15-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo Na Hukmu Za Kuangalia: Kivazi Cha Mwanamke: Je, Mwanamke Wa Kiislamu Anaruhusiwa Kuonyesha Mapambo Yake Kwa Mwanamke Kafiri?
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ اللِّبَاسِ وَالزِّيْنَةِ وَأَحْكَامُ النَّظَرِ
Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo Na Hukmu Za Kuangalia
لِبَاسُ المَرْأَةِ
Kivazi Cha Mwanamke
015-Je, Mwanamke Wa Kiislamu Anaruhusiwa Kuonyesha Mapambo Yake Kwa Mwanamke Kafiri?
Kundi la baadhi ya ‘Ulamaa wanaona kwamba haijuzu kwa mwanamke kuonyesha mapambo yake kwa wanawake wasio wa Kiislamu ili wasije kwenda kuelezea na kusifu waliyoyaona kwa waume zao. Na hii ni kwa Neno Lake Ta’aalaa: أَوْ نِسَائِهِنَّ “au wanawake wenzao” ambao ni wanawake wa Kiislamu. Na kwa hivyo, wanatoka nje ya duara hili wanawake wa kipagani ikiwa ni pamoja na wanaoishi chini ya ulinzi wa dola ya Kiislamu (dhimmiyyaat) na wengineo.
Ama ‘Ulamaa wengineo, hao wanaona kwamba hilo linajuzu, na kwamba hakuna tofauti kati ya mwanamke wa Kiislamu na mwanamke wa kidhimmiyat katika kumwangalia mwanamke mwenzake. Dalili yao wanasema kwamba wanawake makafiri wa Kiyahudi walikuwa wakiingia kwa wake za Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na wala hawakuwa wanajifunika, na hawakuamrishwa pia kujifunika. Bibi ‘Aaishah amesema:
"أَنَّ يَهُودِيَّةً دَخَلَتْ عَلَيْهَا فَذَكَرَتْ عَذَابَ الْقَبْرِ فَقَالَتْ لَهَا أَعَاذَكِ اللَّهُ مِنْ عَذَابِ الْقَبْرِ ، فَسَأَلَتْ عَائِشَةُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ عَنْ عَذَابِ الْقَبْرِ فَقَالَ: نَعَمْ عَذَابُ الْقَبْر ، قَالَت عَائِشَة رَضِي الله عَنْهَا: فَمَا رَأَيْتُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ بعد صلى صَلَاة إِلَّا تَعَوَّذَ مِنْ عَذَابِ الْقَبْر"
“Kwamba mwanamke mmoja wa Kiyahudi alimtembelea na akamwelezea adhabu ya kaburi, halafu akamwambia (akimwombea): Allaah Akulinde na adhabu ya kaburi. ‘Aaishah baadaye akaja kumuuliza Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu adhabu ya kaburi, naye akamjibu: Na’am, adhabu ya kaburi iko. ‘Aaishah anaendelea kusema: Sikumwona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya Swalaah yoyote anayoiswali, isipokuwa anajilinda kwa Allaah na adhabu ya kaburi”. [Al-Bukhaariy (1372) na Muslim (903)].
Asmaa amesema:
"إِنَّ أُمِّي قَدِمَتْ عَلَىَّ وَهِىَ رَاغِبَةٌ ، فَسَأَلْتُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ : أَفَأَصِلُهَا؟ قَالَ: نَعَمْ "
“Mama yangu alikuja kunitembelea naye amekakasika na Uislamu, nikamuuliza Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam): Je, niendelee kutangamana naye kwa wema? Akasema: Na’am”. [Al-Bukhaariy (2620) na Muslim (1003)].
Ninasema: “Ikiwa mwanamke wa Kiyahudi au Kinaswara atashukiwa kwamba anamweleza mumewe anayoyaona kwa mwanamke wa Kiislamu, basi mwanamke wa Kiislamu ajizuie kuonyesha mapambo yake kwake. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”.