16-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo Na Hukmu Za Kuangalia: Kivazi Cha Mwanamke:Kivazi Cha Mwanamke Mbele Ya Mtumwa Wake
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ اللِّبَاسِ وَالزِّيْنَةِ وَأَحْكَامُ النَّظَرِ
Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo Na Hukmu Za Kuangalia
لِبَاسُ المَرْأَةِ
Kivazi Cha Mwanamke
016-Kivazi Cha Mwanamke Mbele Ya Mtumwa Wake:
‘Ulamaa wengi wanaona kwamba mtumwa anayemilikiwa na mwanamke anakuwa ni kama mahramu yake, anaweza kumwangalia yale anayoyaangalia mahramu. Dalili yao ni Kauli Yake Ta’aalaa:
"وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا ۖ وَلْيَضْرِبْنَ بِخُمُرِهِنَّ عَلَىٰ جُيُوبِهِنَّ ۖ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا لِبُعُولَتِهِنَّ أَوْ آبَائِهِنَّ أَوْ آبَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ أَبْنَائِهِنَّ أَوْ أَبْنَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي أَخَوَاتِهِنَّ أَوْ نِسَائِهِنَّ أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُنَّ"
“Na wala wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa yale yanayodhihirika. Na waangushe khimaar (shungi) zao mpaka vifuani mwao, na wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa kwa waume zao, au baba zao, au baba za waume wao, au wana wao wa kiume, au wana wa kiume wa waume zao, au kaka zao, au wana wa kiume wa kaka zao, au wana wa kiume wa dada zao, au wanawake wao (wa Kiislamu), au wale iliyowamiliki mikono yao ya kuume”. [An-Nuwr: 31].
Wamesema: Kauli Yake أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُنَّ “au wale iliyowamiliki mikono yao ya kuume”, inawahusu watumwa wa kiume na vijakazi, na haiwezekani kauli hii ikawahusu vijakazi, kwa kuwa hilo limetajwa kabla ya hapo katika Kauli Yake Ta’aalaa أَوْ نِسَائِهِنَّ “au wanawake wenzao”. [Al-Mabsuwtw (10/157)].
Na pia Hadiyth ya Anas:
"أَنَّ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَتَى فَاطِمَةَ بِعَبْدٍ قَدْ وَهَبَهُ لَهَا، قَالَ: وَعَلَى فَاطِمَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا ثَوْبٌ، إِذَا قَنَّعَتْ بِهِ رَأْسَهَا لَمْ يَبْلُغْ رِجْلَيْهَا، وَإِذَا غَطَّتْ بِهِ رِجْلَيْهَا لَمْ يَبْلُغْ رَأْسَهَا، فَلَمَّا رَأَى النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ مَا تَلْقَى قَالَ: إِنَّهُ لَيْسَ عَلَيْكِ بَأْسٌ إِنَّمَا هُوَ أَبُوكِ وَغُلاَمُكِ "
“Kwamba Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimletea Faatwimah mtumwa ambaye alikuwa amemzawadia, na Faatwimah amevaa nguo ambayo akijifunika kichwa chake haifiki chini ikafunika miguu, na akijifunika nayo miguu, basi haifiki kichwani. Rasuli alipoona Faatwimah anavyohangaika alimwambia: Usitaabike, hakuna neno, ni mimi hapa baba yako na mtumwa wako”. [Abu Daawuwd (4106) na Al-Bayhaqiy (7/95). Ni Hadiyth Hasan].
Sheikh wa Uislamu amerajihisha kujuzu mtumwa kumwangalia bibi anayemmiliki kwa ajili ya haja, kwa kuwa bibi huyu anahitaji kuzungumza na mtumwa wake zaidi ya anavyohitajia kuonwa na shuhuda, au mwenye kufanya naye miamala au anayemsemesha. Na hawa kama wanaruhusiwa kumwangalia, basi mtumwa wake ana haki zaidi ya kumwangalia. [Majmuw’ul Fataawaa (16/141)].