12-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo Na Hukmu Za Kuangalia: Kivazi Cha Mwanamke: Mahram Anaruhusiwa Kumgusa Mwanamke Na Kumbusu Ikiwa Si Kwa Matamanio
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ اللِّبَاسِ وَالزِّيْنَةِ وَأَحْكَامُ النَّظَرِ
Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo Na Hukmu Za Kuangalia
لِبَاسُ المَرْأَةِ
Kivazi Cha Mwanamke
012-Mahram Anaruhusiwa Kumgusa Mwanamke Na Kumbusu Ikiwa Si Kwa Matamanio
Katika Hadiyth ya ‘Aaishah kuhusiana na yeye kumkasirikia ‘Abdullaah bin Az-Zubayr ambaye ni mtoto wa dada yake Asmaa, akaweka nadhiri kwamba hatomsemesha, na kisha ‘Abdullaah bin Az-Zubayr kumwomba na kumsihi aseme naye. (Na hii ni baada ya kupangwa namna ya kuwasuluhisha. Mpango ulipokuwa tayari, ‘Abdullaah bin Az-Zubayr alikwenda kwa ‘Aaishah pamoja na watu wawili, wakagonga mlango na) ‘Aaishah akasema:
"ادْخُلُوا كُلُّكُمْ -ولا تَعْلَمُ أّنَّ مَعَهُمَا ابنُ الزُّبَيْرِ- فَلَمَّا دّخَلُوا دَخَلَ ابن الزُّبِيْرِ الحِجَابَ فَاعْتَنَقَ عَائِشَةَ وطَفِقَ يُنِاشِدُهَا ويَبْكِيْ..."
“Ingieni nyote -naye hajui kwamba wako pamoja na ‘Abdullaah bin Az-Zubayr-. Walipoingia, ‘Abdullaah bin Az-Zubayr akaingia ndani ya pazia, akamkumbatia ‘Aaishah, na akaanza kumsihi na kumwomba (aachane na msimamo wake) huku analia. [Al-Bukhaariy (6073)].
Na pia ‘Aaishah amesema:
"..كَانَتْ إِذَا دَخَلَتْ عَلَيْهِ قَامَ إِلَيْهَا النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ ، فَأَخَذَ بِيَدِهَا وَقَبَّلَهَا وَأَجْلَسَهَا فِي مَجْلِسِهِ، وَكَانَ إِذَا دَخَلَ عَلَيْهَا قَامَتْ إِلَيْهِ فَأَخَذَتْ بِيَدِهِ، فَقَبَّلَتْهُ، وَأَجْلَسَتْهُ فِي مَجْلِسِهَا"
“Alikuwa (Faatwimah) anapoingia, Rasuli humsimamia, akaukamata mkono wake, akambusu na kumkalisha sehemu yake anakoketi. Naye (Faatwimah) kwa upande wake, Rasuli anapoingia kwake, humsimamia, akaukamata mkono wake, akambusu na akamkalisha sehemu yake anakoketi”. [Abu Daawuwd (5217), At-Tirmidhiy (3872) na Al-Haakim (4/272). Ni Hadiyth Swahiyh].