [Al-Bukhaariy (251) na Muslim (320)].

 

Al-Qaadhiy ‘Ayyaadh amesema:  “Inavyoonekana ni kwamba wawili hao waliona anavyofanya kwenye kichwa chake na sehemu ya juu ya mwili wake inayoruhusika kuonwa na mahram, kwa kuwa Bibi ‘Aaishah ni khalati ya Abu Salamah kwa kunyonya.  Bibi ‘Aaishah alisitiri sehemu ya chini ya mwili wake ambayo si halali kwa mahram kuiona”.

 

Kauli ya pili:  Maharimu wanaruhusiwa kuangalia sehemu ambayo kikawaida inakuwa wazi kwa mwanamke kama viungo vya wudhuu.  [Sunan Al-Bayhaqiy (9417), Al-Inswaaf (8/20), Al-Mughniy (6/554) na Al-Majmuw’u (16/140)].

 

Ibn ‘Umar amesema: 

 

"كَانَ الرِّجَالُ وَالنِّسَاءُ يَتَوَضَّئُونَ فِي زَمَانِ رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ جَمِيعًا"

 

“Wanaume na wanawake walikuwa wakitawadha wote kwa pamoja enzi ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam”.  [Al-Bukhaariy (193), Abu Daawuwd (79), An-Nasaaiy (1/57) na Ibn Maajah (381)].

 

Na hili linachukulika kama linawahusu wake na maharimu.  Na kwa muktadha huu, kuna dalili ya kujuzu mwanamume kuangalia sehemu za kutiwa maji ya wudhuu ya maharimu zake na kinyume chake.  Allaah Ndiye Mjuzi zaidi.

 

Maangalizo:

 

1-  Kwa mujibu wa maelezo yaliyotangulia, ruksa ya maharimu kumwangalia mwanamke inashurutishwa kwamba kuangalia kwenyewe kusiwe kwa njia ya matamanio, au kuhisi utamu, au burudiko.  Ikiwa haya yatakuwepo, basi hakuna shaka kwamba itakuwa hairuhusiwi.

 

2-  Baadhi ya ‘Ulamaa wametofautisha baina ya baadhi ya maharimu kingazi kwa ambayo mwanamke anaweza kuyaonyesha kwa mujibu wa yaliyomo ndani ya nafsi za watu.  Hakuna shaka yoyote kwamba sehemu ya mwili ambayo mwanamke anaiacha wazi mbele ya baba yake au kaka yake, haiwi sawa mbele ya mtoto wa kiume wa mumewe, kwani huyu inabidi kuweko hadhari na sitara zaidi.  Hivyo, ngazi za sehemu ya kuonekana ya mwili wake zinatofautiana.  Kwa baba yake, atawacha wazi sehemu ambazo haruhusiwi kuziacha wazi mbele ya mtoto wa kiume wa mume wake.  Haya yamesemwa na Al-Qurtubiy.  [Yameelezwa haya pia na Sheikh wetu katika kitabu cha Jaami’u Ahkaamin Nisaa (4/504), kisha akasema: “Haya yanakubalika kwa upande wa mwono, lakini yanahitaji dalili ya kuyathibitisha”]. 

 

 

 

Share